KWA MARA YA KWANZA, MONDI AMLIPUA VIBAYA ZARI!

DAR ES SALAAM: BAADA ya kimya kirefu tangu wamwagane, msanii wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ ameibuka hadharani na kumchana mzazi mwenziye, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ kwa kuweka bayana kuwa anajutia kuwa naye.

 

HUYU HAPA DIAMOND

Akizungumza katika mahojiano aliyofanya kupitia mtandao mmoja maarufu wa nchini Kenya hivi karibuni, Diamond aliweka wazi kuwa moja kati ya makosa aliyowahi kuyafanya maishani ni kutoka na Zari aliyemzidi umri. “Wakati mwingine tunafanya maamuzi lakini nimejifunza kupitia makosa niliyoyafanya na ninamshukuru Mungu kwa hilo,” alisema.

 

NI KOSA KUBWA…

“Kutembea na mtu ambaye amekuzidi umri ilikuwa ni kosa kubwa sana na siwezi kurudia kosa hilo, nilifanya makosa sana kutembea na mtu ambaye ana miaka karibu arobaini,” alisema Diamond bila kumtaja jina lakini kiuhalisa inafahamika mwanamke pekee aliyewahi kuwa naye kwenye uhusiano mwenye umri huo ni Zari.

UMRI WA ZARI UTATA

Mitandao mbalimbali imekuwa ikiripoti kuwa Zari ana miaka 40 lakini mwenyewe (Zari) amewahi kukaririwa kwenye mahojiano ya runinga moja ya mitandaoni akisema ana umri wa miaka 38.

 

WATU WAMSHANGAA

Baada ya Diamond kufunguka maneno hayo mazito kwa mama watoto wake huyo, watu wengi wa nchini humo waliichangia habari hiyo kupitia mitandao mbalimbali iliyokuwa ya kwanza kuandika habari hiyo. “Mh! Inakuwaje Diamond aongee haya sasa wakati ambao ameshaachana naye? Muda wote alikuwa wapi? Au kwa sababu ana kifaa kipya?” alihoji mdau mmoja mtandaoni.

 

Mfuasi mwingine wa mtandao huo alihoji kuwa, Diamond amepatwa na nini kwani tangu wamwagane, hakuwahi kumzungumzia vibaya zilipendwa wake huyo. “Mara nyingi nimekuwa nikiona Mondi (Diamond) anamzungumzia vizuri Zari lakini ghafla tu amemzungumzia vibaya kweli?”

 

ZARI AMWAGA MBOGA

Zari naye hakuwa nyuma, kupitia mitandao yake ya kijamii ikiwemo Snapchat, alimtolea uvivu mzazi mwenziye huyo kwa kumwambia kuwa anasumbuliwa na wivu huku akimshauri kukaa kimya kama hana cha kuzungumza. “Wakati mwingine ni vyema kukaa kimya moja kwa moja, kunishambulia mimi kwenye mahojiano yako hakuwezi kukuongezea hata shilingi katika akaunti yako,” alisema Zari.

MAPOVU KAMA YOTE

Kuonesha kwamba yupo ‘serious’, Zari aliendelea kushusha mapovu kama yote kwa mzazi mwenzake huyo ambaye kwenye uhusiano wao Mungu aliwazawadia watoto wawili, Tiffah na Nillan. “Wivu utakuua wewe. Namshukuru Mungu nimebarikiwa, nimepata mwanaume mpya na ni bora kuliko wewe katika kila kitu,” alisema Zari kupitia mtandao wa Snapchat.

 

TUJIKUMBUSHE

Zari alitangaza kumwaga Diamond Februari 14, mwaka jana, Siku ya Wapendanao ambapo alitumia ukurasa wake wa Instagram kueleza uamuzi wake huo huku akitaja sababu kubwa ya kumuacha ni msanii huyo kutotulia ‘njia kuu’.

 

Tangu atamke uamuzi huo, Diamond alionekana kufanya jitihada za kurudisha penzi lake lakini hata hivyo hazikuzaa matunda, hadi mwishoni mwa mwaka jana alipoamua kutangaza uhusiano wake mpya na mrembo kutoka Kenya, Tanasha Dona ambaye ni mtangazaji na mwanamitindo nchini humo.

Stori: Erick Evarist, Ijumaa Wikienda


Loading...

Toa comment