The House of Favourite Newspapers

KUSIKILIZANA; SILAHA KUBWA YA KUDUMISHA PENZI

NI Jumatatu nyingine Mungu ametupa pumzi tunaendelea kusukuma gurudumu la maisha yetu ya hapa duniani, yatupasa tumrudishie yeye sifa na utukufu. Kwa wale wenye changamoto mbalimbali kama za magonjwa, tunawaombea wapone haraka!  Nikirudi kwenye mada ya leo kama inavyojieleza hapo juu, dunia ya sasa imekuwa na matatizo mengi kwa sababu tu ya watu kushindwa kusikilizana. Ulimwengu wa wapendanao unakumbana na hili tatizo ambalo limekuwa likichochea machafuko.

KUAMINI WEWE NI BORA

Watu wanagombana, wanashindwa kuendelea na safari kwa sababu tu ya kushindwa kuelewana. Kila mmoja anaamini yupo sahihi, anachowaza yeye ndio sahihi kitu ambacho si kweli. Hata kama unaamini upo sahihi lakini unapaswa kumsikiliza mwenzako. Kwa kawaida binadamu tumeumbwa hivyo. Binadamu tuna umimi. Mtu anataka yeye kwanza halafu wengine baadaye na hiyo ndiyo changamoto tunayopaswa kuifanyia kazi hususan katika suala zima la mahusiano.

KUBALIANENI KUTOKUBALIANA

Wapendanao mnakutana mkiwa na umri wa kujitambua, kila mmoja anafahamu mazuri na mabaya. Kila mmoja anaweza kuwa na mtazamo wake katika kila jambo lakini sasa kwa kuwa mnakwenda kuwa mwili mmoja basi hamna budi kukubaliana kutokukubaliana.

Wakati mwingine yawezekana mawazo yako yakawa yapo sahihi lakini mwenzako akakupinga kwa hoja zake ambazo yeye anaamini ni sahihi lakini ili wakati mwingine kuyafanya mambo yaende sawa basi yakupasa tu umsikilize.

MPE NAFASI KWANZA

Hata kama hoja zake hazina mashiko na katika akili ya kawaida unaona kabisa hazina mashiko lakini hauna budi tu kumsikiliza kwanza. Mpe nafasi, halafu baada ya muda unaweza sasa kumpa hoja zako na akakuelewa.

TUJIFUNZE KUWEKA AKIBA

Wengi wetu huwa tunakosea kwa kuwa na desturi ya kushikilia hoja zetu na kung’ang’ania hadi kieleweke muda huohuo. Tunashindwa kuelewa kwamba, jambo hilohilo unaweza kuliweka kiporo halafu baadaye ukaja kuliwasilisha na likafanikiwa.

Tengeneza utamaduni wa kuahirisha jambo hususan pale unapoona mpo kwenye jazba. Mnapoona mpo kwenye hatua ya kuiharibu amani basi hamna budi kuahirisha. Kila mmoja wenu awe na hiyo hulka ya kusema, ‘tuliache hili tutaliongea baadaye.’

WENGI WAMEFANIKIWA

Hii mbinu imekuwa ikiwasaidia wengi, nimekuwa nikipata maoni mengi kutoka kwa wasomaji wangu ambao wamekuwa wakieleza namna ambavyo wamenusuru mahusiano yao kwa sababu tu ya kusema, ‘acha hili lipite tutalizungumza baadaye.’

Kwa kawaida mnapozidi kupandisha hasira wakati mnazungumza huwa kinachofuata ni maamuzi yenye majuto baadaye. Mnaweza kupigana, mnaweza kutangaziana maazimio ya kuachana halafu baadaye hasira zikiwaisha mnaona kwamba mlikosea. Kumbe pengine mngemuepusha shetani apite wakati ule msingefikia hatua mliyofikia. Yawezekana mkawa mmedundana, mmetoana makovu na hata kupelekana polisi kwa sababu tu ya kushindwa kusikilizana.

KUSIKILIZANA NI MUHIMU

Ndugu zangu, hakuna kitu kizuri kama kusikilizana kwenye mahusiano. Kila mmoja ajenge utamaduni wa kumsikiliza mwenzake hata kama anachokizungumza hakina umuhimu sana. Heshimu mawazo yake, heshimu mchango wake kwani hiyo itamfanya hata yeye aheshimu mawazo yako.

Ukijenga mfumo wa kuheshimika wewe tu halafu hutaki kumheshimu mwenzako hakika hilo penzi litakuwa na walakini. Hata kama mtafanikiwa kusonga mbele lakini halitakuwa na ladha nzuri maana litakuwa ni penzi la maagizo kwamba mmoja ndio anaheshimika na ndio mwenye kutoa maagizo.

PENZI NI MALI YA WAWILI

Lifanyeni penzi liwe la wote. Kila mmoja aone ni sehemu ya mahusiano, ana mchango na heshima sawa. Mkiishi kwa staili hiyo, hakika mtafanikiwa sana! Instagram na Facebook: Erick Evarist Twitter: ENangale.

Comments are closed.