Kuzimu na Duniani

KAMA kweli kuna malipo ya ubaya na uovu basi mimi nililipwa kwa yale ya uovu. Lakini namshukuru sana Mungu kwani alijua dhamira yangu ikafika mahali akakataa hivyo akaamua kuniokoa mwenyewe kutoka kwenye mateso ambayo mimi nilijua ni ufahari,” anasimulia Mussa Kibwana kuhusu mkasa wake wa kutisha wa namna alivyokuwa akitumika kuchukua roho za watu na kuzipeleka kwenye mateso.

Ilikuwa Jumapili moja, miaka ya 90, saa kumi jioni nikiwa natoka kazini, Ruaha, Iringa narudi nyumbani eneo moja linaitwa Mlandege.

Kwa miaka ile usafiri mkubwa wa mji wa Iringa ulikuwa ni mabasi ya kutoka Iringa mjini kwenda eneo linaitwa Tanangozi, hivyo kwa wafanyakazi wanaofanya kazi Ruaha ili warudi mjini ilikuwa lazima wasubiri usafiri huo kwa muda.

Tofauti na sasa ambapo kuna vibasi vinatoka mjini na kumalizikia Ipogoro au mpaka Kibwabwa.

Basi, mimi siku hiyo niliamua kurudi mjini kwa kupitia njia ya mkato. Njia hii inakatisha kwenye mawe makubwa kutoka Ipogoro hadi eneo linaitwa Kitanzini kisha naingia eneo linaitwa Mshindo na kupanda basi hadi Mlandege.

Nikiwa nimemaliza nusu ya safari, nilikutana na mwanamke mmoja amesimama. Nilijua amechoka kwani kwenda mjini kutoka Ipogoro unapanda mlima. Ni kawaida ya wapandaji wengi kupumzika au kutembea polepole mpaka wanaumaliza mlima huo.

Nilimsalimia mwanamke huyo na kumpa pole kwa safari, akasema hataki pole yangu kwa sababu alikuwa ananisubiri mimi.

Nilishangaa sana kwa vile sikumfahamu au niseme sikuwa namkumbuka mwanamke huyo. Ilibidi nisimame na kumkazia macho kwa maana ya kuitafuta sura yake kama ningeweza kumkumbuka, lakini wapi!

Alivaa gauni la kuishia miguuni lenye mchanganyiko wa rangi mbalimbali za maua. Nikamuuliza:

“Kwani mwenzangu unaitwa nani na unanisubiri kivipi?”

“Mimi naitwa Maua. Nakusubiri maana nimekuona unavyopanda, mimi naogopa kupanda peke yangu,” alisema mwanamke huyo.

Maneno yake niliyaona kama ni ya ulaghai tu, niliamini  kuna ambacho kiko nyuma ya hapo. Mlima ule watu ni wengi, japo si sana. lakini kwa muda ule wa saa kumi haikuwa rahisi kutokuwepo kwa watu, kwani mara nyingine hata saa mbili usiku watu wanapanda na kushuka.

Basi, nilimwambia siamini maneno yake kwa vile hakuna kitu ambacho kingemfanya aogope. Tena wakati namkuta, kuna watu wawili walikuwa nyuma yangu na mbele yake niliwaona wanawake watatu wakipanda huku wakizungumza kwa sauti.

Lakini swali jingine ni kwamba, aliposema alikuwa akinisubiri mimi alijuaje kama nipo nyuma yake kwani mlima wenyewe una konakona. Alikosa jibu la moja kwa moja akabaki akisema alikuwa anajua lazima kuna mtu anakuja.

Tulitembea wote, yeye akiwa kushoto kwangu mpaka tukawa tunakaribia kufika. Akaniambia yeye amefika tayari. Nilishangaa kwani tulikuwa hatujatokea kwenye nyumba za wakazi.

Nilimuuliza anakoishi akanionesha kwa mkono upande wa kulia wakati wa kupanda ambako kuna mawe na mitimiti. Kifupi ni kichakani kwa wakati huo.

“Sasa pale unaishi wapi?” nilimuuliza.

“Unataka kuona?”

“Ndiyo.”

Hapo tulikuwa tumesimama, akasema nimwangalie anapokwenda kuingia. Kweli, alitembea kwenye kichaka huku nikiwa namshangaa. Mimi moyoni mwangu niliamini yule mtu alikuwa na mambo mawili, mchawi au hana akili nzuri. Lakini mwonekano wake haukuashiria kwamba hana akili nzuri.

Ghafla nikamwona anaingia kwenye jumba moja kubwa sana. limepakwa rangi nyeupe lote huku sehemu ya madirisha ikizungushwa na rangi nyekundu. Nilifikicha macho ili nione vizuri lakini nikaendelea kuona kichaka kisha kicheko kutoka upande ule.

Si mimi tu, hata ungekuwa wewe ungetoka mbio. Basi mimi nilitoka mbio, tena mbio kama nafukuz   wa na simba wakati kumbe niliyoyaona yalifutika machoni pangu. Nikatokezea kwenye sehemu watu wanauza vyakula mbalimbali na ndiyo eneo linaloanza kuitwa Kitanzini.

Baadhi ya watu ambao wao ndiyo walikuwa wakianza kushuka, wakaniuliza kinachonikimbiza, lakini sikuwajibu.

Niliingia mitaani mpaka nikafika Mshindo na kupanda gari hadi Mlandege.

Nilifikia kujitupa kitandani. Mke wangu, akanifuata kutaka kujua kama naumwa kwani siyo kawaida yangu.

“Nilichokiona mke wangu si cha kawaida. Leo ndiyo nimeamini kwamba kuna watu si wazuri.”

“Kwani umeona nini wewe, niambie vizuri.”

Je, unajua nini kiliendelea? Usikose kusoma mkasa huu wiki ijayo.


Loading...

Toa comment