Kumbuka Kubembelezwa Sana Siyo Kupendwa-2

Tumshukuru Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia pumzi na kuiona siku hii njema ya Jumatatu. Karibu mpenzi msomaji wangu wa safu hii ya XXLove ambaye umekuwa ukifuatilia mada zangu pamoja na kutoa maoni mbalimbali.

Wiki iliyopita tulizungumza namna ambavyo baadhi ya watu hujikuta wanaingia kwenye uhusiano wa kimapenzi na wenza wasiokuwa na mapenzi ya dhati bali hutumia ulaghai wa kubembeleza na kupetipeti kinafiki.
Niliahidi kupokea maoni ya wasomaji wa safu hii na wiki hii kuyachapisha maoni yao kwa lengo la kujifunza zaidi kama ifuatavyo;

AISHA

Nimesoma Makala ya XXLove kuhusu Kubembelezwa Sana Siyo Kupendwa, binafsi naamini katika hilo kwa sababu nina mpenzi wangu, yeye hanibembelezi sana ila kila ninachohitaji ananisaidia na kama nikilalamika huwa ananiambia najichanganya mwenyewe kwani yeye ananipenda kwa dhati.

MSOMAJI
Mada yako imenigusa sana, mimi nimeolewa mke wa pili (mke mdogo), mume wangu hajalala nyumbani kwangu takriban miezi 10 sasa ila kila kitu ananipa, nikimwambia suala la kulala kwangu anaanza kunibembeleza mpaka nakubali ingawa namuhitaji zaidi yeye.

MSOMAJI

Nawashukuru sana kwa kuandika mada za uhusiano, naomba muandike mada za kuwaelimisha zaidi wanawake, namna ya kuwahudumia waume zao, kwani wengi hawajui na hujikuta wakiachika.

EVODEAR WELL, NJOMBE
Kubembelezwa ni kuzuri lakini ni kubaya pia kama utampata mpenzi tapeli. Wasichana wengi wanajisahau kwa kubembelezwa na kuhisi wao ndiyo wenye bahati kuliko wengine ila siku ikitokea wakitendwa au kuumizwa, wanaumia na kujutia sana, ushauri wangu kubembelezwa sana siyo ishara ya mapenzi ya ukweli.

NYAMONG’ONG’ANA KIKEKARAMBWE
Nina mpenzi wangu nampenda sana tatizo lake anapenda sana kubembelezwa wakati mimi siyo mbembelezaji, ni mpendaji, najua tatizo la wanawake wakibembelezwa sana wanajisahau na kuanza kejeli.

Kimsingi iko hivi; ni kweli mapenzi yanahitaji kubembelezwa ili anayebembelezwa aone thamani ya yeye kuwa karibu na mpenzi wake. Ingawa ni kweli kuna watu ambao siyo wabembelezaji bali ni watu wa kupenda kiukweli, sema tafsiri ya kupendwa kwa walio wengi wanafahamu ni kubembelezwa.

Ushauri wangu, kabla watu hawajaingia kwenye uhusiano ni vizuri sana wakafahamiana kwa muda ili kila mtu amfahamu mwenza wake ni mtu mwenye tabia zipi, hata kama wakiamua kuingia kwenye uhusiano kila mtu anakuwa anamfahamu mwenza wake vizuri.

Tukutane wiki ijayo kwenye mada nyingine tamu, pia usikose kutembelea ukurasa wetu wa Mimi na Uhusiano kwenye Mtandao wa Facebook na Instagram kwa elimu zaidi kuhusu mapenzi.


Loading...

Toa comment