KUTENGANA KWA MUDA KUNAVYOWEZA KUOKOA PENZI LINALOKUFA

KATIKA safari ya mapenzi ya watu wawili wanaopendana, lazima kuna milima na mabonde. Wakati mwingine, changamoto zinazoibuka, zinakuwa ni ndogo na wanandoa wanaweza kuzipatia ufumbuzi ndani ya muda mfupi.  Hata hivyo, zipo changamoto nyingine ambazo huwa zinazidi uwezo wa wanandoa wote. Chukulia mfano huu, mmeishi na mwenzi wako kwa kipindi kirefu, lakini maisha yenu yamekuwa yakitawaliwa na ugomvi usioisha katika siku za karibuni.

Kila siku mmekuwa ni watu wa kupigizana kelele, kutukanana au hata kupigana. Vikao vya kuwasuluhisha vimeshakaliwa mara kibao hadi wanaowasuluhisha wamechoka. Ni sawa kuendelea kuishi kwenye uhusiano wa aina hii? Bila kujali chanzo kilichosababisha mkawa mnagombana kila siku, pale mnaposhindwa kumaliza matatizo yenu na kuyafanya yaendelee kwa kipindi kirefu bila kupata suluhisho la kudumu, maana yake kuna kitu kikubwa hakipo sawa kati yenu.

Tabia zenu zimeshindwa kuchangamana, hakuna anayekubali kushuka, kila mtu ni mjuaji na ndiyo maana mnaendelea kugombana kila kukicha. Hatari ya kuendelea kwenye uhusiano wa namna hii, ni kuja kufanyiana ukatili mkubwa ndani ya nyumba.

Upo ushahidi wa watu ambao waliwadhuru wapenzi wao vibaya, lakini nyuma yake ikaja kubainika kwamba kumbe walishakuwa na migogoro kwa kipindi kirefu nyuma. Utasikia majirani wakisema ‘tulishawazoea hao’, ‘kila siku ni ugomvi usioisha’ na maneno mengine kama hayo.

Zipo hasara nyingi za kuishi kwenye uhusiano wa namna hii, usiokuwa na amani. Ukiachilia mbali wanandoa kufanyiana ukatili, wapo ambao kwa ajili ya kutafuta furaha, wamejikuta wakiingia kwenye usaliti kwa kutoka na wanaume wengine au wanawake wengine nje ya ndoa.

Mwanaume anahangaika kivyake kutafuta amani nje ya ndoa, mwanamke naye anadanga kutafuta furaha ndani ya moyo wake, mwisho wake unafikiri itakuwa ni nini? Mtaishia kuleteana magonjwa hatari kama Ukimwi na maisha yenu yakapoteza kabisa mwelekeo.

Kumbe nini cha kufanya katika hali kama hii? Inapotokea umedumu kwenye migogoro ya muda mrefu na mwenzi wako, njia pekee inayoweza kumaliza matatizo yenu kwa wakati huo, ni kupeana ‘break’, mnatengana kwa muda.

Inaweza kuwa ni kwa mwanaume kumrudisha mkewe nyumbani kwa wazazi wao (wazazi wa mwanamke) au kwa mwanaume kuondoka na kwenda sehemu nyingine tofauti.

Mnapopeana muda wa kila mmoja kuishi mbali na mwenzake, kwanza inampa nafasi kila mmoja kujitathmini kama ni kweli anahitaji kuendelea kuishi kwenye ndoa au uhusiano uliopo. Kwa mtu ambaye anakupenda kwa dhati, akikaa mbali na wewe atakumisi na kukusamehe kwa yote yaliyotokea.

Lakini pia inatoa nafasi ya mioyo iliyojeruhiwa kupona na hasira kupungua au kuisha kabisa. Mtakapokutana baada ya kuwa mmetengana kwa muda, mtaweza kufikia hitimisho zuri kama muendelee kuishi pamoja au muachane kwa amani. Lazima kukubaliana na ukweli kwamba kuna wakati mapenzi huisha, usiendelee kung’ang’ania kwamba huwezi kuondoka au hutaki aondoke kwenye mikono yako wakati kila siku mnagombana sana na penzi kati yenu limeisha. Chukua hatua! Kwa leo ni hayo tu, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri.

Loading...

Toa comment