The House of Favourite Newspapers

Kwa Kosi Hili…. Mmekwishaaa!

0

KAMA utakwenda kwa Mkapa leo ukiwa na matokeo yako mfukoni, basi jiandae kurudi nyumbani unalia, kwani lolote linaweza kutokea.

 

Yanga itakuwa mwenyeji wa Simba kesho Jumamosi katika mchezo unaosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini, utakaochezwa kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.

 

Kila timu imejiandaa vya kutosha na mashabiki wa kila upande unawatambia wenzao kwa kuwaambia “mmekwishaa” kutokana na namna kila kikosi kilivyojipanga. Ndiyo maana unatakiwa uende ukitarajia lolote lakini ukienda na matokeo yako mfukoni, basi ujiandae kulia.

 

Kimsingi, mechi hiyo ya watani, ina pointi tatu kama mechi nyingine tu, lakini ni mechi kubwa zaidi Afrika Mashariki na Kati, kwa kuwa wanakutana watani wa jadi na kwa kawaida wanaofungwa huwa hawabaki salama.

 

Mechi hiyo itakayoanza saa 11:00 jioni, tayari imeshaibua presha kubwa kwa mashabiki na viongozi wa pande zote mbili.

 

Lakini kocha wa Simba, Sven Vandebroeck, yeye amesema wala hana presha yoyote na Yanga ambayo katika mchezo wake wa mwisho dhidi ya Yanga alishinda 4-1 katika nusu fainali ya Kombe la Shirikisho, maarufu kama FA. Hata hivyo, mchezo wa mwisho baina ya timu hizo kwenye ligi, Yanga ilishinda 1-0.

 

Lakini Sven, raia wa Ubelgiji, amelihakikishia Championi Ijumaa, kuwa hana presha na Yanga hata kidogo.

“Nafikiri timu kubwa muda mwingine zinahitaji presha kwani inasaidia kupata matokeo mazuri na inasaidia sana.

 

“Lakini kwenye mechi hii hatuna presha kwa sababu tumezoea na tushacheza mechi za namna hii nyingi, nafikiria tutafanya vizuri kwa sababu tumeweka mpango wa kutopoteza pointi kwa kipindi hiki,” alimaliza Mbelgiji huyo.

 

Kwa upande wake Kocha Mkuu wa Yanga, Mrundi, Cedric Kaze, amesema ataingia uwanjani kuwavaa Simba kivingine, tofauti na alivyocheza michezo minne iliyopita ya Ligi Kuu Bara.

 

Kocha huyo aliwashangaza wengi kwa kuwaacha nje mastaa wake muhimu katika sare dhidi ya Gwambina juzi Jumanne, ikielezwa kuwa anawatunza mastaa hao kwa ajili ya kuikabili Simba.

 

Mrundi huyo tangu ametua kukinoa kikosi hicho, amefanikiwa kushinda michezo mitatu kati ya hiyo minne huku mmoja akitoa suluhu dhidi ya Gwambina FC ya Misungwi, Mwanza.

 

Akicheza michezo hiyo minne, kocha huyo ameonekana akibadili mifumo miwili ya uchezaji ambayo ni 4-5-1 na 4-4-2, sambamba na kubadili kikosi cha kwanza katika kila mchezo wa ligi.

 

Akizungumza na Championi Ijumaa, Kaze alisema kuwa katika mchezo huo ameandaa sapraizi ya kutosha ya kupata matokeo mazuri.

 

Kaze alisema kuwa sapraizi hiyo ni siri ambayo ataifanya katika mchezo huo, kikubwa anaendelea kukiimarisha kikosi chake kwa kuwaongezea mbinu za kiufundi zitakazowapa furaha mashabiki wa timu hiyo.

 

“Nitaingia uwanjani kwa kuwaheshimu wapinzani wetu Simba, lakini kikubwa maandalizi yamekamilika kwa asilimia kubwa, kikubwa niwaondoe hofu mashabiki wa Yanga kwa kuwaambia wasiogope na badala yake waje uwanjani kuwasapoti wachezaji wangu.

 

“Naahidi kucheza soka safi la ushindani litakalotupa matokeo mazuri ya ushindi, kikubwa nimeandaa sapraizi kubwa katika mchezo huu ambao ni lazima tupate matokeo mazuri ili tutimize malengo yetu ya kukaa kileleni kwenye msimamo wa ligi.

 

“Hatuoni sababu ya kushindwa kucheza soka safi la kuvutia, kwani uwanja tutakaoutumia ni mzuri ambao unaturuhusu kucheza soka lile lililozoeleka la pasi nyingi wakati tukiwa na mpira tukilishambulia goli la wapinzani wetu,” alisema Kaze.

 

Yanga ndiyo timu pekee mpaka sasa kwenye ligi ambayo haijapoteza mchezo wowote, rekodi ambayo inaibeba kuelekea kwenye mchezo huo dhidi ya Simba ambayo tayari imeshapoteza michezo miwili.

 

Hadi sasa Yanga imedondosha pointi nne tu dhidi ya Prisons (sare ya 1-1) na dhidi ya Gwambina (suluhu), wakati Simba imeshadondosha pointi nane (sare ya 1-1 dhidi ya Mtibwa) na vipigo mfululizo, bao 1-0 dhidi ya Prisons na JKT Tanzania, mtawalia.

 

Mbali na hilo, Yanga ndiyo timu yenye ukuta wa chuma, mgumu zaidi, ukiwa unaongozwa na Mghana Lamine Moro na Mtanzania Bakari Mwamnyeto, ambao hadi sasa wameruhusu nyavu zao kutikiswa mara mbili tu, wakati wapinzani wao Simba wakiruhusu mabao manne.

 

Lakini Simba ndiyo timu yenye safu imara zaidi ya ushambuliaji, ikiwa inaongoza kwa ufungaji, ikifunga mabao 21 hadi sasa, wakati Yanga imefunga mabao 11 tu, hivyo unaweza kusema ni vita ya ulinzi na ushambuliaji.

 

Katika michezo mitano ya mwisho, Yanga kashinda michezo minne na kutoka sare moja, waliwafunga Coastal Union bao 3-0 kwenye dimba la Mkapa, wakawafunga Polisi Tanzania 1-0 pale Uhuru, kisha wakaenda Mwanza CCM Kirumba wakawafunga KMC 2-1, wakawafunga Biashara United 1-0 na kutoka suluhu na Gwambina. Wakati katika michezo mitano ya Simba, wamechapwa mechi mbili na kushinda michezo mitatu.

 

Walifungwa 1-0 na Prisons kwenye dimba la Nelson Mandela kule Sumbawanga, wakarudi Uwanja wa Uhuru, Dar, wakafungwa 1-0 na Ruvu Shooting, halafu wakawachapa Mwadui 5-0, Kagera wakawachapa 2-0, mechi zote zikichezwa Uhuru, huku mwingine wakishinda 4-0 mbele ya JKT Tanzania kwenye Dimba la Jamhuri, Dodoma.

Said Ally na Wilbert Molandi

Leave A Reply