The House of Favourite Newspapers

Kuzimu Na Duniani-20

1

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
Lakini ukiachana na hayo, lingine ni hayo maeneo ambayo yalitajwa kuwa ni hatari. Niliifikiria njia panda ya kwenda Tosamaganga, nikaufikiria mji wa Mkimbizi kwamba una wakazi wanaowasumbua majini. Lakini hapa sikuwa makini kujua hasa wanasumbua kivipi!

Ghafla mawazo yaliyonijia ni ya mke wangu. Kwamba, kule alipo, akirudi kutoka kwenye maji na kutonikuta, atajua nimekwenda wapi na kufanya nini.
“Kila mmoja atege sikio sasa ili tuelekezane,” ile sauti ilisema. Nikashangaa kwamba kumbe wote tulishatoka nje. SASA ENDELEA MWENYEWE…

Maelekezo yalitoka kwamba, kila mmoja alipo atajikuta yupo kwenye kundi linalomhusu na kwamba, huko atapatiwa maelekezo na msisitizo na baada ya hapo, kila mmoja ataoneshwa sehemu ya kuishi. Hiyo sauti ilisisitiza hivi:

“Napenda kuwaambia wazi kwamba tuna vita kubwa lakini ni lazima tushinde. Kuwaachia wanadamu wakamcha Mungu wao, kwetu sisi ni hatari sana. Dunia ipo katika nyakati ya haraka kuelekea kwenye hitimisho lake, lazima tupate wengi.”

Sauti hiyo ilipoacha kusema, mimi nikajikuta nimo ndani ya chumba kimoja chenye giza nene. Lakini kelele ziliashiria kwamba, mle ndani sikuwa peke yangu.

Lakini wasiwasi wangu mkubwa ulikuwa ni je, ni akina nani ambao nilikuwanao ndani ya kile chumba? Maana hewa ilikuwa nzito sana ndiyo maana nasema kwamba, nilikuwa ndani ya chumba.
Mbaya zaidi, kelele zenyewe zilikuwa hazijulikani ni za nini? Yaani sauti zilizokuwa zinasikika, hazikuweza kunipa nafasi ya kujua kilichokuwa kikiongelewa!

Nilisikia kama watu wakisema: “Poleke…pikapika…kuwekokuweko…jumbi ilo…jumbi ilo…poleke pikapika…kuwepokuweko…jumbi ilo…jumbi ilo.”

Nilitega sikio kwa umakini sana, mara kukawa kimya! Hapo pia nilibaini kuwa, hata kama kweli nilikuwa ndani ya chumba lakini nilikuwa peke yangu. Zile kelele ni za mazingira ya mle ndani tu na hayakutokana na kiumbe chochote kuwemo.

Pia nilijua niko peke yangu baada ya kunyoosha mkono wangu wa kulia upande wa kulia, mbele na nyuma na wa kushoto vivyohivyo bila kushika kitu chochote kile.
“Upo peke yako lakini upo salama sana,” sauti nzito na nene ilisema huku ikiacha mtetemesho mkubwa.
“Sawa,” nilijibu.

“Wewe umechaguliwa kwenye kitengo cha kulisha majini kile chakula chao maalum,” ile sauti ilirudia kusema.
Nilishtuka kidogo kusikia hivyo kwani sikujua maana ya kitengo cha chakula cha majini tena kile maalum ndiyo chakula gani!

Utakuwa unahusika moja kwa moja na kuleta chakula hicho huku ukiwa kama wakala mkuu. Usichangamane na wengine. Wewe eneo lako litakuwa kwa wanawake wenye mimba tu,” ilisema hiyo sauti.

Baada ya kumaliza kusema maneno hayo, niliambiwa kitakachofuata sasa ni kuelekezwa kwa vitendo na si sauti tena kama awali.
Nilijikuta nipo kwenye chumba chenye wanawake wengi wenye mimba wakilia kwa machozi huku wakionekana kuombeleza na vilio vyao hivyo kwamba waonewe huruma.

Kiumbe mmoja kama binadamu kwa mbali, ila yeye mnene, hana shingo. Kwa maana kwamba, sehemu ya shingo ilijaa na kuwa sanjari na mabega, akiwa na macho ya pembe tatu huku meno yakitoka kwa nje kama ya mnyama ngiri, alikuwa akimfuata mwanamke mmojammoja na kumshika tumboni kisha mwanamke huyo hulia sana na kuanguka chini na kufuatia na damu nyingi kusamba sakafuni.
Alifanya hivyo kwa kila mwanamke mpaka wakaisha wote na walikuwa kama wanawake hamsini mle ndani. Alipomaliza aliingia kwenye chumba kimoja cha pembeni bila kuniangalia.

Baada ya muda, wakatoka viumbe kama yeye, wawili wakiwa wamebeba beseni kubwa lililojaa damu mpaka kumwagika. Wakaliweka chini kisha wakarudi kwenye kile chumba.

Mara, wakatoka viumbe wengine watatu. Wao walikuwa wakubwa zaidi kimaumbile na walivaa tofauti na wale waliotangulia. Walionekana kama ndiyo mabosi wao. Wakaja kusimama pembeni ya lile beseni, wakaangalia kisha wakaondoka na kuingia kwenye chumba kingine upande wa kushoto.
Walipozama tu, wakaja wale watu wawili, wakalichukua lile beseni. Wakaingia nalo kwenye kile chumba walichoingia wale niliosema ni kama viongozi wao kwa jinsi walivyovaa.

Kufumba na kufumbua na mimi nilikuwa kwenye kile chumba walichoingia wale viongozi na wale wenye beseni lenye damu. Lakini wale waliopeleka damu hawakuwepo.

Nilifikia kwa kusimama wima. Nikawaona wale watu wakubwa wakianza kunywa ile damu kwa kutumia vikombe vyekundu ambapo walikuwa wakichota na kupeleka kinywani huku wakicheka sana kuashira kwamba, walichokuwa wakikipeleka kinywani kilikuwa kikiwafurahisha sana.

Je, wewe msomaji unajua kilichotokea? Usikose kusoma wiki ijayo kwenye gazeti hili.

1 Comment
  1. Prince'kabagala says

    tuzidi kuomba sana

Leave A Reply