The House of Favourite Newspapers

KUNA FAIDA WAPENDANAO KUKWARUZANA

MUNGU ni mwema tena Jumamosi ya leo ametupa pumzi. Kwa wale wenye changamoto mbalimbali, msikate tamaa, Mungu atawatia nguvu mtarejea kwenye hali nzuri na maisha yataendelea kama kawaida.  

 

Nikirejea kwenye mada yangu ya leo, nataka tuzungumze kuhusu suala zima la faida za wapendanao kukwaruzana. Najua wengine mnaweza kujiuliza kwa nini niseme faida lakini ninachotaka kushea na nyinyi hapa, mikwaruzano ni muhimu kwa wapendanao.

 

Mikwaruzano kwenye uhusiano inawafanya muwe imara. Inapotokea inawapa funzo kwamba mkishasameheana, muishi vipi ili msiweze kuingia tena kwenye kitu ambacho kiliwafanya mkwaruzane au mpoteze amani yenu.

 

Katika hali ya kawaida kabisa, hakuna mwanadamu aliyekamilika hivyo tunapaswa kuelewa kwamba suala la kupishana mawazo lipo tu. Hauwezi kuepuka kutofautiana na mwenzako ambaye mmekutana mkiwa tayari na akili zenu timamu, hivyo mnachotakiwa kufanya ni kuitumia nafasi hiyo kujiimarisha.

 

Hamuwezi mkakaa kwenye uhusiano mwaka mmoja, miwili hamjagombana hata iweje lazima itafika mahali kidogo mwenzako atakukwaza na mtaingia kwenye mvutano. Mnachotakiwa tu kufanya ni kuchukulia changamoto hiyo kama funzo.

 

Mjue ni nini kimesababisha hadi mpishane. Kwenye eneo hili kila mtu anapaswa kujitathimini yeye mwenyewe. Zungumza na nafsi yako uone ni kweli hujamkosea mwenzako? Kama ulimkosea, muombe radhi na ujue kwamba hilo liwe kama mwongozo kwako ili kuwasaidia lisitokee tena.

 

Kwa kawaida Waswahili wanasema siku huwa  hazifanani, kuna siku mwenzi wako anaweza akawa ameamka vibaya, labda pengine alikuwa na mawazo fulani hivyo ni muhimu pia kumsoma mwenzako na kumjua vizuri.

 

Siku ambazo unamuona anakuwa hayupo sawa, epuka sana kumzungumzisha vitu ambavyo unahisi vitamkwaza kwa haraka. Mathalan mwenzako ametoka kazini pengine ameshavurugwa na bosi au wafanyakazi wenzake basi ni jukumu lako kumsoma na kumweka karibu katika mazungumzo rafiki na siyo ya kumkwaza.

 

Wanaoshindwa kulizingatia hili wamejikuta kwenye migogoro ya kila mara na wenzi wao. Utasikia mtu analalamika kwamba mpenzi wake anakasirika kwa jambo dogo bila kujua kwamba chanzo cha hasira hizo huwa ni yeye.

 

Itazameni migogoro au jambo lolote baya katika jicho la kujiimarisha. Usiichukie migogoro au malumbano ila unatakiwa kuitumia kama funzo. Mnatakiwa kuitumia kama elimu ya kuiepuka ili isiwe inatokea mara kwa mara.

 

Ujue kwamba jambo fulani liliwafanya mgombane kwa sababu gani? Ukishaijua sababu basi ikuongoze katika kuwapa mbinu ya kuliepuka pindi litakapotokea tena. Msiiogope migogoro, msiifanye kama sababu ya kufikia maamuzi ya kuachana bali muitumie kujifunza ili isitokee tena.

Tatizo la vijana wengi wa sasa ni kwamba huwa hawana uvumilivu. Wanaona suluhu kubwa na ya haraka ya ugomvi ni kuachana. Hawataki kuzinguliwa kwa muda mrefu, wanachagua kuachana tu. Anaachana na huyu anahamia kwa mwingine. Kule nako akizinguliwa kidogo tu anasonga mbele zaidi.

 

Ndugu zangu hakuna mwanadamu mkamilifu. Kila mmoja ana mapungufu yake. Baki na huyo mmoja uliyenaye. Shikamana kwelikweli sababu huyo unamjua zaidi kuliko yule ambaye utakwenda kuanza upya. Gombana na huyohuyo na utashangaa mnaishi miaka mingi kwa kuwa mnasameheana.

 

ANGALIZO

Hata kama nimesema kuna faida kwenye changamoto hizo lakini unapaswa kuzipima je, hazijirudii mara kwa mara? Kila mkisameheana haipiti muda changamoto hiyohiyo inajirudia? Unapoona hali hiyo inadumu kwa muda mrefu sana basi unapaswa kuchukua hatua maana mtakuwa mmeshindwa kuitumia migogoro kama sehemu ya kujifunza bali migogoro imekuwa sehemu ya maisha yenu.

Tukutane wiki ijayo. Unaweza kunifuata kwenye mitandao ya kijamii, Instagram na Facebook natumia Erick Evarist, Twitter natumia ENangale.

Comments are closed.