Kwa Kilichoonekana Mapinduzi, Simba, Yanga Zijipange CAF

Wachezaji wa timu ya Yanga wakiendelea na mazoezi.

MSIMU mpya wa michuano ya kimataifa Barani Afrika unaanza mwezi ujao. Simba inashiriki kombe la Shirikisho wakianza dhidi ya Gendemarie FC ya Djibout ya Djibout.

 

Yanga wao wako kwenye Ligi ya Mabingwa ambapo wataanza na St.Louis ya Djibout mechi zote zikianzia wikiendi ya Februari 9 na 10 jijini Dar es Salaam.

 

Maoni yetu ni kwamba kwa kilichotokea kwenye Kombe la Mapinduzi wawakilishi hao wa Bara wanahitaji kujipanga. Simba na Yanga hazikuonyesha kiwango kizuri kwenye michuano hiyo ambayo ilishirikisha timu pinzani kutoka kwenye ligi tofauti ambazo katika hali ya kawaida ilikuwa ndiyo kipimo cha kuonyesha kuwa wanaweza angalau kufanya kitu kimataifa lakini matokeo yake wamechemka.

Kikosi cha timu ya Simba.

Michuano hiyo imefunua aina ya ubora wa wachezaji na udhaifu uliopo

ambao kama wanataka kufanya vizuri wana kitu cha kujifunza. Simba na Yanga zimeshindwa kucheza fainali ya michuano hiyo na hata matokeo waliyokuwa wakiyapata tangu kwenye hatua ya makundi yalikuwa hayaendani na mbwembwe zao za nje ya uwanja.

 

Michuano wanayojiandaa kushiriki ya Mabingwa na Shirikisho, ina heshima kubwa Afrika, hivyo kwa hadhi ya Simba na Yanga ni wakati muafaka wa kujipanga kisaikolojia kutokana na dosari walizoziona kwenye Mapinduzi.

 

Viongozi na makocha wakae chini wapange mikakati mipya ambayo itawasaidia kuingia kwenye mashindano hayo wakiwa vizuri kuliko kusubiri mpaka dakika ya mwisho ndiyo wanaanza kufanya zima moto.

 

Viongozi wanapaswa kuwa na bajeti ya kutosha na hiyo inapatikana kupitia mipango mikakati ambayo inaweza kutengenezwa kwa umakini na kupelekwa kwa wadhamini ambao ndiyo wawezeshaji.

 

Timu ikiwa inafanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa ndiyo njia rahisi ya kupata fedha na kujijenga vizuri.

Huu ndiyo wakati wa kuanza kuwajua wapinzani wenu ndani na nje ya uwanja. Wanatakiwa ubora na udhaifu wa timu hizo kwavile mambo mengi sikuhizi yanakwenda kisasa ukitaka kuelewa maelezo ya kitu fulani ni muda mfupi tu.

 

Kwa vile miundombinu imekuwa rahisi tofauti na miaka ya nyuma. Mwanzo mzuri kwenye mechi za awali kutapandisha na motisha zaidi kwa wachezaji na mashabiki kufanya vizuri na ni vizuri ukawepo mkakati wa mchezo mmoja baada ya mwingine. Ndio mbinu inayoweza kuwapa wepesi.

 

Maoni yetu ni kwamba Simba na Yanga zijipange vizuri kwenye mashindano ya msimu huu ili kuonyesha kweli kwamba wao ndiyo wakubwa wa soka la Bara.

 

Macho ya wengi msimu huu yatakuwa kwenye michuano hiyo kutaka kujionea ushindani wa kweli baina ya timu hizo kutokana na historia za utani wao, hivyo ingependeza zaidi kama wangeingia kwa umakini stahiki na wawape heshima pia mashabiki na wafuasi wao.


Loading...

Toa comment