The House of Favourite Newspapers

Kuzungumzia ujamaa kwa sasa ni kupoteza wakati!

Na Walusanga Ndaki| Uwazi|Nionavyo Mimi

KUNA baadhi ya Watanzania -hususan wanasiasa na mashabiki wa siasa – ambao hufikiri kwamba, ukitaka kuheshimiwa na Watanzania, jambo rahisi la kufanya ni kuzungumzia na kusifia tu siasa ya Ujamaa ambayo ilianzishwa nchini mwaka 1967 chini ya utawala wa aliyekuwa kiongozi wa nchi hii, Mwalimu Julius Nyerere.
Kwa kifupi, watu hao hufikiri kwamba ukitaka kupata sifa alizopata Mwalimu  Nyerere, ni kupanda jukwaani tu na kuutukuza ujamaa, ukaulaani ubepari na mabepari, ukashuka jukwaani,  basi!
Kwa wasioelewa,  neno Ujamaa, kwa Kiingereza ni ‘Socialism’ au ‘Communism’.  Pamoja na tofauti katika majina,  maneno hayo, yanamaanisha  kitu  kilekile.  Kwa kifupi, Ujamaa kama Socialism na Communism (Ukomunist) ni nadharia ya kisiasa na kiuchumi ya jamii ambamo njia kuu za uzalishaji, ugawaji na mabadilishano ya kifedha na kadhalika vinakuwa mikononi mwa umma.
Huo ndiyo ujamaa ambao uliivuruga Tanzania kisiasa na kiuchumi na kuifanya irudi nyuma kimaendeleo tangu mwaka 1967 hadi ulipotupiliwa mbali na watu walewale waliokuwa katika chama tawala cha Tanganyika African National Union (Tanu) hadi Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya mwasisi wake mkuu, Julius Nyerere kuondoka madarakani!  Ni kwa vile uzalishaji bidhaa na utoaji huduma nchini ukawa chini ya serikali.
Ni siasa ambayo iliifanya serikali kujikita katika mambo mengi ambayo yangeweza kufanywa na mamilioni ya Watanzania binafsi katika kuchangia ukuaji wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya nchi hii.  Ni siasa ambayo ilikuwa imedhamiria maduka yote – makubwa na madogo – yawe ya serikali au ya ushirika, badala ya kuendeshwa na watu binafsi!
Mfano mwingine wa serikali kujitwisha mzigo huo ulikuwa ni usafiri.  Serikali ilianza kuyaua makampuni binafsi ya usafirishaji wa abiria, mizigo na kadhalika kwa kuanzisha makampuni yake ya  usafiri kama vile Kampuni ya Mabasi ya Taifa (Kamata), kampuni za usafirishaji za mikoa (Regional Transport Companies – RETCO), kumbi za starehe kama vile Dar es Salaam Development Corporations (DDC) na kadhalika!
Huu ndiyo ujamaa ulioacha makovu makubwa kwa jamii tangu vijijini hadi mijini kwa kufanya mamilioni ya watu kuwa masikini hususan kwa kutotumia uwezo,  nguvu  na vipaji vyao  katika kujijenga kihalali kiuchumi , kijamii na kisiasa.
Ni siasa hiyohiyo ambayo imeacha raslimali nyingi za kitaifa zikiwa zimebakia magofu ya kutisha yasiyo na faida leo hii kama vile Kiwanda cha Nguo cha Urafiki cha jijini Dar es Salaam, Kiwanda cha Nguo cha Tabora, Kiwanda cha Nguo cha Musoma, Kiwanda cha Nguo cha Mwatex, Kiwanda cha Nyama cha Kawe (Tanganyika Packers) na kadhalika.
Ni siasa hiyo iliyopunguza nguvu za serikali kutoa huduma kuu kwa wananchi wake, kwani ilikuwa imejikita pia katika kumiliki vimiradi vidogo kama vile bucha za nyama, kuuza chibuku, bia, unga, chakula cha kuku, vitenge na juisi.
Huo  ndiyo ujamaa ambao wanasiasa kadhaa – wakiwemo waliowahi kushika nyadhifa za juu serikalini na katika chama tawala – wamekuwa wakiuzungumzia tu ujamaa kwa sababu wanazojua wenyewe.  Ni watu haohao wanaojifanya kuuheshimu ujamaa leo, wengi wao ni walewale walioshiriki katika kuutupilia mbali  baada ya Nyerere kuondoka ikulu.
Watu hao ambao walikuwa na uwezo na wanaendelea kuwa na uwezo leo hii serikalini na kwenye  chama chao, waliutupilia mbali ujamaa na kurejea katika uchumi wa kibepari ambao umekuwepo duniani tangu enzi za Adam na Eva.
Cha ajabu,  watu haohao ambao bado wana uwezo huo,  wamebakia ‘kupiga domo’ tu badala ya kuchukua hatua na kuuanzisha kama kweli wanautaka!
Ukweli ni kwamba watu hao hawana shida tena na ujamaa, na wanajua kwamba Watanzania wengi  — hasa walioshuhudia madhara yake wakati wa utawala wa awamu ya kwanza — hawana shida na siasa hiyo iliyoibuka duniani mwaka 1917 huko Urusi (ya Kisoviet) na kufa kifo cha mende baada ya miaka ipatayo 70 tu!
Watu hao ambao wamekuwa wakiendesha semina na warsha mbalimbali kuhusu ujamaa wanafanya hivyo wakifikiri watapata huruma na heshima ya Watanzania ambao mamilioni ya watoto wetu, vijukuu na vilembwe wetu wa leo,  hata ujamaa hawakuuona sura yake.
Si hivyo tu, hata majanga yaliyowatia simanzi  baba na mababu zao wakati wa utawala wa Nyerere, hawawezi kuyaamini kuwa yalitokea chini ya utawala wake.
Wanaofikiri watapata heshima kama aliyopata Nyerere afadhali waamke, wasimame na kuanza kutembea.  Kwa nini?  Ni kwa sababu wanaota  ndoto za kuchekesha!   Hawajui au wamesahau kwamba Nyerere aliheshimiwa na wananchi wenzake kwa sababu kuu mbili.
Sababu ya kwanza ni ushupavu wake wa kuongoza mapambano ya wananchi wenzake katika kupigania uhuru wa nchi hii kutoka katika ukoloni wa Waingereza.
Sababu kuu ya pili ni kujishusha kwake na kujitambulisha zaidi na watu masikini nchini mwake na duniani kote, akajitenga na tamaa za utajiri hadi Mungu alipomwita kwake akiwa ni mmoja wa binadamu walioishi maisha ya kawaida licha ya mikono yao kuwa karibu na masanduku ya dhahabu na almasi!
Hivyo, ndivyo vitu viwili vilivyompa Nyerere heshima kubwa kutoka kwa Watanzania na mamilioni ya walimwengu waliomfahamu alichokuwa akikitetea na maisha ya ‘kilofa’ aliyoishi duniani hadi Mungu alipomwita.
Kama kuna kitu kiliibomoa vikubwa heshima ya Nyerere hususan ndani ya nchi yake, ni siasa ya ujamaa iliyoanzishwa na chama chake chini ya Azimio la Arusha mwaka 1967, siasa ambayo nayo iliubomoa vibaya uchumi wa nchi hii na kuwaacha watu wake wakijipanga misururu kila  kona ya nchi kununua viberiti, vitenge, unga, sukari, redio, viatu, sigara – kila kitu!
Ni kwa vile miradi mingi mikubwa ya uzalishaji iliyokuwa inamilikiwa na watu na makampuni binafsi ya ndani na nje, ilitaifishwa na Serikali ya Nyerere, yaani ikawa inaendeshwa na serikali.   Huo ukawa mwanzo wa kuanzishwa kwa mashirika ya umma yaliyojulikana kwa Kiingereza kama ‘parastatal organizations’, magari yake yakiwa na kitambulisho cha (SU – Shirika la Umma kenye namba zake.)
Kwa kizazi cha sasa cha watoto na wajukuu wetu, si rahisi kuwaaminisha kwamba serikali wakati huo ilikuwa inauza kanga kupitia Kiwanda cha Urafiki, viberiti (kupitia kiwanda cha Kibo Match cha Moshi ilichokitaifisha baada ya Azimio la Arusha), ilikuwa inauza Kibuku (kupitia kampuni  ya Chibuku ya Lonrho iliyotaifishwa na Nyerere wakati wa ujamaa), ilikuwa inauza bia kupitia Tanzania Breweries Ltd ( baada ya kutaifishwa  na serikali ya Nyerere  kampuni iliyokuwa inaitwa East African Breweries), ilikuwa inauza unga na mikate, chakula cha kuku na kadhalika,  kupitia Shirika la Usagaji la Taifa (National Milling Corporation) iliyokuwa imetaifishwa  kutoka kwa mmiliki binafsi na kadhalika.
Kutokana na serikali kujitwisha mzigo mkubwa wa kuhudumia watu wake – tangu kuuza chakula cha kuku hadi kujenga mahospitali  na mabarabara – usimamizi na udhibiti wa raslimali za umma katika mashirika hayo ukatoweka.
Kila aliyekuwa na nafasi  katika mashirika hayo  akajikita katika wizi wa mali na fedha, ajira zikawa za holela ambap watu wakawa wanaajiriwa ovyoovyo tu, utaalam katika kuendesha taasisi na mashirika hayo ukatoweka kutokana na waliokuwa wakiyaendesha mashirika hayo kwa ufanisi kuikimbia nchi, na kadhalika.  Matokeo yake, kukawa   hakuna mtu liyekuwa na uchungu na mashirika hayo, kila mtu akawa anasubiri zamu yake ya kuiba!
Matokeo yake, uzalishaji ukashuka, vitu vikaadimika tangu vijijini hadi mijini, misululu ya kununua tangu viberiti, vitenge hadi magari, vikawa sehemu ya maisha ya Watanzania!  Ni kwa vile vitu vyote hivyo vikawa vinazalishwa, kusambazwa na kuuzwa na serikali.  Watu binafsi wakawa hawana fursa pana na za halali za kushiriki katika kujenga uchumi na kutoa huduma kwa wananchi wenzao.

Comments are closed.