Kutokwa na vinyama sehemu za siri (Genital Warts) kwa wanawake-2

hemorrhoids-during-pregnancyTunaendelea kuchambua ugonjwa wa kutokwa na vinyama sehemu za siri kabla ya kuelezea tiba yake, tuangalie dalili zake.

Wiki iliyopita tulieleza dalili za ugonjwa huu. Tukasema mojawapo ni kuota vinyama vidogo au Genital Warts huonekana kama vioteo laini vinavyojitokeza juu ya ngozi ingawa wakati mwingine vinaweza kuwa vidogo mno kiasi cha kutoweza kuonekana vizuri kwa macho ya kawaida.

Tukasema dalili nyingine ni mgonjwa kuwa na ganzi maeneo yaliyozungukwa ugonjwa na kwa wanawake, uchafu unaotoka sehemu za siri huongezeka na atakuwa anawashwa sana maeneo ya siri na wakati mwingine kutokwa na damu ukeni mara baada ya tendo la ngono, hata hivyo hali hii ni kwa baadhi ya wanawake.

Wanawake wengine ugonjwa huu hujitokeza ndani ya uke au njia ya haja kubwa, nje ya uke au ngozi ya nje kuzunguka njia ya haja kubwa, au ndani ya uke kuzunguka eneo la shingo ya kizazi.

Uchunguzi wa ugonjwa wa huu kwa wanawake hujumuisha maeneo ya nyonga (pelvic examination) ambapo daktari huchunguza eneo hilo kwa kutumia vifaa maalum vinavyomuwezesha kuona uwepo wa maradhi haya na wapi vilipo.

Wakati mwingine daktari anaweza pia kufanya kipimo cha Pap Smear kwa ajili ya uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi. Kwa wanaume, huchunguzwa maeneo ya siri ili kuona kama kuna vinyama hivi vimejitokeza.

Akina baba vioteo hivi hutokea zaidi kwenye uume, ngozi ya korodani, eneo la mitoki, mapajani pamoja na maeneo ya kuzunguka nje ya njia ya haja kubwa au ndani yake.
Wanaume wanaoambukizwa, wengi wao huwa hawaoneshi dalili zozote za ugonjwa ingawa wanaweza kuwaambukiza wenzi wao bila ya wao kujua.

TIBA NA USHAURI
Ni vema Genital Warts zitibiwe na daktari na haishauriwi kutumia dawa za kununua kujitibu mwenyewe kwa vile kuna uwezekano mkubwa wa kuchanganya aina ya dawa zinazotumika maalum kutibu aina nyingine za Warts.

Zipo dawa nyingi zinazotumika kutibu ugonjwa huu kama vile Podophyllin na Podofilox, Trichloroacetic acid (TCA) au Imiquimod. Mgonjwa anaweza pia kutibiwa kwa kufanyiwa upasuaji mdogo.

Anayetibiwa ugonjwa huu anashauriwa awe na mwenza wake anayeshirikiana kimapenzi ili wote wapate tiba kuepuka kuambukizana.

Kwa wanawake ambao wametibiwa Genital Warts na kupona au wale ambao wamewahi kuwa na wenza waliowahi kuugua ugonjwa huu, wanashauriwa kufanya uchunguzi wa mara kwa mara wa shingo za kizazi kila baada ya miezi 4 mpaka 6 tangu kupata matibabu ya awali ya ugonjwa huu, hasa kama wana dalili ya kupata kansa ya kizazi.

Bado tunasisitiza kwamba ni muhimu kuchukua hatua za kujikinga wakati wa kujamiiana na mtu ambaye humfahamu au kujua afya yake.

Kwa wanaume ugonjwa huu unaweza kusababisha saratani ya uume, yaani Cancer of the penis au saratani ya njia ya haja kubwa, kitaalam Anal cancer.

Tofauti na magonjwa mengine ya zinaa, matumizi ya kondomu hayana uhakika wa asilimia mia moja katika kukukinga dhidi ya HPV kwa sababu virusi wa HPV au vinyama vinaweza kuwa nje kwenye ngozi ambayo uwezekano wa kugusana ni mkubwa.
Pamoja na hayo, bado kondomu inaweza kupunguza hatari ya kuambukizwa ugonjwa huu ikiwa tu itatumika vema mara zote unapokutana kingono na mwenza usiyemfahamu kiundani kiafya.

Inashauriwa kuwa wanawake wote wenye umri wa miaka kati ya tisa mpaka 26 wapate chanjo dhidi ya virusi wa HPV ili kuzuia uwezekano wa kuambukizwa.


Loading...

Toa comment