The House of Favourite Newspapers

Kwa Mwanangu Nitakayemzaa – 34

0

Siku hiyo Mtima na Abdulrahman walikuwa katika mapumziko ambapo siku iliyofuata walikuwa na kazi ya kwenda kushambulia katika eneo liitwalo Chaka-kiganjo kwenye Kaunti ya Nyeri karibu na mpaka wa Somalia na Kenya. Vijana hao walikuwa tayari, gado kwa kazi, kutokana na shauku ya kufanya mauaji waliona saa haziendi kabisa.

SONGA NAYO…

HATIMAYE kulikucha, mida ya saa 9 alfajiri Mtima na Abdulrahman walikwenda hadi karibu kabisa na mpaka wa Kenya na Somalia walikokuwa wamepanga kufanya tukio la mauaji ya kutisha.

Kama ilivyokuwa kawaida ya eneo hilo, watu walikuwa ni wengi sana wakiendelea na mishemishe zao, hakuna hata mtu aliyeonekana kuhisi hali yoyote ya hatari kutokea siku hiyo, kila kitu kilionekana kwenda sawa.

Akiliendesha kwa tahadhari gari lao aina ya Jeep, Mtima alizidi kuambaaambaa katika eneo hilo huku Abdulrahman akitafuta tageti ili aanze kuwashambulia watu wasio na hatia.

“Hapa vipi?”
“Sogea mbele kidogo!”
“Poa,” Mtima aliliendesha gari kwenda mbele kidogo na kuliegesha.
Kisha kwa kitendo cha haraka walishuka, wakaanza kuwashambulia bila huruma yoyote ile wakazi wa eneo hilo.

Hali ilikuwa inasikitisha mno, shambulio hilo la kushtukiza liliwafanya watu wakanyagane wakijaribu kuyaokoa maisha yao, kiasi kwamba hata wafanyabiashara wadogowadogo waliokuwa na watoto wao katika eneo hilo la kazi walijikuta wakiwasahau kwa kuokota midoli na vitu vingine kisha kukimbia ili kuyaokoa maisha yao.

Mtima na Abdulrahman hawakuwa na mzaha hata kidogo, waliendelea kuua kwa kutumia bunduki zao aina ya Ak 47, ndani ya dakika tatu kama walivyokuwa wamepanga tayari walikwisha waua zaidi ya watu 700, wakalidandia gari lao ili watoweke, lakini muda huohuo kwa mbali vilisikika vingo’ra vya magari ya polisi vikija katika eneo hilo.

Walikuwa ni wanajeshi wa mpakani waliofika baada ya kusikia milio ya risasi iliyokuwa inarindima, kwa Mtima na Abdulrahman jambo hilo liliashiria hatari kubwa sana mbele yao, Mtima akaliondoa gari kwa mwendo mkali lakini tayari magari ya wanajeshi yapatayo matano yalikuwa yamekwisha wakaribia karibu zaidi. Wakaanza kufukuzana huku wakirushiana risasi.

“Ongeza kasi wanatukaribia!” Abdulrahman alimwambia Mtima.
“Hii ndiyo kasi ya mwisho!”
“Jitahidi tutakufa!”

“Nalielekezea gari kwenye maporomoko.”
“Ni kheri kuliko kufa kwa mateso makali baada kukamatwa.”
Kutokana na hali halisi, Mtima na Abdulrahman waliamini hawakuwa na nafasi nyingine ya kuyaokoa maisha yao zaidi ya kulielekezea gari lao kwenye Maporomoko ya Mto Afmadow wakitegemea Mungu kutenda miujiza yake, magari ya wanajeshi wa Kenya waliokuwa eneo hilo la mpakani yalikuwa yamewazunguka kila upande.
“Kaka kwakheri,” Mtima alimwambia Abdulrahman.

“Kwaheri pia, inaniuma tunakufa bado hutujafikia nusu ya azma yetu.”
“Hakuna jinsi ni lazima tufe, hatuwezi kupona kwenye maporomoko haya.”
“Mungu anaweza kutenda miujiza yake!”

Kwa ujasiri mkubwa, Mtima aliliendesha gari na kwenda kulitosa kwenye maporomoko hayo ya Mto Afmadow, nyuma walisindikizwa na risasi nyingi lakini baada ya sekunde hamsini gari hilo lilidumbukia kwenye maji chubwi, risasi zikaendelea kurindima juu yake kwa kitendo cha haraka pia wanajeshi wa Kenya walishuka kwenye magari yao na kulizunguka eneo hilo lote! Walipania kuwatia nguvuni vijana hao hasa walipogundua kuwa ndiyo wanaounda kundi la Wab.
***
Maandamano yalikuwa yamepamba moto katika miji mbalimbali nchini Kenya na Somalia.

Wakazi kwenye miji hiyo waliamua kuandamana huku wakilaani mauaji ya kinyama yaliyokuwa yanatendwa na Kundi la Wab (War against Blacks) ambapo nchini Kenya wananchi walimshinikiza waziri wao wa usalama na ulinzi, Jenerali James Nkoyo kuhakikisha ndani ya mwezi mmoja analiangamiza kundi hilo la sivyo ajiuzulu wadhifa wake kabla ya wao kuchukua uamuzi.

Je, kitafuatia nini? Usikose simulizi hii wiki ijayo hapahapa.
Jambo hilo lilifanya ulinzi nchini humo kuimarishwa zaidi, mbali na hilo nchi nyingi za jirani zilitoa tahadhari kwa wananchi wake kuitembelea Kenya.
Swali la kina nani waliunda kundi la Wab, wapi lilikuwa chimbuko lao, kwanini walifanya mauaji hayo na walifadhiliwa na nani silaha lilizidi kuwaumiza maofisa wengi wa usalama, lakini wachambuzi wa masuala ya kijasusi walisema huenda kikundi hicho kilikuwa kinashirikiana kufanya ugaidi na vikundi vya kigaidi vya Somalia.
Maeneo ya mipakani, mashuleni, kwenye vituo vikubwa vya kibiashara, sehemu za ibada na kila kona kulipo na mikusanyiko ya watu ulinzi uliimarishwa zaidi, kazi ikawa moja tu, kupambana na kundi la WAB.

***

Mtima na Abdulrahman walikuwa wameingia kwenye kumi na nane za majeshi ya Kenya yaliyokuwa yanawatafuta kwa udi na uvumba.
Ambapo baada ya mafukuzamo ya muda mrefu, Mtima alilielekezea gari lao kwenye Maporomoko ya Mto Afmadow hiyo yote kujaribu kuyaokoa maisha yao.
Gari lilikwenda kwa kasi ya ajabu na kujipigiza kwenye maji ya mto huo, kioo cha mbele kilipasuka, kikawachana chana vibaya akina Mtima, lakini kutokana na mafunzo ya kikomando waliyopitia vijana hao walijitahidi kupambana na maumivu ya kuchanwa na kioo wakachomoka ndani ya gari hilo kwa kupitia kwenye kioo cha sehemu iliyopasuka kisha wakaanza kuchapa maji bila kuelewa kila kona wanajeshi wa Kenya walikuwa wametanda!

Leave A Reply