The House of Favourite Newspapers

Kuzimu Na Duniani-10

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
Lakini licha ya kuziba masikio, bado nilisikia maumivu makali sana. Kumbe kinachochoma si kusikia jina bali hata likitajwa jirani na wewe pia tosha. Nikasema kwa sauti mamaaa! Mke wangu akasimama, akanishika mabegani.
SASA ENDELEA MWENYEWE…

“Nini tena jamani?”
Kilichoendelea hapo sikumbuki, ni kama nilipoteza fahamu lakini nilipokuja kuzinduka, nilimwona mke wangu akilia kwa uchungu huku akiwa amepiga magoti na kulalia kitandani kwa upande wa kifuani huku akisali.

Alipobaini nimezinduka, alikaa na yeye kitadani, akaniangalia kwa macho yenye huruma na wasiwasi kisha akasema:
“Unajua saa hizi ni saa ngapi?”

Niliangalia saa nikabaini ni saa sita na dakika kumi na mbili mchana. Nilishtuka sana, nikaangalia nje kwa kutoamini, nikamtajia muda kama alivyoniuliza. Akaniuliza tena.
“Unajua kilichotokea kwako?”
“Sijui mke wangu, waweza kunisimulia ukitaka lakini kama hauko tayari hata mimi sitakulazimisha,” nilimwambia hivyo.

Lakini wakati nasema hivyo, nilikumbuka kwamba, nilishaonywa na wale viumbe kuhusu kuzungumzia mambo ya kule nilikokuwa lakini pia nikajisemea moyoni kwamba, haitawezekana niwe na hatia wakati anayesimulia hali ilivyokuwa ni mke wangu na si mimi na wala yeye hajui hali ilikuaje kule.

“Mume wangu kwanza pole sana. lakini pili, najua yote yaliyokupata si wewe bali ni nguvu iliyokuzidi. Mchungaji alikuja hapa, mimi nilimfuata baada ya kuona hali yako inazidi kuwa mbaya.

“Alipofika akakufanyia maombi, ukaanza kusema mambo makubwa sana na ya kushangaza. Kwa kweli, mimi mwenyewe nilikuwa nakuogopa sema mchungaji alinipa ujasiri hasa baada ya kuomba sana.

“Sikumbuki ni lini ulikuwa haupo hapa nyumbani kwa siku kadhaa, lakini ulisema ulisafiri kwa siku kadhaa kwenda kwenye makazi ya majini lakini kwa mchungaji ndivyo ulivyosema na mchungaji alisema ile haikuwa kauli ya akili zako ila maombi yake.
“Mume wangu ukiwa kwenye makazi ya majini, ulifundishwa mambo mengi lakini kubwa walikutana wewe uwe wakala wao wa hapa duniani.”

Wakati mke wangu ananisimulia hayo, mwili ulikuwa unasisimka kwa sababu nilijua siku zangu za kuishi hapa duniani ziliisha. Maana ilionesha katika kuombewa kwangu na mchungaji, nilisema siri zote za kule ujinini. Nilitamani nimwambie mke wangu asitishe maelezo yake ili niwe na amani.

“Ulisema kule ujinini ulipelekwa na wanawake watatu waliokubeba pale Huindini. Mchungaji alishangaa sana, yaani mume wangu ulinena mambo mazito sana.”
“Mke wangu, achana na hayo mazungumzo, we huamini kwamba nilisema kwa sababu nilikuwa sijitambui. We mwenyewe si umesema hujawahi kuniona sipo hapa nyumbani?”

“Ndiyo na mimi nikashangaa hapo.”
“Basi ujue kwamba, nilisema kwa maneno ya kuweweseka kama vile nilikuwa naota njozi.”
“Itakuwa kweli mume wangu. Lakini mimi bado nina maswali mengi kuhusu wewe, hasa siku mbili hizi.”

Wakati tunaendelea kuzungumza na mke wangu akinisimulia nilivyokuwa naanika mambo ya kule ujinini, ghafla wanawake wawili walitua mle ndani, wakasimama kwenye kona ya mlango. Nilitaka kushtuka, wakanionesha ishara niwe mtulivu.
Niliwakumbuka ni wawili kati ya wale watatu walionipeleka ujinini. Nikatulia kimya mke wangu akauliza:

“Mbona kama nasikia harufu ya manukato?”
“Hata mimi,” nilimjibu.

“Labda kuna watu wanapita nje,” alisema yeye. Mimi nikakaa kimya.
Nilijua kuwa, manukato yale yalitoka kwa wale wanawake walioingia.
“Lakini mume wangu nilikwambia kwamba ulikuwa unaota, kuna wanawake wakasikika wakikupongeza kwa kazi nzuri, hivi we hujiulizi ni vipi? Kwa nini mimi niwasikie watu unaoongea nao kwenye simu?”

Kabla sijamjibu, mwanamke mmoja kati ya wale alisema kwa sauti:
“Kwa swali hilo kaa kimya tafadhali!”
Nilishtuka nikiamini kwamba, sauti ya yule mwanamke ilisikika vyema na mke wangu kwani alizungumza Kiswahili sawasawa na kwa sauti ya juu.

Lakini cha ajabu, nikamwona mke wangu akiangalia juu ya paa la nyumba na kusema kuwa kuna upepo mkali umepita. Mimi nilikaa kimya!
“Kwa hiyo wewe mume wangu kwa mtazamo wako huna baya la mambo ya majini?”
Yule mwanamke akasema tena kwa sauti ya juu:

“Mjibu hakuna baya na asiendelee kuuliza.”
Kabla sijamjibu mke wangu, nikamwona anainua tena kichwa kuangalia juu. Akasema:
“Mbona kuna upepo unatikisa bati na kupita, unatokea wapi?”
“Mimi sijui. Lakini kuhusu swali lako kwamba hakuna baya la majini, mimi naona hakuna baya mke wangu.”

“Unataka kusema mchungaji wangu anayetumia damu ya Bwana Yesu kuomba, maono yake si ya kweli?”
Niliwaona wale wanawake wakipepesuka, mikono wakaikinga kama wanaokwepa joto la moto uliokokwa.
Usikose kusoma mwendelezo wake wiki ijayo kwenye gazeti hilihili.

Leave A Reply