The House of Favourite Newspapers

Kwa hili la wanao, Q Chillah kwa nini ujishtukie?

0

q-chillah

Mwanamuziki Q Chief.

HII haitakuwa mara ya kwanza na wala sidhani kama itakuwa ya mwisho, kumzungumzia mmoja kati ya wasanii wa Muziki wa Kizazi Kipya wenye uwezo mkubwa wa kuimba na ambao wamethibitisha hivyo tangu kazi yao ya kwanza tu iliyowatambulisha kimuziki.

Unapomzungumzia Aboubakar Katwila maarufu kama Q Chief unasema kuhusu mtu ambaye tangu alipofanya ngoma yake ya kwanza, Si Ulinikataa, ameendelea kubakia juu, licha ya juhudi kubwa, tena zake mwenyewe kujipoteza kushindwa.

Katika muziki, hasa huu wa kizazi kipya, kuna watu wanafungiwa milango ili wasichomoze, kazi zao hazichezwi redioni, video hazionekani, hawapewi kolabo na baadhi ya maprodyuza wanakataa kufanya nao kazi na mbaya zaidi, hawapati fursa ya kutumbuiza katika matamasha yenye akili.

Kwa wasanii wa Bongo ambao wengi mipango ya kazi zao haieleweki, wakifikia hatua ya kufanyiwa hivi, wamekwisha. Mifano ya wasanii waliopitia hatua hii ipo mingi na wenyewe wanajijua.

Lakini baadhi yao, unasikitishwa wenyewe wanapokuwa vinara wa kujikwamisha, halafu kwa masikitiko makubwa, wanaamini wanafanyiwa mtimanyongo. Mmoja wa wasanii wa sampuli hii ni Q Chief ingawa yeye anapenda zaidi kama ataitwa Q Chillah.

Sijui ilivyotokea, lakini mkali huyu wa kibao cha For You, aliingia katika kundi la wasiojitambua, baada ya kuamua kutumia madawa ya kulevya. Wakati f’lani, alijitokeza na kusema alilazimika ‘kula sembe’ baada ya kufanyiwa vitendo vya hujuma katika muziki wake.

Ingawa kama nilivyosema pale mwanzo kuwa wapo watu wanaoweza fitina za kuwabania wasanii hadi wakakata tamaa, bado utetezi wake huo ni dhaifu, tena usioweza kukidhi viwango mbele ya watu wenye akili zao.

Katika wakati mgumu unaokabiliwa na mapambano dhidi ya mtu anayehujumu kazi zako, ni wazi unatakiwa kuweka ‘concentration’ ya hali ya juu kwa kila hatua unayochukua ili kumfanya asipate nafasi ya kurahisisha hujuma zake.

Sasa kama Q Chillah anafahamu yupo katika mapambano ni vipi aliamua kujilipua kwa staili ya kula unga? Kwa nini nimesema hivi leo, muda mrefu kidogo tangu yeye mwenyewe ajitokeze na kukiri kutumia unga na hapohapo kudai kuwa amejirekebisha na anajutia kosa lake?

Ni kwa sababu ya kauli yake ya hivi karibuni wakati alipokiambia kituo kimoja cha redio kuwa, muziki wake utapata thamani zaidi baada ya yeye kuondoka duniani. Akasema muziki anaoufanya utaishi muda mrefu zaidi kutokana na ubora wa mashairi yake na watoto wake wataishi vizuri kwa kutegemea kazi zake.

Ingawa kuna ukweli juu ya kauli hiyo, lakini kwa wanaomfuatilia msanii huyu, wanatambua kuwa ni maneno ya kukata tamaa. Tafsiri nyingine ya kauli yake ni kuwa watu hawaoni thamani ya muziki wake kwa sasa na haumsaidii yeye wala watoto wake kuishi vizuri.

Mimi nadhani Q Chillah anajishtukia. Anadhani vitendo vyake nje ya jukwaa vimempotezea thamani anayostahili kiasi kwamba kwa sasa, vijana wake hawawezi kufaidi matunda ya kazi zake hadi hapo baadaye!

Wasanii wengi wa Bongo wanasumbuliwa na ujana, wanapopata umaarufu wanasahau kwamba kuna maisha nje ya jukwaa na wanapokuja kubaini ukweli huu, nyakati zinakuwa zimewaacha kutokana na vitendo vyao.

Ningemshauri Q Chillah kuendelea kupambana kwa sababu muda bado upo na uwezo anao badala ya kutoa kauli za kujipa moyo.

Ana uhakika gani watoto wataishi vizuri kwa muziki wake wakati hakuna mipango aliyoitengeneza ya kuwafanya wanufaike? Ni kwa kiasi gani ameshiriki katika kupigania sheria za hatimiliki?

Leave A Reply