The House of Favourite Newspapers

Kuzimu Na Duniani-8     

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:

“Kama anakubali, kama anabisha. Lakini nimeshamwambia  madhara ya kukataa na faida za kukubali kwake.”

“Nenda kampangie kazi haraka sana na umjulishe na maeneo yake. Atakubali tu.”

SASA ENDELEA MWENYEWE…

Nilishampangia kazi na maeneo yake kiongozi.”

“Kampe maji anywe na umwachie akaanze kazi mara moja. Lakini mpangie siku ya kuleta ripoti yake huku.”

“Sawa kiongozi.”

Nilichukuliwa mpaka kwenye chumba kingine na kufikia kukalishwa chini huku nikiambia kila nitakachoelekezwa lazima nitii.

“Fungua kinywa sasa unywe maji,” niliambiwa.

Nilifumbua, maji ya baridi lakini yenye ladha kama ya sukari guru. Nilikunywa kiasi cha lita kama mbili mpaka nikashiba sana na tumbo kuwa gumu.

“Haya, tayari sasa,” alisema aliyekuwa akininywesha maji hayo.

Nilipomaliza akaondoka na kuniacha kwa muda huku nikiwa sijui alikwenda wapi. Niliwaza mengi kwa harakaharaka ikiwemo kutaka kuamua kutoroka, lakini nikasikia kama sauti ikiniuliza ‘utatorokaje humu ndani?’

Kweli, niliamua kuachana na wazo hilo lakini pia yule mtu akawa amefika na kunishika mkono wa kushoto, akaniambia twende huku.

Tukatoka, tukatembea wee mpaka tukafika kwenye eneo moja ambalo lina uwanda. Yaani hakuna mlima, hakuna bonde, hakuna kichaka wala hakuna msitu. Ni majani kama bustani.

Nilimuuliza tunakwenda wapi, maana hapo niligeuka kuangalia lile jumba nililoingizwa, sikuliona na ndiyo nikajua kwamba tulitembea sana.

“Wewe unataka kwenda wapi?”

“Nyumbani,” nilimjibu naye hakusema lingine lolote.

Tulifika mahali kwa mbele nikaona kama tukiendelea kwenda tutaingia kwenye lango moja kuu. Nikawa natembea huku namwangalia yule mtu kutaka kujua ataniambiaje! Lakini hakuniambia kitu mpaka tulipolifikia lile lango.

“Ingia hapo,” aliniambia.

Nikatembea kulielekea lango, likafunguka nikazama ndani ambapo nilikutana na giza nene tena la kutisha.

“Sasa endelea kwenda,” sauti nyingine iliniambia. Sauti hii ilitokea mle ndani kwenye kiza kinene. Kwa hiyo hata sikujua aliyeongea alifananaje kimaumbile ila ilikuwa ya mwanaume mzee!

Niliendelea kutembea kama nilivyoelekezwa huku pia nikiwa sijui nakanyaga kwenye nini wala kutambua nitaishia wapi.

“Hapo kata mkono wako wa kushoto,” sauti nyingine, hii ilikuwa ya mwanamke, iliniambia.

Nilitii na kukata kushoto.

“Hapo nyoosha sasa, usikate tena kushoto kwa usalama wako,” hii nayo ilikuwa sauti nyingine, tena ya mwanaume mwenye nguvu zake.

Kusema kweli nilijitahidi sana kukaza macho nikiamini naweza kuona chochote lakini kadiri nilivyokuwa nikifanya hivyo, ndivyo giza nene lilivyozidi kunizuia nisione kitu mbele yangu.

“Simama hapohapo, usiinue mguu wako kwenda kokote,” sauti hii ya safari hii ilikuwa ya amri zaidi kuliko maelekezo ya kiutu. Nikasimama ghafla.

“Sikia, uliyoyaona, uliyofanyiwa huku yanatakiwa kubaki kuwa siri ya wewe peke yako. Uhai wako uko mikononi mwako mwenyewe. Ukisema siri hii kwa mtu yeyote, siku hiyohiyo roho yako itakuwa halali yetu. Kwa heri, safari njema na kazi njema,” ilisema sauti hiyo ya amri.

Kwa kuwaza kawaida, nilitembea kama kwa nusu saa nzima ndani ya kiza kile kinene nikafika mahali ghafla nikaona kama lango linafunguka na kuona nje kweupe na shughuli za wanadamu zikiendelea.

Nilishtuka zaidi baada ya kujikuta natembea kwenye ardhi hii ya duniani. Nikageuka kuangalia lile lango, sikuliona. Nilijitahidi kujua pale nilipo ni wapi, nikabaini ni maeneo ya Gangilonga.

Ilikuwa yapata saa kumi na mbili jioni kutokana na mwonekano wa jua. Nikajiuliza ina maana nilikotoka nilikuwa kwa siku ngapi? Nikapata jibu moja kwa vile sikulala wala sikuhisi usingizi.

Nilibaini pia kwamba, nilikuwa nimetokea kwenye nyumba za eneo hilo ambazo zipo jirani na milima. Hivyo nilitembea kwa mwendo wa kuchoka mpaka nikafika eneo la Shule ya Msingi Gangilonga.

Je, kilifuatia nini? Usikose wiki ijayo hapahapa.

Leave A Reply