Kuzimu Na Duniani-3
Nilifika kazini kwa muda uleule wa kawaida. Nilipenda sana kuwashirikisha wafanyakazi wenzangu juu ya tukio lote la jana kwenye ndoto lakini kila nilipofikia hatua ya kutaka kusema, nilikuwa nasita au kujisikia hali ya kupuuzia.
ENDELEA SASA…
Muda wa kazi ulipokwisha, nilijiondoa kazini. Mbele barabarani likatokea gari la Sido, dereva akasimamisha maana tunafahamiana, nikapanda kwa ajili ya kuelekea mjini.
Tulipofika kwenye kona ya barabara ya kwenda mjini Iringa na ile inayonyoosha kwenda Morogoro Dar au niseme ile inayokwenda kitongoji cha Ndiuka, sasa dereva anakata kushoto. Gari lilitoa mlio mmoja wa puu! Dereva akasimama pembeni.
Tulishtuka wote, tukashuka kwenye gari na kwenda mbele kuangalia kuna nini. Dereva alifungua boneti na kuangalia lakini hakubaini kitu. Mpaka hapo, gari halikuwa limezima wala kuonesha dalili kwamba haliwezi kuendelea na safari.
“Jamani, haya ni magari tu. Ni chuma, kwa hiyo na vyuma pia huwa vinachoka,” alisema dereva wakati akiingia kwenye gari. Na sisi wengine pia tukaingia kwa mwongozo wake huo.
Safari ilianza, gari likatembea hadi kufika kwenye kuanza kupanda kilima cha kwenda mjini. Cha ajabu sasa, gari lilipofika usawa wa ile njia ya kufika mjini kwa miguu, likalia tena puu! Safari hii likasimama kabisa kwamba haliwezi kuendelea tena na safari.
Tulishtuka tena wote, dereva akaangalia mbele akasema haoni tatizo. Akarudi ndani na kupiga stati, halikuweka.
Tulianza kuuliza cha kufanya. Dereva akasema sisi kama tunaweza tukatize njia ya kwenye kilima kwenda mjini yeye anasubiri magari mengine ya Sido kwa imani kwamba, atapata msaada wowote ule.
Abiria wengine walikataa kwenda mjini kwa kupanda kilima hicho kasoro mimi tu ambapo niliwadanganya kwamba kwa vile nina safari ya kwenda kitongoji kinaitwa Frelimo halafu pia kitongoji kingine kinaitwa Mkimbizi hivyo lazima niwahi. Wakakubali.
Nilipanda kilima. Lakini nilipofika umbali wa kama mita hamsini tu, gari likawaka. Nilishtuka, kidogo nirudi lakini moyoni nikasema acha waende, pangine mimi ndiyo nina mkosi. Naweza kusema narudi kupanda, mbele kidogo likaharibika tena.
Basi, nilizidi kupanda kilima. Lakini niseme wazi kwamba gari lilipowaka, niliwasikia wakicheka halafu mmoja wa abiria akasema waziwazi; ‘unajua abiria wengine wana mikosi bwana’. Niliumia sana, sikujali.
Mbele yangu alikuwa anashuka mwanaume. Lakini pia nyuma yake kulikuwa kuna mwanamke anamfuata. Walionesha hawakuwa safari moja.
Nilianza kupishana na mwanaum e, akanipa pole ya kazi kwa kabila la Kihehe.
“Makasi.”
“Hale,” nilimjibu tukiwa tumeshapeana migongo. Sasa mbele yangu nilikuwa nakabiliana na yule mwanamke. Yeye alionekana kama anapunguza mwendo kwa mambo mawili. Kwanza, anataka nipite mimi kwanza, kwa sababu sehemu hiyo ilikuwa finyu. Pili, alikuwa akinifahamu, sasa alitaka tusimame wote ili tusalimiane.
Kwa hiyo hali hiyo ilinifanya na mimi nipunguze mwendo mpaka nikasimama kabisa. Tulikutana macho, akatabasamu na kusema:
“Unanikumbuka?”
Nilikunja sura kumfikiria nilimwona wapi na kitu gani kilichotufanya tukutane lakini sikupata jibu.
“Hapana,” nilimkatalia.
“Asubuhi?” aliuliza hivyo tu basi.
“Asubuhi imefanyaje?” nilimuuliza.
“Ulikuwa unatoka pale sijui kwako,” alisema.
Niliinua kichwa chini na juu kama ishara ya kukumbuka alichosema.
“Oohooo! Umeshindaje?”
“Nimeshinda salama. Nakuona unatoka kazini!” alisema.
“Eee. Kumbe unaishi huku Ipogoro?” nilimuuliza nikimkazia macho. Nikabaini kwamba, alikuwa na macho meupe sana kama karatasi na kile kiduara cheusi kilikuwa cheusi sana kama mkaa.
Lakini pia nilibaini kwamba, nyusi zake zilikuwa nyingi kiasi cha urefu wa kama nywele za kichwani zilizopunguzwa.
Nahisi alilijua hilo, kwamba nimebaini kitu usoni mwake maana alikimbiza macho pembeni, akasema:
“Mimi naishi Tagamenda.”
Tagamenda ni eneo lenye kituo cha umeme wa Tanesco. Lakini ni mbali kidogo. Ina maana yeye anashuka mpaka Ipogoro kisha anapanda gari pale.
“Sawa. Mimi pale uliponiona asubuhi ndiyo maeneo ya nyumbani kwangu,” nilimwambia, akasema anajua kama mimi naishi pale.
“He! Kumbe wewe si mgeni wa eneo lile?” nilimuuliza.
“Hapana. Si mwenyeji sana bali kuna mwanaume anaishi pale na tuna kazi naye maalum.”
“Mnaishi naye wapi?” nilimuuliza.
“Pale ulipotoka wewe,” alisema.
Muda wote huo hakukuwa na mtu aliyekuwa akishuka wala kupanda. Na si kawaida.
“Mimi pale ni kwangu, naishi na mke wangu na mabinti zangu watatu, sina mpangaji wala ndugu mwingine wa kiume. Sasa huyo unayemsema wewe ni yupi?” nilimuuliza kwa sauti yenye maswali kibao.
Je, unajua nini kilitokea? Usikose kusoma wiki ijayo kwenye gazeti hilihili.