The House of Favourite Newspapers

Kwa Mwanangu Nitakayemzaa 29

0

Mtima, mtoto wa Abikanile, msichana aliyeteseka sana siku za uhai wake, kisa kikiwa ulemavu wa ngozi anafanikiwa kuufahamu ukweli juu ya asili yake ambao alifichwa kwa muda mrefu na walezi wake, bwana na bibi Johannes, walioamua kumueleza baada ya yeye kung’ang’ania iwe hivyo.

Ukweli huo alioambiwa ulimuumiza sana moyoni kiasi kwamba akajikuta akijenga chuki dhidi ya binadamu waliomtesa mama yake, Abikanile kiasi cha kumsababishia kufa kifo cha kinyama.

SONGA NAYO…

 “Hello,” Destiny aliita kwa sauti nyembamba.

“Mtima!” aliita tena baada ya kuona kijana huyo hamjibu chochote, lakini hali ilikuwa vilevile, hata aliporudia zaidi ya mara tatu, akaamua kumsogelea hadi alipokuwa na kumgusa, Mtima alionesha kushtuka sana!

“Unawaza nini?” Destiny alimuuliza.

“Hakuna chochote.”

“Kwa nini unanificha?”

“Huo ndiyo ukweli.”

“Si kweli!”

“Ni kweli.”

Destiny alishindwa kuongeza maneno yoyote yale baada ya Mtima kusisitiza kuwa hakuwa na tatizo lolote lile, alibaki akijiuliza akilini sababu za kijana huyo kumficha kilichokuwa kinamsibu lakini hakuweza kabisa kupata jibu, kilichomsikitisha zaidi ni namna ambavyo Mtima alikuwa amekondeana kutokana na mawazo.

Kitu ambacho Destiny hakukifahamu, baada ya Mtima kuambiwa ukweli juu ya asili yake pamoja na ya wazazi wake, alitokea kujenga chuki kuu dhidi ya binadamu, mara kwa mara alikuwa anawaza hao binadamu wenyewe walikuwa na mamlaka gani ya kuwaua, kuwanyanyasa na kuwabagua walemavu wa ngozi huku siyo wao waliyowaumba!

Aliendelea kujiuliza walimchukulia mlemavu wa ngozi kuwa kiumbe wa namna gani? Mnyama, ndege au mdudu?

Alijiuliza maswali mengi lakini jibu alilopata ni kwamba walemavu wa ngozi pia ni binadamu kama walivyo binadamu wengine, tofauti yao ni kwamba wao katika ngozi yao wamekosa vinasaba (genes) ambavyo vinatengeneza rangi ya ngozi kuwa ya kawaida, macho na nywele ambavyo vinajulikana kama melanin.

Kwa kasi ya ajabu, chuki dhidi ya kulipa kisasi kwa binadamu kama mshahara kwa yale waliomtendea mama yake ilianza kuota mizizi ndani ya kifua chake, kijana huyo akaapa kupambana nao, akasema liwalo na lile na hakuhitaji mtu yeyote kumzuia kuanzisha vita hiyo ambayo ingemhusu kila kiumbe anayeitwa binadamu ulimwenguni kote!

Saa, siku na miezi vikazidi kuyoyoma na kila tabia njema aliyokuwa nayo Mtima, kipindi hiki alikuwa na utofauti mkubwa na alivyokuwa kipindi cha nyuma,  tabia zake zilikuwa za kikorofi, ugomvi na mtu asiyeshaurika wala kumsikiliza yeyote yule, mawazo yake yalikuwa kulipiza kisasi tu.

Walezi wake pamoja na mama yake mdogo, Alile walijitahidi kumsihi kuachana na wazo hilo lakini hakuwa tayari kabisa kuurudisha moyo wake nyuma, alikwishaamua hata kuyatupilia mbali malengo aliyokuwanayo pamoja na Destiny ya kuanzisha kampuni kubwa ya uchoraji na utengenezaji wa katuni ili tu aikamilishe azma yake hiyo.

“Mtima mbona umebadilika hivi?”

“Destiny naomba usifuatilie maisha yangu!”

“Kumbuka mimi ni rafiki yako!”

“Haijalishi, maisha yangu hayakuhusu.”

“Yananihusu maana pia tuna malengo ya pamoja.”

“Sahau kuhusu yote yaliyopita, fuata maisha yako.”

Destiny hakuwa na lolote la kuongea tena zaidi ya hayo, roho yake ilimuuma mno kuona rafiki aliyempenda kuliko kitu chochote duniani alikuwa amebadilika na kuwa na tabia za kinyama zizizofaa kuigwa na binadamu yeyote yule, akakumbuka mambo mengi waliyoyafanya pamoja tangu wakiwa watoto wadogo jambo lililomfanya kushinda siku hiyo yote akiwa amejifungia chumbani kwake akilia kwa uchungu.

“Mwenyezi Mungu msaidie Mtima siku moja abadilike!” aliongea msichana huyo katikati ya kilio kikali huku ameikumbatia picha ya Mtima.

Lakini machozi na maombi yake vilionekana kuwa dua la kuku, Mtima alikuwa amekwishaamua kuwa mnyama, kutokana na tabia hizo baada ya siku chache hakuna ambaye hakumfahamu katika chuo hicho cha sanaa cha Amsterdam.

Kazi yake kubwa wakati huo ikawa kujifunza kuruka sarakasi, michezo ya ngumi, kunyanyua vyuma vizito na kujifunza mbinu tofautitofauti za kivita.

Tofauti na Destiny, rafiki yake mkubwa akawa Abdulrahman ambaye alimshirikisha juu ya azma yake ya kulipiza kisasi, akakubali kushirikiana naye kwa kila kitu katika vita hiyo dhidi ya binadamu ambao hasa waliolengwa ni watu weusi, baada ya kufuatilia na kujua kuwa barani Afrika ndiko walemavu wa ngozi walionewa zaidi.

Ili kufanikisha mpango wao huo, Mtima na Abdulrahman waliamua kwanza kuachana na masomo kisha wakaanzisha kundi la kigaidi waliloliita WAB (War Against Blacks), wakalisajili kwenye mtandao wa makundi makubwa ya kigaidi duniani yakiwemo Al-Qaeda, Al-Shabaab na Boko Haram, baada ya muda wakaufahamu utaratibu mzima wa kupata silaha za kivita pale ambapo wangezihitaji.

Siku nazo hazikusimama, zilizidi kusonga mbele kwa kasi ya kimbunga ambapo kwa wakati huo kila aliyekuwa anamhusu Mtima alimkatia tamaa na kuamua kuyakabidhi maisha yake mbele za Mungu huku wakisema yeye pekee ndiye aliyekuwa anaifahamu hatima yake.

Je, nini kitaendelea? Usikose kufuatilia wiki ijayo.

Leave A Reply