Kartra

Kuna Makabila Hayafai Kuoa, Kuolewa?

IPO kasumba ambayo inawatafuna watu wengi. Kwamba kabila fulani ni zuri, linafaa kuoa au kuolewa, lakini kabila fulani si zuri kuoa au kuolewa. 

 

Wapo watu wazima, kwa uzoefu wao wanawamezesha ushuhuda vijana wao. Kwamba ukitaka kuoa au kuolewa, usikubali kuingia kwenye kabila fulani. Wanatoa hoja zao na kulinganisha na mazingira wanayoyajua wenyewe.

 

Hiyo inawakaa vijana akilini mwao na pengine na wao kwa namna moja au nyingine, wanasambaza habari hizo kwa vijana wenzao. Kasumba hii inakua na kuwafanya watu wengi waiamini na kuona kuwa ni dhana ya kweli kwenye jamii. Wanawake wana makabila yao ambayo hawataki kuyasikia, vivyo hivyo wanaume nao wana makabila  yao wanayoyaogopa.

 

Ndugu zangu, leo nataka tulizungumze kwa undani suala hili. Tujue uzito wake. Yawezekana kabisa hoja hizo zikawa na mashiko, lakini tukubali tukatae, haya mambo yanatokea kutokana na jinsi mtu mwenyewe alivyo.

 

Tabia ya mtu ndiyo ambayo huakisi matendo yake. Kabila mara nyingi hufanywa tu kichaka cha kuhalalisha maovu ya mtu. Tuelewane jamani kwamba, hata kama kuna ukweli, lakini hauwezi kuwa wa watu wote au kabila zima.

 

Tabia ya mtu inapimwa na mtu. Ni kama vile ambavyo wewe unaweza kumuona msichana au mvulana fulani na kuweza kumchunguza kama anakufaa au la. Wewe ndiye unayemuangalia mtu wako na kuona anaweza kuwa wako au la, kutokana na vigezo unavyovihitaji.

 

Jiulize tu wewe mwenyewe kuna makabila umeyasikia ni mazuri, hayana mambo ya hovyohovyo, lakini je, ni wote wanadumu kwenye uhusiano wa uchumba au ndoa? Kuna wangapi ambao ukiwaangalia unaona ni wema, wapole wastaarabu na wenye hekima, lakini ndoa zimewashinda kutokana na tabia zao mbaya?

Ndiyo maana mimi nasisitiza kwamba suala la kabila halina maana sana kwenye masuala ya uhusiano. Zaidi wewe angalia sifa zile za msingi na uwe mwongozo katika kumpata mtu ambaye atakuwa mke au mume mtarajiwa.

 

Achana na kelele za watu maana mara nyingi zinaweza kukupoteza na kukufanya ushindwe kufikia uamuzi sahihi. Kabila fulani lilimshinda, yawezekana wewe ukaliweza. Yawezekana mtu anayekuzuia au kukupa ushuhuda wa kabila fulani yeye ndiye alikuwa tatizo, halafu anasingizia kabila la mwenzake.

 

Unachotakiwa kukiangalia ni kwamba, uliye naye ana tabia njema? Ana hofu ya Mungu? Mnaelewana na kusikilizana au ni kitu kimoja? Maisha ya sasa yanahitaji watu muwe mnazungumza lugha moja na kunia mamoja. Muelewane na mjue njia za kupita kufikia kilele cha mafanikio yenu.

 

Watu wenye sifa hizi wapo. Haijalishi wanaweza kuwa kabila au dini gani, lakini wapo. Suala la msingi ni kumuomba Mungu akupe mtu wa aina hiyo. Akupe mtu ambaye hatakusumbua, mtakayepanda milima na kushuka pamoja.

Acha kuishi kwa mazoea na mahubiri ya kizamani kwa kigezo kwamba yanazungumzwa na wengi au na watu wazima. Mmiliki wa serikali ya maisha yako ni wewe na huyo mwenzako. Ninyi ndiyo mtakaoishi pamoja na si mwingine.

 

Wewe ukijiridhisha na kusema ndiyo kwa mwenza wako, asiwepo wa kukupinga maana akikuchagulia kabila au mtu anayemtaka yeye, anaweza asiwe sahihi kwako. Mnaweza mkashindwana vilevile licha ya kwamba amekuchagulia kabila zuri.

 

Kwa leo inatosha, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri. Unaweza kunifuata kwenye mitandao ya kijamii; Instagram & Facebook: Erick Evarist, Twitter: ENangale.


Toa comment