The House of Favourite Newspapers

KUNA WAKATI PENZI LINAGEUKA KUWA KIFO, JIEPUSHE HIVI

NIANZE kwa kuwatakiwa Waislamu wote nchini mfungo mwema wa Mwenzi Mtukufu wa Ramadhani. Ni kipindi cha kufanya ibada, kujinyima kula na kutoa sadaka. Ni wakati mzuri wa kumrudia Mwenyezi Mungu na kufanya toba ya kweli. Nawaombea muwe na mfungo mwema na muweze kukamilisha funga yenu salama, Mungu awafanyie wepesi na kwa msaada wake yeye mtaweza kuzimaliza siku 30, inshaallah.

MADA YA LEO

Nikirudi kwenye mada ya leo, kama inavyojieleza hapo juu ni vyema tukajifunza kwa pamoja ili kuzielewa nyakati. Kujua jinsi gani ya kuepukana na matatizo, migogoro ambayo inabadilisha pendo kuwa kifo. Mnapoianza safari ya uhusiano siku zote huwa penzi linakuwa sehemu salama. Mapenzi yanakuwa mtomoto, kila mmoja anaamini kwamba hakuna kitu kibaya anachoweza kutendewa na mwenziye zaidi ya kupewa mahaba ya

kweli. Hapo kila mmoja anajisahau, haamini kuhusu mauaji ya wapendanao. Anapoyasikia kwenye vyombo vya habari mara nyingi hudhani kwamba yanatokea kwa wengine tu na hayawezi kumtokea yeye. Yeye anajiona yupo sehemu salama sana.

HAKUNA ALIYE SALAMA

Ndugu zangu tunajiongopea, hakuna aliye salama sana. Yanayowatokea wengine kwenye mahusiano yao yanaweza kukutokea hata wewe. Unaona uhusiano wenu una amani, una

furaha na mnapendana vilivyo na mwenzako, inaweza kutokea siku moja mkawa maadui wa kuuana. ZIPO SABABU… Amini kwamba zipo sababu nyingi ambazo zinasababisha penzi linakuwa si sehemu salama tena. Hata kama mnapendana namna gani lakini kutokana na hizo sababu, lolote linaweza kutokea na mkajikuta hata nyinyi wenyewe hamuaminiani tena.

SABABU ZENYEWE

Miongoni mwa sababu zinazosababisha penzi libadilike na kuwa siyo sehemu salama ni mbadiliko ya tabia. Mabadiliko ya tabia yanaletwa na mambo mengi, yawezekana ikawa ni madaraka au hata mafanikio ya kimaisha kwa maana ya utajiri. Baada ya kupata kitu kimoja kati ya hivyo viwili nilivyoviainisha hapo juu, mtu anaweza kubadilika. Akawa mkorofi, akawa na tabia mbaya. Mathalan anaweza kuwa mlevi au hata mzinzi. Haya na mengine mengi yanaweza kukufanya ufikie kwenye ugomvi wa kifo. Waweza pia kujiingiza kwenye uhusiano na mtu nje ya ndoa na kujikuta hata umepata mtoto nje ya ndoa.

Waweza pia kumpa maudhi mwenzako ambayo yanaweza yakamfanya mwenzako afikie hatua ya kukufikiria jambo baya na hapo ndio uhusiano unapogeuka na kuwa sehemu hatari. Mnajikuta mnaishi kwa machalemachale. Mume hamuamini mke, mke hamuamini mume. Mnapofikia hatua hii ni hatari sana.

CHUNGA SANA USALITI

Ukifuatilia kwa makini matatizo mengi katika masuala ya uhusiano chanzo chake huwa ni usaliti. Unaposaliti mwenzako akakubaini, akakuonya mara moja mara mbili ukawa jeuri. Ukajifanya mjanja, ukawa unaendelea halafu akawa anafahamu, jiandae kwa lolote. Huwezi kujua anapokuwa kimya anawaza nini katika akili yake, anafuga hasira ambazo zikija kulipuka ni maafa. Anaweza kuwa anateseka kwa muda mrefu, anaumizwa na maneno anayosikia kwa watu, anachekwa, anadharauliwa unategemea nini?

JIEPUSHE

Unapokuwa kwenye uhusiano wowote, unapaswa kujiheshimu. Kujichunga sana na vishawishi vya usaliti. Usaliti unaua, usijaribu kabisa kusaliti. Ridhika na uliye naye. Madaraka au utajiri visikubadilishe tabia na mienendo, heshimu mahali ulipo. Kaa mbali na marafiki wabaya. Epuka malumbano ya mara kwa mara na mwenza wako kwani yanafuga hasira ambazo zinajenga chuki mbaya inayoweza kukuletea madhara makubwa. Ufanyeni uhusiano wenu uwe salama kwa kumtanguliza Mungu mbele katika kila jambo. Instagram & Facebook: Erick Evarist Twitter: ENangal

Comments are closed.