The House of Favourite Newspapers

Kwa Heri Maria na Consolatha, Huu ni Zaidi ya Msiba – Video

Maria na Consolata Mwakikuti

MUNGU ni mwema na ni wa ajabu kwa sababu matendo yake ni makuu! Ukuu wake umejidhihirisha katika muujiza wa watoto pacha waliozaliwa wakiwa wameungana kiwiliwili, Maria na Consolata Mwakikuti (22) ambao usiku wa Jumamosi iliyopita walifariki dunia na kuibua simanzi nzito!

 

NI ZAIDI YA MSIBA

Uwazi linaweza kuthibitisha bila shaka kuwa, vifo vya wapendwa hawa waliokuwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Ruaha vilivyotokea kwa kupishana dakika kumi hadi kumi na tano katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa ni zaidi ya msiba kwa namna tukio hilo lilivyopokelewa ndani na nje ya nchi.

 

Gazeti hili ambalo limekuwa likiwaripoti watoto hao katika ngazi mbalimbali tangu wakiwa wadogo, iwe kwa furaha au huzuni, lilifika hospitalini hapo muda mfupi baada ya kutokea kwa vifo hivyo vya mshtuko.

 

KAULI YA CONSOLATA

Miongoni mwa mambo yaliyoibua simanzi nzito hospitalini ni pamoja na kauli Consolata ambaye alikuwa mzima alipopaza sauti na kusema; ‘TUNAKUFA’ kisha wakakata roho hivyo kuibua huzuni kila kona hasa kupitia mitandao ya kijamii. Kwa mujibu wa madaktari wa hospitali hiyo, sababu ya vifo vya mapacha hao ni tatizo la njia ya hewa.

 

Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Museleta Nyakaloto alisema kuwa, watoto hao walipokelewa Mei 17, mwaka huu wakitokea Hospitali ya Taifa Muhimbili ambapo aliyeanza kufariki dunia ni Maria.

Kuonesha kuwa ni msiba mkubwa, Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Iringa ambako mapacha hao walipata elimu ya sekondari alisema vifo hivyo ni pigo kubwa huku Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela akisema kuwa, Serikali ilipokea kwa masikitiko vifo vya pacha hao ambapo Rais Dk John Pombe Magufuli alituma salamu za rambirambi.

 

MAMBO WALIYOSHINDWA KUYATIMIZA

Katika mahojiano na Uwazi, mara kadhaa Maria na Consolata walisisitiza juu ya ndoto au mambo manne ambayo walitamani kuyaona kwenye maisha yao.

 

MOJA

Maria na Consolata walikuwa na ndoto ya kusoma kwa kiwango cha Chuo Kikuu na kupata Digrii ya Ualimu. Walieleza namna ambavyo watoto wengine waliojaliwa viungo vyote na afya bora walivyoshindwa kusoma kwa bidii hadi ngazi za juu hivyo wao waliahidi kufanya hivyo.

Jambo hilo lilishindikana kwani pamoja na kusoma kwa juhudi kubwa, lakini wamefariki dunia wakiwa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Ruaha wakisomea Digrii ya Ualimu.

 

“Ndoto yetu ni kuwa walimu, kila mmoja wetu anasoma kwa bidii, mimi naandika kwa mkono wa kushoto na Maria anaandika kwa mkono wa kulia, tumezoea na lengo ni kutimiza ndoto yetu,” alikaririwa Consolata katika mahojiano ya mara ya mwisho na Uwazi.

Maria na Consolata walieleza namna ambavyo wangeitumia elimu yao ya ualimu kwa ajili ya kuitumikia Serikali, lakini ndoto hiyo wameondoka nayo.

 

PILI

Jambo lingine ambalo Maria na Consolata walitamani kulitimiza, lakini imeshindikana, ni kuolewa na mwanaume mmoja, lakini kwa sharti la kuwa awe mcha Mungu.

“Awe na tabia nzuri na mcha Mungu, mwanaume huyo anaweza kufikiri kuwa tutakuwa mzigo kwake, lakini hapana, tutapigana katika maisha na tutamheshimu,” alikaririwa Consolata katika mahojiano na Uwazi huku akionekana mchangamfu zaidi.

 

TATU

Maria na Consolata walikuwa na ndoto ya kupata watoto baada ya kumpata mwanaume wa kuwaoa. “Tungependa nasi tuwe na watoto,” alikaririwa Maria.

NNE

 

Jambo la nne ambalo pia walikuwa wakilisema Maria na Consolata ni juu ya kutamani kuiona Tanzania yenye maendeleo makubwa chini ya Rais Magufuli.

Pacha hao walilieleza jambo hilo siku chache baada ya Rais Magufuli kuwatembelea walipokuwa wamelazwa kwenye Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar.

“Tumemuombea (Rais Magufuli) kwa Mungu na tumeliombea taifa lifike mbali. Tunatamani kuiona Tanzania ya Viwanda,” alikaririwa Consolata mapema mwaka huu.

 

MBALI NA HAYO

Mbali na mambo hayo, pia Maria na Consolata walitamani mno kuwa waimba Injili.

Katika mahojiano ya mwisho na Uwazi, Maria alionesha umahiri wake wa kuimba na kumwambia mwandishi wetu ipo siku wangekuwa waimbaji wakubwa wa nyimbo za Injili.

 

SAFARI YAO NDEFU

Ikumbukwe kuwa pacha wengi walioungana hudumu kwa kipindi kifupi na wengine hupoteza maisha wakati madaktari wakitumia ustadi wao kuwatenganisha ila Maria na Consolata ambao ni miongoni mwa watoto 6 kwenye familia ya Mwakikuti wameishi yapata miaka 22.

Wawili hawa walikuwa wameungana kuanzia kiunoni, wanatumia miguu miwili, mikono minne, na vichwa viwili kwa maana kila mmoja na kichwa chake.

 

WALIKOZALIWA

Maria na Consolata walizaliwa mwaka 1996 katika Kijiji cha Ikonda Wilaya ya Makete mkoani Njombe. Walipata elimu yao ya msingi kijijini hapo na kufanikiwa kufaulu vizuri kabla ya mwaka 2011 kuchukuliwa na wamisionari na kupelekwa wilayani Kilolo kwa ajili ya kuwalea zaidi katika Kituo cha Nyota ya Asubuhi Kidabaga wilayani Kilolo.

Walianza kujulikana wakiwa shule ya msingi.

Wakiwa na umri wa miaka mitatu, baba yao, Alfred Mwakikuti alifariki dunia na walipofikia darasa la pili mwaka 2002, mama yao pia alifariki dunia hivyo kuwaacha yatima.

Katika maisha yao ya kusoma, kila mmoja alikuwa na madaftari yake na wakati wa kufanya mazoezi au kuandika kazi wanazopewa, mmoja huanza kuandika, akimaliza na mwingine huandika. Mungu azilaze roho zao mahali pema peponi. Amina.

STORI:MWANDISHI WETU, UWAZI

 

Usichokijua Kuhusu Maria na Consolata

Comments are closed.