The House of Favourite Newspapers

Kushuka kwa kizazi ( Prolapsed uterus)-2

0

Uterine-Prolapse-Image-4Wiki iliyopita nilianza kuzungumzia mada hii na leo nitaimalizia ili wiki ijayo nianze nyingine.

Niliishia pale ambapo nilisema kuwa, kupungua kwa homoni ya ‘Estrogen’ kunaweza tu kutokea kwa bahati mbaya au kutokana na matumizi ya muda mrefu ya dawa za homoni bila ya mpangilio maalum.

Matatizo mengine yanayosababisha hali hii ni kama vile;

Cystocele. Hii ni hali ambayo mwanamke anahisi uvimbe ukeni kwa ndani upande wa juu sehemu ya kibofu cha mkojo na kusababisha ahisi kwenda haja ndogo mara kwa mara na kupata kiasi kidogo cha mkojo au kubanwa na mkojo na usitoke au mkojo kutoka kidogo kidogo.

‘Enterocele’. Ni uvimbe ndani ya ukeni kwa juu ya kizazi kwa nyuma, hali hii inatokana na utumbo mdogo kusukuma kizazi, hali inakuwa mbaya anaposimama kwa kuhisi kizazi kinavutwa kwa chini upande wa nyuma na kupata maumivu ya viungo na hali hii hutulia anapolala chini.

‘Rectocele’. Ni hali ambayo pia ndani ya uke kunavimba upande wa chini ukeni, ambapo mfuko wa haja kubwa huathiri mwenendo wa matumbo, hivyo mwanamke mwenye tatizo hili hujihisi tumbo kujaa gesi, kukosa haja kubwa, maumivu ya kiuno na mgongo na kuumwa miguu.

Tumeona sababu mbalimbali zinazosababisha hali hii, lakini pia tatizo hili linaweza kutokea hata kwa mwanamke wa umri wa kati endapo atakuwa mjamzito ingawa siyo sana, kuzaa mara kwa mara na mfululizo au kuzaa kwa tabu.

Kuwa na kikohozi cha muda mrefu au ugonjwa wa pumu, kupata haja kubwa kwa tabu. Vilevile kuwa na uzito mkubwa. Matatizo haya husababisha kuongezeka shinikizo tumboni hivyo kusukuma kizazi kwa chini mara kwa mara na kuleta udhaifu wa misuli.

UCHUNGUZI

Endapo utajihisi una dalili zozote katika maelezo tuliyoyatoa, basi muone daktari wa akina mama katika hospitali ya mkoa kwa uchunguzi na tiba.

Vipimo mbalimbali vitafanyika kadiri daktari atakavyoona inafaa.

TIBA NA USHAURI

Tiba itategemea na hatua ya kushuka, hivyo daktari ataangalia nini cha kufanya. Mgonjwa anaweza kuwekewa vifaa maalum kuzuia kisiendelee kushuka au aina maalum ya mazoezi ili kudhibiti kuzuia kisiendelee kushuka. Kama itakuwa kwenye hali mbaya ya kushuka zaidi hasa hatua ya tatu na nne, mgonjwa atafanyiwa upasuaji kwa kuangalia umri na chanzo cha tatizo. Upasuaji unaweza kuwa wa kurekebisha au kuondoa kizazi.

Inashauriwa mwanamke aepuke kazi ngumu za kunyanyua vitu au mizigo mizito, kusukuma mikokoteni, dhibiti unene au ubonge kwa kuangalia ulaji na kufanya mazoezi. Hakikisha unapata haja kubwa vizuri na kila siku. Wahi hospitali kwa uchunguzi na tiba.

JIUNGE NA GLOBAL BREAKING NEWS!

globalbreakingnews.JPG

Leave A Reply