The House of Favourite Newspapers

Kununua gari kisa mwezako analo ni ulimbukeni uliopitiliza!

0

Wakati f’lani uliwahi kuibuka mjadala mzito sana kwenye kundi letu la WhatsApp ambapo mmoja aliuliza kwamba kati ya gari na nyumba, kipi ambacho kijana anatakiwa kumiliki kwanza?
Ulikuwa mjadala mzito sana kwani waliokuwa wakisema nyumba kwanza, walijaribu kutoa sababu za wao kusema hivyo na wale waliosema gari nao hawakukubali kushindwa! Nao walitaka kila mmoja aamini gari kwanza, mengine baadaye!
Kwa watu wanaojali maisha, najua watasimamia kwamba nyumba kwanza kwani litakuwa ni jambo la ajabu kama utakuwa unamiliki gari la kifahari halafu unalipaki CCM kisha umepanga tena chumba kimoja.

Lakini wakati mwingine tufahamu kwamba kwenye maisha kuna kitu Wazungu wanasema ‘first choice’, yaani chaguo la kwanza! Kwamba leo hii ukiweka gari na nyumba kisha ukawaita vijana wawili na kuwataka wachague, yupo atakayechukua gari na kuna ambaye ataona nyumba kwanza.

Katika mazingira hayo huwezi kumuona yule aliyechagua gari kwanza kwamba ni limbukeni na hajui mambo ya msingi katika maisha. Huenda wewe ukadhani kumiliki nyumba kunakupa heshima kubwa kwenye jamii licha ya kwamba utakuwa unatembea kwa miguu juani lakini elewa wapo wanaoona bora waishi kwenye nyumba ya kupanga lakini wakikatiza mitaani wanaendesha magari ya kifahari.

Hapo ndipo linapokuja suala la ‘choice’, kwamba wapo wanaoona kumiliki nyumba kwenye maisha yao wala siyo ishu, badala yake wanaona kuwa na gari la kifahari ndiyo furaha ya maisha yao.

Lakini wakati wakiwepo watu wa aina hiyo, wewe hukatazwi kuanza kumiliki nyumba. Kama unaona ukiwa na mjengo wako wa maana, moyo wako unakuwa na amani na furaha, anza kumiliki rasilimali hiyo. Kikubwa ni kuongea na moyo wako.
Katika hili wala hutakiwi kufuata mkumbo. Kwa mfano kama rafiki yako anaishi kwenye nyumba ya kupanga lakini anamiliki gari, hutakiwi kukopi alichokifanya. Jadiliana na moyo wako kwamba uanze kipi, ukikuambia anza na gari huku ukikupa sababu, usikilize!
Hata hivyo, leo hii ukitaka nikushauri kipi uanze kumiliki, nitakushauri kutokana na matakwa yangu na nitakuambia nunua gari kwanza. Kwa nini nitakushauri hivyo? Kwa sababu nafsi yangu ilinisukuma kufanya hivyo.

Nikimaanisha kwamba, hata mimi nilianza kumiliki gari kisha ndiyo likaja suala la nyumba. Unajua kwa nini? Ni kwa sababu kumiliki nyumba katika ulimwengu wa sasa lazima uanze kununua kiwanja, kiwanja ambacho huwezi kukipata kirahisi. Utalazimika kutembea maeneo mbalimbali ambayo kama utakuwa unatumia usafiri wa kukodi, gharama itakuwa kubwa, lakini vipi kama utakuwa na kigari chako?
Lakini pia yawezekana kumiliki kwako gari ni ili ikusaidie kwenye mishe zako za kutafuta pesa zaidi. Kuna ubaya gani sasa kuanza kuwa nayo kabla ya kujenga nyumba?
Yote kwa yote, uamuzi ni wako ila nitakuona limbukeni mkubwa kama utalazimika kununua gari kwanza kisa umeona rafiki yako kafanya hivyo.

Leave A Reply