visa

Kumuombea mwenzako mabaya kuna faida gani?

young-couple-arguing-on-a-sofa-136381366849303901-130702114836Neno wivu katika kamusi ya Kiswahili sanifu ya Taasisi ya uchunguzi wa Kiswahili ya Chuo kikuu cha Dar-es-Salaam limetafsiriwa kuwa ni hali ama tabia ya mtu kusononeka au kukasirika anapomuona mpenzi au rafiki yake ana uhusiano wa mapenzi na mtu mwingine. Kamusi hiyo pia imeeleza kuwa neno hilo wakati mwingine hutumika kama ngoa ama kijicho.

Ngoa ni hali ya kuona uchungu, kujisikia vibaya au kuwa na chuki kwa kukosa kitu mara nyingi kizuri ambacho mwingine amekipata. Kijicho nalo limeelezwa kuwa ni tabia ya mtu kutopenda mwingine apate mafanikio.

Sasa, leo nitazungumzia hali ya mtu kuona uchungu, kujisikia vibaya na kuumia kutokana na mtu mwingine kupata mafanikio. Watu wengi wanaposikia neno wivu masikioni mwao huona kwamba ni kitu kibaya na kamwe hakiwezi kuwa kizuri.

Sawa, wivu ni tabia mbaya sana kama mtu hatakuwa makini nayo lakini pia ni tabia ambayo ikitumika vilivyo inaweza kuleta faida katika maisha ya binadamu. Wivu ni tabia asilia ambayo kila binadamu anayo.

Lakini sasa ni wivu wa aina gani ambao unakubalika na una faida kwa binadamu? Kwa wale ambao wako mashuleni wivu unahitajika ili uweze kufanya vizuri katika masomo. Usipokuwa na wivu unaweza kuona kwamba mwenzako kupata 100%  na wewe ukapata 20% ni kitu cha kawaida tu na wala hakiwezi kukuuma.

Lazima uwe na wivu na umuonee ‘gere’ huyo aliyepata alama nzuri ili uweze kufanya jitihada za dhati kuhakikisha kwamba unamfikia ama unampita kabisa.

Kama unaishi na mtu ambaye amekuwa na mafanikio makubwa, siyo vibaya kama utakuwa na wivu juu yake kwa kujiuliza kwa nini yeye kafanikiwa, lazima ikuume na wivu huo ukufanye kuwa na juhudi katika kuhakikisha na wewe unafanikiwa kama yeye.

Kama uko kazini na mwenzako akapandishwa cheo kuwa na wivu, kwa kuanza kujiuliza kwa nini mwenzako amepandishwa cheo wewe umeachwa. Maswali hayo ndiyo yatakupatia jibu ambalo naamini linaweza kukupa changamoto na kujikuta unaongeza bidii.

Kwa kifupi wivu ambao unakubalika ni ule wa kuumia, kuona uchungu na kutolala ama kukosa raha kutokana na mafanikio aliyoyapata mwenzako na hali hiyo ikakufanya uone umuhimu wa kuongeza bidii katika maisha yako ili na wewe ufanikiwe kama alivyofanikiwa mwenzako.

Ninachojaribu kusema ni kwamba, wivu ukuweke katika mazingira ya kujiuliza kwa nini mwenzangu kafanya hivi mimi nishindwe? Kwa nini fulani kasoma mpaka chuo kikuu mimi niishie darasa la saba? Hiyo ndiyo roho ya kwa nini inayokubalika.

Wapo watu katika jamii tunayoishi wana tabia ya kuwaonea kijicho wenzao kiasi cha kufikia hatua ya kuwaendea kwa waganga ili ikiwezekana mafanikio wayasikie kwa wenzao tu. Hivi ukifanya hivyo itakusaidia nini?

Eti unakasirika kabisa na kutumia pesa zako ili jirani yako asipate pesa ya kununulia nyama, awe anakula dagaa tu kila siku. Asipate pesa ya kujengea nyumba ili awe wa kupanga kila siku, asipate pesa ya kununulia gari ili kila siku atembee kwenye jua kwa miguu.

Hivi ikiwa hivyo wewe utanufaika nini? Huoni utakuwa unajichumia dhambi za bure tu? Hebu tubadilike jamani. Tuwe na mioyo ya kutakiana mema kwa kuwa mwisho wa siku kila mmoja ataondoka duniani, yanini umtakie mwenzako mabaya? Badilika!
Toa comment