The House of Favourite Newspapers

Kupoteza hamu ya kula “Anorexia Nervosa”

0

healthy_food_decisions (1)Hili ni tatizo la kukosa kabisa hamu ya kula na kumfanya mtu apungue sana uzito kutokana na kuogopa kunenepa au kuongezeka uzito. Watu wanaopata zaidi tatizo hili ni wale waliokusudia hasa kwa dhati kujinyima kula ili wapungue uzito na mwili kuwa mwembamba hivyo hujinyima kula kwa kiasi kikubwa kwa kujihisi kuwa wana uzito au miili mikubwa au kujihisi wanene.

Tatizo hili la kujihisi unene ni la kisaikolojia zaidi kwani tunaposema fulani ni mnene lazima upime “BMI” ambayo ni uwiano wa uzito na urefu. Hivyo ni vema ukajifahamu ‘BMI’ yako ikoje kabla ya kuanza kupanga utaratibu wa kupunguza uzito.

Kupoteza hamu ya kula kunasababishwa na mambo mbalimbali, mojawapo ni kutokana na muendelezo wa kuzoea kujinyima chakula, tatizo la kiugonjwa na inaweza kuwa hali ya kurithi.

CHANZO CHA TATIZO

Chanzo halisi mbali ya hilo la kukusudia kujinyima bado hakijulikani rasmi lakini inaweza kuwa matatizo ya kimwili, matatizo ya kisaikolojia na matatizo ya kijamii kutegemea na aina ya vyakula vinavyopatikana katika jamii husika.

Katika tatizo la kimwili ambapo kitaalam tunasema ‘Physiological’ hali ya kuvurugukika katika mfumo wa kichocheo cha ‘Serotonin’ huchangia.

Tatizo hili pia hurithiwa endapo katika familia kuna watu wa aina hiyo wasiopenda kula.

Wanawake wajawazito huweza kuathirika na tatizo hili la kupoteza hamu ya kula kutokana na hali ya ujauzito na kusababisha apate tatizo la upungufu wa damu, kisukari, kifafa cha mimba, matatizo katika kondo la nyuma na matatizo kwa mtoto aliye tumboni na hata mtoto akishazaliwa.

Wengine wanaopatwa na tatizo hili ni wagonjwa hasa wale wenye homa kama malaria au wenye matatizo katika mfumo wa chakula. Watu wenye magonjwa sugu au wanaotumia dawa kwa muda mrefu pia hupatwa na tatizo hili.

DALILI ZA TATIZO

Mtu hupoteza hamu ya kula, wengine kupoteza hamu ya kula hata kwa kutumia dawa ili kupunguza mwili au kujipunguza uzito, kwa hiyo mtu anapojinyima kula lengo ni kujikondesha na kujikondesha kuna madhara kiafya kama tutakavyokuja kuona.

Mtu anayejikondesha anaweza kuwa na dalili za utapia mlo kama vile ngozi kuzeeka na kunyauka, mifupa ya usoni, mabega kujitokeza na mbavu kuhesabika kirahisi, kuchoka mara kwa mara na mwili kukosa nguvu, misuli kukaza na baadhi ya viungo vya mwili kuathirika mfano ubongo, moyo na figo hata ini.

Tatizo hili la kujikondesha kwa makusudi au kutokana na maradhi humfanya mtu apate tatizo la kiafya liitwalo ‘Hypokalaemia’ ambapo madini ya ‘potassium’ mwilini hupungua, hivyo hulalamika mapigo ya moyo kutokwenda vizuri, kufunga kupata choo kikubwa, uchovu wa mwili na wakati mwingine mwili kupooza.

Dalili nyingine ni kupoteza kabisa hamu ya kula, kufunga kupata hedhi, nywele kichwani kuwa nyepesi, shinikizo la damu hushuka na kuhisi moyo kwenda mbio wakati wa kuongea au kutembea, kuwa na msongo wa mawazo, tumbo kujaa gesi na kutoa harufu mbaya ya mwili, ngozi huwa kavu na ngumu.

MADHARA

Tatizo la kukosa hamu ya kula kama tulivyoona mtu hukonda na unapofikia hali hiyo unaharibu mifumo mbalimbali ya mwili na hukufanya uwe mgonjwa. Mfumo ambao huathirika zaidi na kuonesha dalili za wazi ni mfumo wa uzazi kwa mwanaume na mwanamke.

Mwanaume hupoteza uwezo wa kufanya tendo la ndoa kutokana na matatizo mbalimbali ya mfumo wa mwili yanayotokana na upungufu wa lishe bora.

Mwanamke hupoteza hedhi, hupoteza uwezo wa kuzaa na hamu ya tendo la ndoa na hata wakati wa tendo.

Uwezo wa kuzaa unapotea ndipo tunaposema ugumba, hapa vichocheo au homoni za uzazi huvurugika na kupungua kwa kiasi kikubwa.

USHAURI

Epuka kujipunguza uzito, fuata ushauri wa daktari kama unahisi uzito wako ni mkubwa na unataka kupungua ili kuepuka matatizo.

Mwanamke au mwanaume aliye katika mpango wa kuzaa inampasa azingatie kanuni bora katika uzito unaostahili ili aweze kupata mimba haraka au aweze kumpa mwanamke ujauzito katika kipindi muafaka.

Uzito mkubwa kupita uwezo wa mwili wako ni tatizo, na uzito mdogo kuliko mwili wako unavyostahili pia ni tatizo hasa katika mfumo wako wa uzazi.

Zipo dawa zinazoshauriwa kitaalam kwa kupunguza uzito na zipo ambazo hazishauriwi jambo la msingi ni kumuona daktari kwa ushauri katika hospitali ya wilaya na mkoa.

Leave A Reply