Kwa mbio za Diamond, Kiba ana haya ya kufanya!

STORI: Na Andrew Carlos | RISASI JUMATANO| Risasi Vives

ALLY Saleh Kiba, ni msanii mkubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki. Ni mtu ambaye hana historia ya Bongo Fleva au chuki tu, ndiye anaweza kumbeza mwanamuziki huyu mwenyeji wa Mkoa wa Kigoma.

Ali Kiba

Ni miongoni mwa wasanii wachache sana waliowahi kutangulia mbele, wenzake wakifuata nyuma. Yes, alipoibuka na kibao chake cha Cinderella, pale robo ya mwisho ya mwaka 2007, aliukamata usukani, licha ya kuwa aliwakuta ma-legend kibao.

Huo ukawa wakati wake kama ambavyo baadhi ya wasanii wachache waliweza kupata bahati hiyo. Maana kabla yake, kuna ambao nao waliwahi kushika usukani, baadhi yao ni kama Profesa Jay, Mr Nice na Juma Nature.

Diamond Platinumz

Wakati wa Kiba ulimalizika baada ya kuibuka kwa Diamond Platnumz ambaye bado yupo kileleni, kwa zaidi ya miaka mitano sasa na hakuna dalili zinazoonyesha anaweza kuwekwa pembeni na wenzake, licha ya rundo la chipukizi kuibuka na kufanya vizuri.

Kwa bahati mbaya, kuna mashabiki wenye nia njema, hawaamini kama Diamond ni mzuri kuliko Ali Kiba. Nasema wana nia njema kwa vile siamini kama wanamaanisha wanachosema, isipokuwa wanataka kuufanya muziki huu uendelee kuchangamka, isije kuonekana kama ni wa mtu mmoja.

Walifanya hivyo wakati ule walipokuwa wakimpambanisha Juma Nature na Inspekta Haroun, Profesa Jay na Sugu na hata enzi za Mr Nice akihasimiana na Dudubaya. Walitengenezwa wapinzani wa uongo na kweli, ilimradi kama nilivyosema hapo juu, maisha yaendelee.

Lakini wakati mashabiki hao wenye nia njema wakifanya hivyo, kwa namna inavyoonekana, Ali Kiba ni kama ‘ameingia mkenge’ na kuamini kuwa yeye ni bora kuliko Diamond kimuziki. Kiukweli, licha ya ubora wa sauti yake, ukongwe wake na hata uwezo mkubwa alionao, mwimbaji huyu wa Kibao cha Aje, ameachwa mbali.

Mashabiki wa Kiba wanatoa tuhuma za upande wa pili kuwa unatumia nguvu kubwa kupromoti nyimbo zake, wananunua baadhi ya tuzo ili aonekane anafanya vizuri na kwamba mtu wao hana kile wenyewe wanakiita ‘show off’.

Binafsi ningependa kuona Kiba anafikia levo za Diamond ili tuzidi kuongeza idadi ya wasanii wa kuishambulia Afrika, baada ya jitihada za miaka mingi kuanza kuzaa matunda. Na ili aweze kufanya hivyo, kama kweli ana dhamira, yafuatayo ni miongoni mwa mambo anayopaswa kuyafanyia kazi mara moja.

Anatakiwa kuwekeza katika muziki wake. Sanaa hii hivi sasa ni biashara kubwa na ili uifanye vizuri ni lazima uwekeze vya kutosha. Studio, prodyuza bora, video nzuri na promosheni ya kutosha.

Humuoni Kiba akiingia na kutoka katika vituo vya redio na televisheni kusambaza kazi zake, humuoni akifanya kampeni katika mitandao ya kijamii kuhamasisha watu kuitafuta ngoma yake na ni nadra kumsikia akiingia vyumba vya habari tofauti kwa sababu ya kutafuta sapoti ya kazi yake mpya. Labda ni kazi ya menejimenti, lakini inapendeza mwenyewe akiwa ‘front’.

Kitu kingine ambacho King Kiba anapaswa kukifanya ni umakini pia awapo jukwaani. Kama watu wanampima na Diamond basi ni vyema naye amtazame mpinzani wake, namna anavyojiandaa kwa shoo, je maandalizi yanafanana?

Lakini pia Kiba yuko mbali na media. Siyo rahisi kumpata msanii huyu kwa ajili hata ya mahojiano tu au kuweka mambo f’lan sawa. Yeye ni staa, mambo mengi yanaibuka yanayomhusu, yanahitaji ufafanuzi. Kuna wasanii ambao yeye aliwakuta wako kwenye gemu miaka kumi, lakini hadi leo wanahitaji sapoti ya media.

Anyway, nisiongee mengi sana lakini ukweli unabaki palepale kwamba Kiba anatakiwa kubadilika kama anataka kuleta ushindani wa kweli kwa Diamond vinginevyo atazidi kuachwa nyuma kimuziki.

 


Loading...

Toa comment