The House of Favourite Newspapers

KWA HILI LA DKT. MWAKYEMBE, BONGO MOVIE MSHINDWE WENYEWE

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe

JUMANNE wiki hii baada ya Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe kutembelea ofisi za Global Publishers na kupata nafasi ya kuulizwa maswali, nilimuuliza juu ya jitihada ambazo serikali inazifanya kuhakikisha inanusuru Tasnia ya Filamu za Kibongo ‘Bongo Movie’. 

 

Majibu aliyonipa ni kama alikuwa anapeleka ujumbe kwenye tasnia hiyo kwamba wizara yake imekwisha inusuru tayari na imesafisha njia, kwa hiyo kazi ni kwa wasanii tu kuhakikisha wanatimiza wajibu wao na mambo yatakuwa sawa.

 

Ninakubaliana na Dkt. Mwakyembe kutokana na majibu aliyonipa pamoja na uchunguzi niliofanya. Hapa nitachambua maeneo aliyoyazungumzia kwamba wizara yake imeyafanyia kazi na kuwasafishia njia Bongo Muvie.

MIKATABA

Dkt. Mwakyembe alianza kueleza kwamba ili kuhakikisha wanainusuru tasnia hii, wizara iliangalia namna ya kusimamia masilahi ya wasanii. Kwanza, ilianza kutoa elimu juu ya mikataba. Wakawaonyesha pia wasanii mifano ya mikataba bora ambayo wanatakiwa wasainishwe na watu wanaofanya nao kazi.

 

Zaidi ya hilo Dkt. Mwakyembe akaunda kamati ya watu tisa, watano wakiwemo wanasheria, mmoja akiwa ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa (Basata), Godfrey Mngereza pamoja na yeye mwenyewe. Kazi ya kamati hii ni kupitia mikataba ambayo wasanii walisaini huko nyuma na kama kuna mazingira yoyote ya unyonywaji basi wizara inamsaidia msanii hadi anapata haki zake.

 

Mpaka sasa akasema wamepata mikataba 19, tisa ikiwa ya marehemu King Majuto, sita ya marehemu Steven Kanumba, mingine ya mwanadada Wastara Juma. Lakini pia mpaka sasa wamewasaidia waigizaji kadhaa kupata stahiki zao akiwemo Vicent Kigosi ‘Ray’ aliyekuwa na shida na bodi ya filamu, alilipwa milioni 32 kupitia kampuni yake ya RJ.

Kwa hiyo unaweza kuona kwamba kwa upande wa mikataba, kile kilio cha wasanii cha muda mrefu kuhusu kunyonywa kimesikika kwa serikali. Kwa hiyo kazi ni kwao, kupata elimu juu ya mikataba bora ambayo wanashauriwa na serikali na kuachana na tabia ya kuendekeza njaa kwa kusaini mikataba mibovu ili tu iwavushe kwenye njaa ya siku moja.

 

UZALISHAJI WA FILAMU

Kuhusu uzalishaji wa filamu, Tanzania hatuko vibaya. Tunazalisha filamu takriban 1400 kwa mwaka; kwa mujibu wa Bodi ya Filamu. Sisi ndiyo nchi ya pili Afrika kwa uzalishaji wa filamu. Tupo nyuma ya Nigeria (Nollywood) ambao wanazalisha filamu takriban 50 kwa wiki, sawa na filamu 2400  kwa mwaka, Nigeria inaifuatia India (Bollywood) kisha Marekani (Hollywood).

 

Kwa hiyo hatupo vibaya kwenye uzalishaji. Tatizo linalokuja ni kwamba ingawa uzalishaji wetu ni mkubwa lakini filamu zetu nyingi hazina ubora wa kimataifa. Wanachotakiwa kufanya wasanii kwa sasa ni kujipanga kwenye suala zima la mtaji na kuhakikisha wanazalisha filamu bora ambazo zinaweza kufika mbali na kufanya vizuri zaidi kimataifa, huo ni ushauri alioutoa pia Dkt. Mwakyembe.

USHAURI KUHUSU SOKO

Ukizungumzia wasanii kufanya filamu za kimataifa hoja yao kubwa mbali na mtaji ni soko. Kwamba soko la filamu limeporomoka kiasi kwamba unaweza kutengeneza filamu kwa gharama kubwa na ukakosa soko.

 

Ushauri wa Dkt. Mwakyembe ulikuwa ni mzuri sana. Kwanza wasanii kuwa na msimamo pale wanapokwenda sokoni na kuacha kujirahisisha kwa sababu kwa kufanya hivyo wanakuwa wanaliharibu soko lao wenyewe. Lakini pia wanatakiwa kuendana na mabadiliko ya teknolojia. Hawawezi kushindana na ukweli kwamba kwa sasa soko la filamu kwa upande wa CD na DVD limeporomoka.

Kwa hiyo wanatakiwa kuangalia njia mbadala. Mfano Televisheni nyingi sikuhizi zinanunua muvi na tamthiliya. Lakini pia wanaweza kuuza kupitia mitandaoni na kwenye uzinduzi mfano kwenye majumba ya sinema. Ni ushauri mzuri wa kufanyia kazi.

 

SAPOTI KUTOKA KWA SERIKALI

Pamoja na wizara yake kufanya hayo yote niliyokueleza mwanzo bado Dkt. Mwakyembe aliweka wazi kwamba serikali haiwezi kuwaacha hivyohivyo wasanii. Pale msanii anapokuwa na kazi yake nzuri na njaa inamkumba anaweza kuonana na Bodi ya Filamu ikaona namna ya kusaidia wakati anatafuta soko. Bila shaka kwa mambo haya, wizara chini ya Dkt. Mwakyembe inasimama kama baba, mama na mlezi wa kweli wa Tasnia ya Filamu.

 

Imetengeneza barabara mlimani. Yani mahali ambapo palionekana ni pagumu kupitika imefanya pawe rahisi, kazi kwenu Bongo Movie, mshindwe wenyewe kwa sababu mna kila mnachohitaji kwa sasa ili kusimama na kwenda mbele zaidi kwenye tasnia yenu.

MAKALA: Boniphace Ngumije

Comments are closed.