Kumiminika Kwa Wawekezaji Wa Kibiashara Nchini Tantrade Yapongeza Uongozi Wa Rais Dk. Samia
Dar es Salaam 7 Julai 2024: Ikiwa ni siku Siku ya Korea ya Biashara katika Viwanja vya Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ‘Sabasaba’ Mkurugenzi wa Tantrade, Bi. Latifa Khamis amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake bora na kuwezesha biashara kufunguka baada ya Tanzania kuonekana kuwa sehemu bora ya kuwekeza.
Mkurugenzi huyo amesema hali hiyo imepeleka wafanyabiashara kutoka sehemu mbalimbali ulimwenguni kumiminika hapa nchini kuja kuwekeza.
Ameendelea kusema kuwa hali hiyo imepelekea mashirikiano mema ya kibiashara katika Tanzania na Korea na kupelekea maadhimisho hayo ya Kibiashara ya Korea kufanyika kwenye viwanja hivyo na kuhudhuriuwa na wadau mbalimbali.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara Na Maendeleo ya Viwanda, Fatma Mabrouk Khamis aliyemuwakilisha waziri wake, Omary Said Shaaban ameipongeza hafla hiyo iliyowakutanisha wafanyabiashara wa Korea na Tanzania na kubadilishana ujuzi.
Bi. Fatma ameyasifu maonesho yaliyofanywa kwenye hafla hiyo ambapo makampuni kadhaa ya Korea yalionesha ubunifu wa bidhaa zao.
Naye Mtafiti Mwandamizi Na Mshauri wa Masuala ya Siasa na Uchumi kutoka Ubalozi wa Korea hapa nchini, Hyunseok Jeon ameyapongeza maonesho hayo waliyofanya kwa ushirikiano wa Watanzania kwa mara ya kwanza mwaka huu na kuweza kuonesha ubunifu wa bidhaa zao na hivyo kuweza kupanua wigo wao kiuchumi.
Miongoni mwa bidhaa zilizooneshwa kwenye maonesho hayo ni pamoja vipodozi, mitindo ya mavazi na mengineyo.