The House of Favourite Newspapers

KWA HILI LA EMMA THE BOY, WASANII WA BONGO FLEVA NIMEWAPAKA MATOPE!

0

`Nilishangazwa sana na ukimya wa wasanii wa Bongo fleva juu ya sakata la kupotea kwa Prodyuza wa THT, Emma The Boy, ambaye alipotea kwa takribani siku tano ila kwa sasa ameshapatikana, lakini cha ajabu wasanii wa Bongo fleva walikaa kimya, kama vile hawajui au haiwahusu, jambo hili linaonyesha wazi ndani ya tasnia yenu kuna ubaguzi.

Maswali ninayojiuliza hadi sasa ni kwanini alivyotekwa Roma mlihangaika usiku na mchana? Mkapaza sauti zenu kupitia mitandao yenu ya kijamii na mkashinda vituo vya polisi na mahospitalini?  Mkaitisha mkutano wa kujadiliana juu ya nini cha kufanya?, kwa takribani siku mbili hakukuwa na stori nyingine zaidi ya huzuni tu.

Na kwa kiasi kikubwa juhudi zenu zilizaa matunda na hatimaye Roma na wenzake wakapatikana, ndiyo maana kwa kulitambua hilo kupitia ngoma yake za Zimbabwe akawashukuru wale wote waliopaza sauti zao.

Lakini juhudi hizo mlishindwa kuzionyesha kwenye tukio la Emma The Boy, ambalo linafanana na lile la Roma,  siyo mitandaoni, wala kikao cha kujadili mtampata wapi, ndiyo kwanza mpo bize na mambo yenu, kwani yeye na Roma wana tofauti gani?, ni kwamba taarifa hamkuzisikia au haikuwagusa ndiyo maana mliwasusia wasanii wa THT tu, wakiwemo Ditto, Amini na Barnaba ndiyo wahangaike peke yao?, basi hata kinafiki tu kuonyesha kwamba aliyepotea naye ni muhimu kwenye tasnia hii ya muziki pia mlishindwa!

Yaani kwa hili bila woga nawaita wabaguzi, hamna umoja wowote ni unafiki mtupu, tena nawakumbusha kwamba kuna kesho ambayo ni fumbo, wekeni utu mbele siyo lazima hadi tukio limtokee msanii mkubwa au mtu maarufu sana ndiyo mjue kujali na kulichukulia uzito, lakini la Emma mlilichunia kama viziwi vile.

Siku zote umoja ni nguvu utengano ni udhaifu, zile nguvu zenye uzito unaofanana na Panton, mlizozitumia kumlilia Roma hadi akapatikana, mlitakiwa kuzitumia tena kwa Emma The Boy.

NA ISRI MOHAMED/GPL

 

 

 

 

 

 

 

 

Leave A Reply