KWA ALICHOKIFANYA MLIMANI CITY DIAMOND PESA INAONGEA

 MWANAMUZIKI grade one kwenye Muziki wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ ameendeleza jeuri zake na kuthibitisha kuwa pesa kwa upande wake si tatizo bali inaongea, Risasi Mchanganyiko linaye hatua kwa hatua.

 

TUJIUNGE MLIMANI

Usiku wa kuamkia juzi katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar, Diamond au Mondi alifanya tukio la kumwaga pesa baada ya kuandaa sherehe baab’kubwa ya kukata na shoka kwa ajili ya birthday ya mama yake, Sanura Kassim ‘Bi Sandra’ na mchumba’ke, Tanasha Donna Oketch.

 

Katika tukio hilo lililohudhuriwa na mastaa wa kada mbalimbali, kila mmoja aliondoka na lake moyoni; “Hii ya Diamond haijawahi kutokea!”

TUKIO LINGINE

Mbali na mpangilio, ulinzi wa uhakika, vyakula na vinywaji ambapo watu walikunywa hadi wakawa nyang’anyanga’ na kuserebuka hadi majogoo, Diamond alifanya tukio lingine lililoacha watu midomo wazi.

 

MAGARI YA KIFAHARI

Diamond aliwazawadia magari ya kifahari mama yake mzazi, Bi Sandra pamoja na mpenzi wake, Tanasha na kusababisha gumzo kila kona.

LAND CRUISER V8

Gari hizo aina ya Toyota Land Cruiser V8, yanaelezwa kila moja kuwa na thamani isiyopungia zaidi ya shilingi milioni 150 hivyo yote mawili kuwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni 300.

 

Magari hayo yalibandikwa namba yakisomeka majina ya ‘Mama Dangote’ ambaye ni mama yake mzazi na lile la mpenzi wake likiandikwa ‘Tanasha’. Wa kwanza kukabidhiwa gari alikuwa mama yake mzazi aliyemfungilia mlango kisha akahamia kwa Tanasha na kufanya hivyohivyo.

 

MAGARI MATATU MILIONI 400

Kufuatia Diamond kuwapa magari hayo, sasa familia hiyo inakuwa na jumla ya magari matatu ya aina hiyo likiwemo analotumia mwanamuziki huyo aina ya Toyota Land Cruiser V8. Thamani ya magari hayo matatu inatajwa kuwa zaidi ya shilingi milioni 400 kwa jumla ambapo ili angalau kupiga misele miwili-mitatu itamlazimu kuweka mafuta ya shilingi efu 50 kwa kila moja.

SIYO MARA YA KWANZA

Tukio hilo la Diamond kutoa magari kwa watu mbalimbali siyo la mara ya kwanza kwani mwaka 2014 alifanya hivyo kwa kumpa mama yake huyo gari aina ya Toyota Harrier Lexus (New Model).

 

Pia alishafanya hivyo kwa aliyekuwa mpenzi wake, Wema Isaac Sepetu aliyempa gari aina ya Nissan Murano. Alifanya hivyo pia kwa mzazi mwenzake, Hamisa Mobeto kwa kumpa gari aina ya Toyota RAV 4 (New Model).

 

WENGINE

Wengine aliowahi kuwapa magari ni pamoja na aliyewahi kuwa mpenzi wake, Penniel Mungilwa ‘Penny’, msanii kutoka lebo yake ya Wasafi Classic Baby (WCB), Rajab Abdul ‘Harmonize’, mpigapicha wake, Lukamba, marehemu Muhidin Gurumo na wengineo.

 

UTAJIRI WA DIAMOND

Miaka miwili iliyopita, Diamond alitajwa kuwa na utajiri unaofikia shilingi bilioni 8.6 unaotokana na kuuza muziki wake mtandaoni, shoo, matangazo na ubalozi wa makampuni mbalimbali jambo lililozua utata mkubwa mitandaoni na kwa wadau wa muziki.

ZARI SASA

Hata hivyo, wakati pongezi zikiendelea kwa Tanasha ambaye ana mimba ya miezi saba kupewa gari hilo, huku nyuma kuliibuka minong’ono kuwa anazidiwa kete na mzazi mwenza mwingine wa Diamond, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’.

 

Zari aliyezaa na Diamond watoto wawili, anatajwa kuwazidi wote waliowahi kuwa wapenzi wa jamaa huyo kwani yeye aliambulia nyumba wakati wao wameishia kupewa magari.

 

Zari anatajwa kujimilikisha nyumba ya Diamond aliyonunua jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini kabla ya kutengana na mwanamama huyo. Hata hivyo, baada ya kutengana, Zari alidaiwa ‘kuiteka’ nyumba hiyo na kujimilikisha.


Loading...

Toa comment