The House of Favourite Newspapers

Kumekucha Uchaguzi 2020… Mastaa Kibao Wajitosa Ubunge

0

WIMBI la watu maarufu kujitosa kwenye mbio za siasa mwaka huu, limeanza kuchanua kadiri siku zinavyosonga baada ya kundi kubwa la wasanii kujitokeza kuwania ubunge katika majimbo mbalimbali nchini.Hatua hiyo imekuja kipindi hiki ambacho wimbi la vijana wameamka na kushika hatamu katika nafasi mbalimbali ndani ya Serikali inayoongozwa na Rais Dk John Pombe Magufuli.

 

Aidha, katika uchaguzi mkuu uliopita, wabunge ambao ni manguli wa fani ya sanaa, Joseph Haule ‘Profesa Jay’ (Mikumi – Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ (Mbeya Mjini – Chadema), wamedaiwa kuwa kivutio cha kipekee kwa mastaa wenzao ambao nao katika uchaguzi huu, wamenuia kutobaki nyuma.Wafuatao ni Mastaa kutoka tasnia ya sanaa nchini ambao wametangaza nia za kugombea ubunge katika majimbo mbalimbali;

Zuwena Mohammed maarufu Shilole.

HARMONIZE

Mkurugenzi (CEO) wa Lebo ya Konde Gang World Wide Music, Rajab Abdul ‘Harmonize, amejitosa kugombea Ubunge huko Tandahimba mkoani Mtwara kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).Juni 14, katika mahojiano na chombo kimoja cha habari, Harmonize alifunguka kugombea baada ya Rais Magufuli, kumpendekeza msanii huyo kuwania ubunge jimboni huko.

 

SHILOLE

Mwanamama mwenye harakati nyingi hapa mjini na msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Zuwena Mohammed maarufu Shilole, alitangaza rasmi kugombea ubunge Igunga kupitia tiketi ya CCM.

 

Shilole ambaye kwa sasa anatikisa na ngoma ya Pindua Meza, Januari mwaka huu alitangaza kugombea katika Jimbo la Igunga, mkoani Tabora.Shilole aliandika waraka katika ukurasa wake wa Instagram kuwa “Mimi Shishi, ambaye ni mbunge kivuli wa muda mrefu na wa kujitolea katika jimbo langu la Igunga na ambaye sipo rasmi bungeni kwa sasa…

 

“Naisubiria kwa hamu siku isiyokuwa na tarehe, lakini ni mwezi wa 10, Jumapili moja hivi asubuhi ya mwaka huu 2020, baada ya ibada ya kwanza, ni siku ambayo nitatangazwa rasmi kama Mbunge mwakilishi wa Igunga.“Nimefanikiwa kuiweka Igunga kwenye ramani nzuri ya Tanzania, bila ya kuwa mbunge rasmi, hivyo sitashindwa kuifanyia maendeleo Igunga yangu nikiwa mbunge rasmi pale mjengoni,’’ aliandika Shilole.

STEVE NYERERE

Steven Mengele ‘Steve Nyerere, ni msanii na kiongozi wa Bongo Movie Unity.Steve ambaye ni Mwenyekiti wa Kampeni ya Uzalendo Kwanza, tangu mwaka 2015, alikuwa katika harakati za siasa. Februari mwaka huu, alifunguka kugombea ubunge katika Jimbo la Iringa Mjini kupitia tiketi ya CCM.Steve alisema kuwa, nia ya kugombea ni kuleta maendeleo katika Jimbo la Iringa Mjini.“Nimeona Iringa Mjini pana kila sababu ya kuwa jiji kama Arusha na mengine. Ili pachangamke, mimi natosha, nafaa na nina uwezo wa kuibeba Iringa yangu,’’ alisema Steve Nyerere.

Rashid Mwinshehe ‘Kingwendu’.

KINGWENDU

Msanii wa Vichekesho Bongo, Rashid Mwinshehe ‘Kingwendu’, hivi karibuni naye katangaza nia ya kugombea ubunge.Katika uchaguzi wa 2015, Kingwendu aligombea ubunge katika Jimbo la Kisarawe, Pwani kupitia tiketi ya CUF na kushindwa.

 

Katika Uchaguzi wa mwaka huu, ametangaza tena kurudi na kugombea kupitia chama kile kile, akiwa na nia ya kuwatumikia wananchi wa Kisarawe.“Mwaka 2015 niligombea japo sikufanikiwa kupita, lakini kwa mwaka huu narudi tena jimboni kwa ajili ya kugombea, ili niweze kuwatumikia wananchi,’’ alisema Kingwendu.

Clayton Revocatus Chipando ‘Baba Levo’.

BABA LEVO

 

Msanii wa muziki wa Bongo Fleva na Diwani wa Kata ya Mwanga Kaskazini (ACT Wazalendo), Clayton Revocatus Chipando ‘Baba Levo’, pia ametangaza kugombea ubunge.

 

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa Habari Juni 5 mwaka huu, Baba Levo alitangaza rasmi kugombea ubunge katika Jimbo la Kigoma Mjini, kupitia tiketi ya Chama cha ACT Wazalendo.Baba Levo alisema kuwa, sababu ya kugombea ubunge ni kwa sababu anakubalika na wananchi.

 

“Sababu kubwa, ninakubalika kwa wananchi, wamekuwa wakinipa moyo kuwa nivuke hatua ya udiwani hadi ubunge. Tayari kuna maendeleo, lakini nitaendeleza miradi mingine mjini Kigoma,’’ alisema Baba Levo.

Hamis Mwinjuma ‘Mwana Fa’.

 

MWANA FA

Mwanamuziki nguli wa Hip Hop, Hamis Mwinjuma ‘Mwana Fa’, naye pia amekiri kutangaza nia ya kugombea.

Katika mahojiano na ‘media’ moja Aprili 27 mwaka huu, Mwana Fa alitangaza kugombea ubunge, japo hakuweka wazi jimbo wala chama atakachogombea.

 

“Kuhusu kugombea ubunge mwaka huu, chama changu hakijaruhusu kuongea, muda ukifika nitasema, nia ya kugombea ninayo, subiri,’’ alisema Mwana Fa.

 

KALA JEREMIAH

Rapper anayefanya vizuri katika kiwanda cha Hip Hop, Kala Jeremiah, aliwahi kusema kuwa anaombwa sana kugombea ubunge.Kala ambaye amekuwa akitoa ngoma zinazoigusa Serikali kwa namna moja ama nyingine, alisikika akisema kuwa kutokana na kile anachokiimba, watu wanaona nafaa kugombea ubunge.“Mimi ni msanii ambaye nimekuwa nikiimba Serikali, hivyo nimeombwa tangu mwaka 2010 kugombea ubunge na wananchi hata viongozi,’’ alisema Kala.

 

PROFESA JAY

Nguli wa muziki wa Hip Hop na Mbunge wa Jimbo la Mikumi, Morogoro kupitia Chadema, Joseph Haule ‘Profesa Jay’, naye alitangaza kutetea nafasi yake jimboni humo.Profesa Jay, ambaye ameliongoza Jimbo la Mikumi kwa muda wa miaka mitano, anatarajia kurudi tena Mikumi ili kuwawakilisha wananchi wake mjengoni.

 

SUGU

Joseph Mbilinyi maarufu Sugu au Mr. 2, ni mwanamuziki mkongwe na muasisi wa muziki wa Hip Hop nchini.Sugu ametumikia wananchi wa Jimbo la Mbeya Mjini, tangu mwaka 2015.Amesema anatarajia kurudi tena jimboni kwake kwa ajili ya kujinadi na kuendelea kuwatumikia wananchi wake.

 

DUDE

Staa wa filamu hapa nchini, Kulwa Kikumba ‘Dude’, mwaka jana alisikika akikiri kuwa atatangaza nia ya kugombea ubunge nyumbani kwao Tabora.Dude ambaye ni Katibu wa kampeni ya Uzalendo Kwanza, alisema kuwa vijana wanatakiwa kujitokeza pale inapotokea fursa hata kama ni msanii.“Mimi nitatangaza nia katika uchaguzi mkuu, nitarudi nyumbani kugombea,’’ alisema Dude.

 

JOKATE

Jokate Mwegelo aliwahi kuwa Miss Tanzania namba 2 mwaka 2006 na kwa sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe.Februari mwaka huu, Jokate aliwahi kukiri kuwa kama atapata nafasi ya kugombea ubunge, ni lazima akagombee nyumbani kwao Ruvuma.“Mimi ni kiongozi na bado naona kuna fursa nyingi, kama nitapata nafasi ya kugombea ubunge, basi lazima nirudi nyumbani kwetu Ruvuma, nilikozaliwa ili nikawatumikie wananchi wa huko,’’ alisema Jokate ambaye ni mwanachama wa CCM.

 

JOHARI

Msanii wa filamu kunako Bongo Movies, Blandina Chagula maarufu Johari, pia ametangaza nia ya kugombea ubunge uchaguzi wa mwaka huu kupitia CCM.Johari alisema, “Kutangaza nia ni lazima, katika maisha usipende kujiweka nyuma, nikiingia mjengoni naweza kuwatetea wasanii wenzangu,’’ alisema Johari.

 

NAY AUTAKA URAIS

Mbali na mastaa wengine kutangaza nia ya kugombea ubunge, mwanamuziki wa Hip Hop hapa nchini Emmanuel Elibariki, yeye anataka kugombea nafasi ya Rais.Nay wa Mitego aliwahi kusikika akisema kuwa, hawezi kugombea ubunge bali urais.“Nimekuwa nikishawishiwa na wananchi, kugombea lakini siko tayari, labda nigombee Urais, tena Rais ambaye si mwanasiasa, ambaye atafanya vitu kama wafanyavyo wengine,’’ alisema Nay wa Mitego.

STORI: HAPPYNESS MASUNGA, DAR

WASANII KUFURIKA SABASABA, ZAMARADI ATOA LIST, YUMO JUX, WOLPER, FA, SHISHI

Leave A Reply