The House of Favourite Newspapers

Kwa Mwanangu Nitakayemzaa

0

Huku Alile akipanga kumtafuta dada yake Abikanile, msichana huyo alikuwa mitaani akitangatanga kutafuta eneo walikoishi watu wasio na makazi ambapo baada ya kutembea umbali mrefu alifanikiwa kuipata sehemu hiyo alikopokelewa na msichana wa Kizungu Jesse.

Majira ya usiku wa siku hiyo akiwa amelala pamoja na Jesse, Abikanile alivamiwa na vijana wawili waliombaka na kumsababishia damu nyingi kuvuja katika sehemu zake nyeti, pia walimuacha na maumivu makali sana.

TAMBAA NAYO…

“Wameniumiza Jesse, huenda wameniambukiza hata maradhi.”

“Usiseme hivyo, mkabidhi Mungu kila jambo alisimamie.”

Abikanile hakuongeza tena neno zaidi ya kugumia kwenye kwikwi, usiku wote wa siku hiyo alikesha akilia na kuiutia nafsi yake mwenyewe, alifahamu kama asingekubali kushawishiwa na Bartoz Arian kujiingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya huenda asingefikia hatua hiyo.

Moyo wake ulimuuma mno, akaona ni afadhali kufa apumzike kuliko kuishi katika maisha ya kupambana na matukio ya kutisha kila kukicha.

Hatimaye kulikucha, msichana huyo akayaanza maisha mapya ya kutangatanga mitaani kutafuta chochote cha kutia kinywani akiwa na mwenyeji wake Jesse.

Kwa upande wao familia ya mzee Van Loo, kupotea kwa Abikanile kuliendelea kuwachanganya sana, japo walitumia kila jitihada kuhakikisha wanampata msichana huyo, mwezi wa kwanza ulikatika, wa pili na hata wa tatu ulifuata bila hata kupata fununu ni wapi alikuwa.

Wakakata tamaa kabisa, wakaamua kuliacha jambo hilo mikononi kwa Mungu na kila mara kwenye sala walimuombea Abikanile kuishi akiwa kwenye mikono salama huko alikokuwa.

 

***

Siku zikaendelea kusonga mbele, lakini hata baada ya miezi mitatu kukatika tangu Abikanile ajiunge na kundi la vijana hao wasio na makazi bado kitendo cha kubakwa alichofanyiwa na kina Ruben pamoja na Lars kilikuwa hakijafutika katika akili yake.

Huo kwake ulikuwa ni unyama ambao ulimuumiza kila mara, lakini hakuwa na namna nyingine ya kukabiliana na hali hiyo zaidi ya kuikubali, akaendelea kuzisindikiza siku zilizozidi kusonga mbele huku akizidi kuyazoea maisha hayo ya mitaani.

Alikula kwa kuombaomba pesa na alivaa kwa kupewa nguo zilizochakaa na watu wenye roho zenye utu alipokuwa anapita kwenye majumba yao akiomba msaada.

“Jesse,” Abikanile aliita kwa sauti ya upole.

“Nambie Abikanile.”

“Unajua huu ni mwezi wa tatu  sijaziona siku zangu!”

“Mwezi wa tatu! Itakuwa hali ya mtaani imekukataa.”

“Hapana mimi nahisi nina ujauzito.”

“Umepewa na nani, mbona hujawahi kuniambia kama kuna mtu unatoka naye?”

“Sina mtu, ila nahisi kina Ruben waliponibaka walinipa ujauzito!” Abikanile aliongea huku akianza kudondosha machozi.

Hali aliyokuwa anaihisi ilimfanya ahisi kuwa na ujauzito, moyo wake ulimuuma sana, kila sekunde alikuwa anawaza ni maisha ya namna gani ambayo angeyaishi mitaani akiwa na ujauzito hadi kufikia hatua ya kujifungua.

“Itabidi kesho twende ukapime.” Jesse alishauri.

“Nina ujauzito Jesse, kwenda kupima ni kuhakikisha tu.”

“Sawa, ni vizuri kujiridhisha.”

Ushauri alioutoa Jesse, Abikanile hakuupinga, siku iliyofuata walikwenda kwenye kituo cha afya walichokuwa wanamudu gharama zake ili kuhakikisha juu ya jambo hilo.

Baada ya kufika kwenye hospitali hiyo Abikanile alifanyiwa vipimo na kama alivyokuwa anahisi kweli alikutwa na ujauzito wa miezi mitatu.

Bila kuelewa akiwa mbele ya Dk. Resh Wouda, Abikanile alijikuta akianza kulia kwa uchungu, akainuka bila hata kuaga, akatoka ndani ya chumba hicho na kuanza kuelekea nje kule alikokuwa Jesse.

“Daktari amekwambiaje?” Jesse alimuuliza lakini Abikanile hakujibu lolote lile zaidi ya kulia, Jesse alifahamu nini kilikuwa kinaendelea.

Siyo siri, kuwa na ujauzito lilikuwa jambo zito sana kwa Abikanile kukabiliana nalo, alizidi kulia kwa uchungu huku akiwa hapati majibu ya nini itakuwa hatima ya maisha yake mitaani akiwa na ujauzito huo. Jesse aliendelea kumbembeleza bila mafanikio yoyote yale.

“Abikanile, itabidi tufanye juu chini tuutoe,” Jesse alimshauri.

“Unasemaje Jesse?”

“Tutoe, ni vigumu kuishi ukiwa mjamzito mitaani.”

“Siwezi kutenda dhambi kubwa kiasi hicho, bora nife lakini siyo kuutoa ujauzito huu.”

Abikanile alionyesha kuwa na msimamo mkali juu ya kutoutoa ujauzito aliokuwa nao jambo lililomshangaza Jesse, lakini ukweli ni kwamba msichana huyo asingeweza kumlazimisha juu ya suala hilo, aliamua kukubaliana naye wakarudi hadi yalipokuwa makazi yao kule mitaani.

Je, nini kitaendelea? Maisha ya Abikanile yatakuwaje mitaani baada ya kubeba ujauzito? Usikose kufuatilia wiki ijayo.

Leave A Reply