The House of Favourite Newspapers

KWA HILI MAMA WEMA ANAJIPA PRESHA ZA BURE!

LENGO la makala haya ni kueleza jinsi mama wa staa mkubwa Bongo, Wema Sepetu, Miriam Sepetu anavyojitafutia presha za bure katika kumchunga mwanaye lakini kabla ya kwenda huko, niwape kisa kimoja ambacho kilinitokea nikiwa nasoma shule ya msingi. 

 

Wakati mimi nikiwa darasa la tatu, kuna kijana mmoja nakumbuka alikuwa akiitwa Masharubu, yeye alikuwa darasa la saba. Alinizidi kiumri lakini alikuwa rafiki yangu sana. Kijana huyu alikuwa mtukutu ile mbaya.

 

Alijulikana kwa kuwa na sifa mbaya shule nzima, walimu wamemchapa weee lakini hakubadilika, ndiyo kwanza alizidisha utukutu. Sikujua urafiki wetu ulikujakujaje lakini Masharubu alikuwa rafiki yangu. Kila alipokua yeye na mimi nilikuwepo. Yeye ndiye aliyenifundisha kutoroka shule, kwenda kuiba miwa na maembe kwenye mashamba ya watu, kuvuta sigara, ugomvi na kila aina ya tabia mbaya.

Cha ajabu sasa, siku moja nikiwa nyumbani jioni nilimuona mama wa Masharubu akifika nyumbani kwetu akiwa amefura. Hii ilikuwa ni baada ya mama Masharubu kupewa maneno kuwa mimi ndiye niliyemharibu mtoto wao.

 

Mama huyu akayachukua yale maneno bila kunijua mimi nikoje, akaja kunishitaki kwa wazazi wangu kwamba eti mimi ndiye niliyemharibu mtoto wao na kwamba iwe ni mwanzo na mwisho kuonekana nikiwa na Masharubu.

 

Wazazi wangu walipigwa butwaa kwani walishindwa kuelewa mimi na umri wangu mdogo vile na kiumbo changu kama ‘piritoni’ ningewezaje kumfundisha tabia mbaya Masharubu ambaye alikuwa kanizidi kiumri, kidarasa na hata kimwili?

 

Nakumbuka baba alinyanyua mdomo wake na kusema: ‘Hata sisi tulitaka kuja kwenu maana mtoto wenu ndiye aliyemharibu mtoto wetu, kamfundisha kuvuta sigara, wizi na kila aina ya tabia chafu.’

 

Nilipoitwa na mama wa Masharubu kuniona, mwenyewe alistaajabu, hakujukua kwamba Amran mwenyewe alikuwa akiburuzwa tu na Masharubu. Wazazi hao wakakubaliana kutunyoosha kwa pamoja lakini ikabainika kuwa, aliyekuwa kinara wa tabia mbaya alikuwa Masharubu.

Kisa hiki kinaenda sambamba sana na mazingira yaliyopo kati ya Wema na mama yake. Kuna msemo wa Kiswahili usemao, mtoto kwa mama hakui. Ni msemo maarufu sana na wazazi wengi wamekuwa wakiutumia wakimaanisha kwamba, hata uwe mkubwa kiasi gani, bado wazazi wako wana nafasi ya kukuongoza kama mtoto wao.

 

Mimi sina shida kabisa na msemo huo lakini kuna wakati nauona kama unatumika ndivyo sivyo. Nasema hivyo kwa sababu msemo huo ndiyo ambao unamfanya mama Wema hadi leo anamchunga binti yake hata katika yale ambayo hastahili kuchungwa nayo.

 

Hivi karibuni ulitokea mtiti kati ya mama Wema na binti ambaye ni msanii wa filamu Bongo, Diana Kimari. Kwa wasiomjua vizuri binti huyu ni yule ambaye alikuwa akiitwa Pacha wa Lulu. Alikuwa rafiki mkubwa wa msanii wa filamu Elizabeth Michael ‘Lulu’ na katika kuigiza wakati mwingine walikuwa wakipewa ‘scene’ zinazoendana.

 

Kiumri Diana ni mdogo sana kwa Wema, kwa maana nyingine ni kwamba Wema ni dada wa Diana. Cha ajabu sasa, mama Wema hivi karibuni alifungukia tukio la kumpa kipigo Diana kisa kikiwa ni kuwa karibu na mwanaye.

 

Hii si mara ya kwanza kwa mama Wema kuwawashia moto marafiki wa mwanaye. Amekuwa akifanya hivyo kwa wasichana wengi ambao wamekuwa wakijisogeza kwa Wema mwenyewe akidai kuwa, ndiyo ambao wanamfanya aingie kwenye majanga.

 

Nakubaliana kabisa na ukweli kwamba, marafiki siku zote ndiyo ambao wanaweza kukutengeneza ama kukuharibu, kwa maana ya kwamba ukiwa na marafiki wabaya, basi na wewe utakuwa mbaya, na kinyume chake pia. Lakini nakaa na kujiuliza kwamba, hivi inawezekana kweli Wema akashikiwa akili zake na Diana?

 

Najiuliza tu maana wapo wanaoweza kusema hata mdogo anaweza kumfundisha mkubwa tabia mbaya lakini sioni nguvu ya Diana kumuingiza Wema kwenye majanga, badala yake nilitarajia kuwaona wazazi wa Diana wakiibuka na kulalamika kuwa Wema anamharibu mtoto wao.

 

Matokeo yake sasa tunamuona mama Wema anapata presha akiamini kwamba Wema ataharibiwa na Diana na hivyo inabidi atumie nguvu kubwa kuwatenganisha ikiwa ni pamoja na kutoa kichapo. Mimi naona mama Wema anatumia muda na nguvu zake vibaya.

 

Hata kama mtoto kwa mama hakui lakini kwa aliyopitia Wema ilitosha kabisa kuamua kutulia na kutokuwa tayari kuyumbishwa na marafiki. Mtakumbuka tangu Wema awe staa amekuwa na marafiki wengi sana na kila alikuwa na nia ya kumharibu.

 

Hapo ndipo ambapo tumeona mama Wema kila wakati anatibuana na marafiki wa Wema. Huku ni kujipa tu presha za bure. Ifike wakati mama Wema achukulie kwamba mwanaye amekua, hastahili kuchaguliwa marafiki. Yeye sasa hivi ni mtu mzima, anajua ni rafiki yupi anamfaa na yupi ambaye anaweza kumuingiza kwenye majanga. Aamue mwenyewe sasa maana hatma ya maisha yake iko mikononi mwake.

 

Haya matukio ya mama Wema kila mara kuwavurumusha marafiki wa mwanaye yametuchosha. Yaani kweli mama aache yote aanze kudili na nani anafaa kuwa rafiki wa mwanaye nani hafai! Huko ni kujipotezea muda tu na kama ataendelea basi ajue mwanaye huyu atamuua kwa presha.

 

Nihitimishe makala haya kwa kusema tu kwamba, Wema amekuwa mtu mzima, amepitia mapito mengi yaliyosababishwa na marafiki zake, inatosha kuwa fundisho kwake. Achague watu ambao wakimzunguka hawezi kujikuta matatizoni. Hilo litamfanya kwanza apate heshima anayostahili lakini pia itampa amani mama yake ambaye inaonekana bado anasimamia ule msemo wa kwamba mtoto kwa mama yake hakui.

MAKALA: AMRAN KAIMA

Comments are closed.