MAUMIVU ya mara kwa mara ya tumbo ni yale ambayo yanampata mtu kwa muda mrefu au kwa vipindi yaani yanakuja na kupotea yenyewe au yanapotea baada ya kunywa dawa na kurudi tena. Maumivu ya aina hii ndiyo tunayaita maumivu sugu ya tumbo na huweza kukutia gharama kubwa kuchunguza na kutibu endapo hutalichukulia kwa umakini. Tatizo hili la maumivu sugu ya tumbo humpata mtu yeyote, mwanamke au mwanaume, mkubwa au mdogo. Maumivu haya husumbua kwani huwa hayaishi, yaani yanatulia kwa muda fulani na kurudi tena. Maumivu yanaweza kuwa upande wa juu wa tumbo au upande wa chini na yanatulia kwa vipindi na kurudi yakiwa makali au madogo, lakini hayaishi.
TATIZO LINAVYOTOKEA
Kama tulivyoona, humtokea yeyote, mwanamke au mwanaume, utokeaji wake hutofautiana kwa jinsi. Kwa mwanaume vyanzo vya maumivu haya vinaweza kuwa hernia au ngiri au matatizo kwenye korodani, lakini kwa wote vyanzo vinaweza kuwa vidonda vya tumbo, matatizo ya mkojo, kidole tumbo, matatizo ya utumbo mkubwa, kukosa au kufunga kupata haja kubwa, gesi kujaa tumboni. Yapo mengine kama kuwa na mawe kwenye mfumo wa mkojo au kifuko cha nyongo, matatizo ya ini na mengineyo.
Kwa upande wa wanawake, matatizo hutokea zaidi chini ya tumbo na uhusisha kibofu cha mkojo kama ilivyo kwa wanaume, mfuko wa uzazi, mirija ya uzazi na vifuko vya mayai. Magonjwa yanayosababishwa na maumivu haya hutofautiana kwa kiasi kikubwa kuanzia vyanzo hadi dalili.
Vyanzo vya matatizo katika sehemu ambazo magonjwa yanatokea yanaweza kuwa maambukizi (infections), uvimbe, kuumia na athari zitokanazo na madawa, vinywaji, vyakula na hata kuumia iwe kwa ajali au upasuaji. Kwa upande wa wote, wanawake na wanaume, ugonjwa huambatana na dalili mbalimbali, mfano kwa mwili kudhoofika, kupoteza hamu ya kula na hata kupoteza hamu na uwezo wa kufanya tendo la ndoa.
Wanawake ndiyo waathirika wakubwa wa tatizo hili la maumivu kwa kuwa wana viungo vingi katika mfumo wa uzazi. Matatizo katika viungo hivyo ni kama vile maambukizi ndani ya kizazi yanayotokana aidha na utoaji wa mimba au maambukizi ya ukeni. Maambukizi haya huweza kusambaa hadi katika mirija ya uzazi na kuathiri mfumo wa uzazi. Uwepo wa uvimbe katika viungo vya uzazi vya mwanamke mfano uvimbe wa ‘fibroid’ au aina nyinginezo, huweza kusababisha maumivu ya daima au ya kuja na kupotea.
Tatizo hili linahitaji uchunguzi wa kina kwa athari kubwa kutokana na kupoteza uwezo wa kushika ujauzito.
DALILI ZA TATIZO
Kama tulivyoona hapo awali, dalili za tatizo hili hutofautiana kati ya mtu na mtu hata kijinsia. Mtu mwenye vidonda vya tumbo hulalamika maumivu ya tumbo juu ya kitovu ambayo husambaa hadi mgongoni na huambatana na kiungulia au moto kifuani, mtu mwenye matatizo ya ini tumbo huuma sana upande wa kulia kwa juu na wakati mwingine tumbo hujaa au kuvimba.
Matatizo katika njia ya mkojo huambatana na maumivu chini ya tumbo yanayozunguka upande wa ubavu wa kulia au kushoto, maumivu ya mkojo au kutoa mkojo wenye rangi ya njano kila siku. Kwa ugonjwa wa kidole tumbo au ‘Appendicitis’, maumivu huwa chini ya tumbo upande wa kulia usawa wa kati ya kitovu na nyonga ya kulia.
Maumivu yanayohusiana na viungo vya uzazi vya mwanamke huwa daima chini ya kitovu na yanaweza kusambaa kulia na kushoto, wakati mwingine huambatana na kutokwa na uchafu ukeni, maumivu wakati wa tendo la ndoa au wakati wa hedhi. Maumivu haya ni vema yakaangaliwa kwa kina kwani yanaweza kuwa makali na ghafla mfano mimba kutunga nje ya kizazi au kidole tumbo.
UCHUNGUZI, TIBA NA USHAURI
Maumivu ni kitu kigumu kwani tiba bila kujua chanzo chake huwa ngumu. Ni vizuri kutopendelea kunywa dawa za kutuliza maumivu bila kujua hasa chanzo cha tatizo. Ni vizuri uende hospitalini mara unapohisi maumivu ya tumbo na endapo tatizo lako ni la muda mrefu, basi waone madaktari bingwa katika kliniki maalum kwa uchunguzi makini na matibabu.
Comments are closed.