The House of Favourite Newspapers

Kuzungumzia ‘ujamaa’ ni kupoteza wakati!

Mwalimu Julius Nyerere (kulia) akiwa na kiongozi wa Jamhuri ya Watu wa China na kiongozi wa Chama cha Kikomunist cha China, Mao Tse Tung.

Na Walusanga Ndaki/GPL

WIKI iliyopita tuliona baadhi ya wanasiasa nchini wanavyoendesha makongamano ya ‘ujamaa’  wakitafuta kusifiwa na Watanzania kuhusu mfumo huo wa kisiasa na kiuchumi ulioanzishwa na kiongozi wa kwanza wa nchi hii, Julius Nyerere, mwaka 1967, endelea:
Ujamaa uliingia nchini kupitia la Azimio la Arusha na chama tawala wakati huo – Tanganyika African National Union  (Tanu) — kufuatia mkutano mkuu uliofanyika Arusha.
Kwa Kiingereza, Ujamaa ambao ni ‘Socialism’ (Usoshalist) na ‘Communism’ (Ukomunist),  ni nadharia ya kisiasa na kiuchumi ya jamii ambamo njia kuu za uzalishaji, ugawaji na mabadilishano ya kifedha na kadhalika huwa mikononi mwa umma. Pamoja na maneno hayo kutofautiana  kimaandishi, kwa vitendo ni kitu kilekile!
Maneno ‘Ujamaa wa Kiafrika’ au ‘Ujamaa wa Kidemokrasia’ ni blabla tu za wanasiasa wasiojua wanachotaka kuwaeleza Watanzania wenzao!
Kupitia ujamaa, serikali ya Nyerere, ilitaifisha mali na njia kuu mbalimbali za uchumi na uzalishaji kutoka kwa aliowaita mabepari, mabwanyenye na makabila – au wanyonyaji – na kuziweka chini ya serikali.  Hivyo ni pamoja na viwanda, majumba, maduka, njia za usafiri za ardhini, majini, baharini, na kadhalika.
Kwa mfano — kwa watu wenye umri mdogo  wanaosoma safu hii — nyumba nyingi za Shirika la Nyumba la Taifa zilizopo leo, ni zilizohamishiwa katika shirika hilo kutoka Shirika la Msajili wa Majumba lililokuwa linamiliki mamia ya nyumba nchini zilizochukuliwa bure mwaka 1970 na serikali ya Mwalimu Julius Nyerere baada ya kuingia kwa ujamaa.
Matokeo ya serikali  kujitwisha mzigo huo wa kuchekesha, uchumi ukakosa ushindani, utaalam na ubunifu.  Uhaba wa bidhaa na huduma ukaenea nchi nzima, watu wakipanga misururu kununua viberiti, sukari, unga, vitenge, kandambili, redio, majani ya chai, na kadhalika!
Ujamaa ukazaa balaa la kiuchumi na kisiasa, ukaibomoa vibaya heshima ya Nyerere, ambapo wakati ujamaa huo unatupiliwa mbali na aliowaacha madarakani,  hakuwa na la kusema.  Tunaendelea…
Kutaifishwa kwa njia zote kuu za uchumi na huduma, kukaanzisha mashirika ya umma (parastatal organizations) magari yake yakiwa na kitambulisho cha SU  yaani Shirika la Umma.
Serikali ikawa inauza viberiti kupitia kiwanda ilichotaifishwa  cha Kibo Match, ikauza Kibuku  kupitia kampuni  ya Chibuku ya Lonrho, ikauza bia baada ya kuitaifisha East African Breweries, ikauza unga, mikate na chakula cha kuku kupitia  National Milling Corporation  – mambo ambayo watoto na wajukuu wetu leo hii hawaamini kama yalifanyika.
Katika tafrani hiyo usimamizi na udhibiti wa mali hizo ukatoweka, hakuna aliyekuwa na uchungu na mashirika hayo, kila aliyepata nafasi akaiba,  ajira zikatolewa kiholela, kila kitu kikawa ‘shamba la bibi’!
Ujamaa duniani ukashindwa kuhimili nguvu ya ushindani wa kisiasa, kijamii na kiuchumi, kama ilivyokuwa katika nchi za kijamaa chini ya chama kimoja -– tangu Urusi, Cuba, China hadi Tanzania ambako matajiri wakawa maadui wa taifa  na kuitwa manyang’au, yaani mafisi!
Ujamaa ukaikwamishaTanzania kiuchumi  baada ya miaka kama 12 tu  na serikali ikajitoa kimasomaso kwa kuanzisha ilichokiita “vita dhidi ya wahujumu uchumi” mwaka 1983 ambapo raia aliyekutwa na kopo la Blue Band, gunia la chumvi, shati la mtumba, na kadhalika alikamatwa!
Matokeo yake, watu wengi waliishia magerezani, wakapokonywa vitu  walivyovipata kwa shida kutokana na kuadimika nchini.  Nyerere alipoondoka madarakani, waliobaki waliitupilia mbali  siasa hiyo iliyokuwa imewajaza umaskini na majonzi ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Kwa wanaotaka umaarufu kupitia dirisha la ujamaa, waamke, wasimame na watembee, kwani dhamira njema ya serikali,  chama au mtu binafasi  kwa binadamu wenzake  — kama vile miiko ya viongozi na kadhalika — inapatikana popote, haiko katika ujamaa tu!
Hivyo, kuzungumzia ujamaa leo  – kitu kilichoshindikana duniani mbele ya wasomi na wajinga – ni kupoteza wakati!

Comments are closed.