The House of Favourite Newspapers

Sugu, Profesa Jay Wampigia Saluti Diamond

0

sugu na faiza (2)Joseph Mbilinyi (Sugu)

Makala; Ojuku Abraham

DIAMOND Platnumz atakuwa mmoja wa wasanii watatu wanaofanya muziki barani Afrika, ambao watapanda katika jukwaa la ukumbi maarufu wa Barclays Centre, jijini New York nchini Marekani, Julai 22, mwaka huu wenye uwezo wa kuingiza watu 20,000 katika tamasha lililopewa jina la One Africa.

Wengine watakaoungana naye ni Wizkid na Flavour kutoka Nigeria, ambao kwa pamoja watakuwa wasanii wa kwanza wanaofanyia muziki barani Afrika kuwahi kutumbuiza kwenye ukumbi huo uliozinduliwa mwaka 2012 kwa shoo kubwa ya rapa Jay Z.

IMG_0599profJoseph Haule (Profesa Jay)

Maana yake ni kuwa Diamond atakanyaga jukwaa ambalo mastaa kama Rihanna, Justin Bieber, Bayonce na wengine wamefanya na hivyo kujiwekea historia ya kuwa msanii wa kwanza Bongo kufanya hivyo, kwani mara nyingi Wabongo wamekuwa wakifanya shoo Ulaya na Marekani katika kumbi ndogondogo na wakati mwingine hata uani kwa mtu.

Wabunge wawili vijana wanaoheshimika na jamii ya Bongo Fleva, Joseph Mbilinyi (Sugu) na Joseph Haule (Profesa Jay) ambao ni wakali wa Hip Hop wa muda wote Tanzania, wamekiri kuwa ilikuwa ni kilio chao siku zote, kutaka wasanii wafikie hatua iliyofikiwa na Diamond.

“Ninaufahamu huo ukumbi ni mkubwa sana kwa kweli, kumuona mtu kama Diamond anakwenda kufanya shoo pale ni jambo la kufurahisha sana. Kwa maoni yangu, muziki wa Bongo unakwenda kubatizwa rasmi pale, kwamba sasa tunaingia katika ramani halisi ya dunia kimuziki,” anasema Profesa Jay.

DIAMOND (4)

Diamond

Alisema anafurahishwa sana na jitihada binafsi zinazofanywa na Diamond kiasi kwamba sasa amekuwa msanii mkubwa Afrika, jambo linalomtia moyo, hasa akikumbuka siku kijana huyo kutoka Tandale alipomwaga machozi mbele yake.

“Nilipomuuliza analia nini, aliniambia hakuwahi kuwaza maishani mwake kama kuna siku anaweza kufanya wimbo na Profesa Jay, hakuwahi kuamini kama anaweza kufikia levo zangu, jambo hili lilinigusa sana na najua mimi ni mmoja wa wasanii waliom-inspire kuupenda na kuufanya muziki,” alisema mkongwe huyo aliyemshirikisha Diamond katika kibao chake cha Kipi Sijasikia.

Jay alisema Diamond anawa-inspire vijana wengi kutokana na juhudi zake na mafanikio anayoyapata ni ishara kwamba ukiwa na nia na kitu utafanikiwa kama utajibidisha.

“Ni jambo jema kabisa kwamba Diamond sasa anatubeba wasanii wote, lazima tumpongeze maana anakoelekea, ndiko tulikokuwa tukipigania miaka yote.”

Kwa upande wake, Sugu alisema siku zote alikuwa katika harakati za kutaka msanii wa nchi hii aheshimike, hatua ambayo Diamond amefikia.

“Natambua uwezo wake na jitihada zake, mimi sizungumzii tu muziki, bali biashara ya muziki, tunataka tuwe na ma-CEO wasanii, watu ambao tunaweza kutengeneza ajira kupitia muziki. Katika hotuba yangu kama Waziri Kivuli wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, nimeitaka serikali kutoa mwongozo kwa redio na televisheni nchini, kupiga asilimia 80 ya muziki wa nyumbani na unaobaki ndiyo uwe wa nje.

“Maana huwezi kufahamika kimataifa bila kwanza kufahamika nyumbani, tunataka hivi kwa sababu tunahitaji kuwa na akina Diamond wengi, akina Samatta (Mbwana, mwanasoka) wengi, kwa hiyo ni lazima serikali itoe fursa hizi, siyo mtu anajibidisha mwenyewe, akipata mafanikio mtu wa serikali anajitokeza kumpongeza kana kwamba walijihusisha naye.

“Diamond anafanya vizuri sana na kwa kweli tunajivunia, tunataka tuwe kama wenzetu Nigeria, kule kuna akina P Square, Davido, 2Face Idibia na wengine wengi wanafahamika kimataifa, au DRC wapo akina Koffi Olomide, Fally Ipupa, Feregora, Werasson na wengine na sisi tunatakiwa tuwe na kina Diamond, Ali Kiba, AY, yaani tuwe nao wengi,” anasema Sugu.

Barclays Center ni ukumbi unaotumika kwa shughuli mbalimbali na upo Brooklyn, New York City. Pia hutumika kama uwanja wa nyumbani wa timu ya kikapu ya Brooklyn Nets pamoja na New York Islanders ya National Hockey League.

KUNUNUA NA KUSOMA MAGAZETI YA GLOBAL PUBLISHERS ONLINE, INGIA HAPA==>VODACOM M-PAPER APP

*********

JIUNGE NA SOCIAL MEDIA ZETU

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA

INSTAGRAM: @Globalpublishers

ERIC SHIGONGO INSTAGRAM: @ericshigongo

TWITTER: @GlobalHabari

FACEBOOK: @GlobalPublishers

SUBSCRIBE YOU TUBE: Global TV Online

GLOBAL TV ONLINE: www.globaltvtz.com

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, ERIC SHIGONGO FACEBOOK PAGE:@shigongotz

Leave A Reply