The House of Favourite Newspapers

Kwa Mwanangu Nitakayemzaa-39

0

ILIPOISHIA:

Matukio waliyokuwa wanafanya Kundi la WAB yalikuwa yanatisha kiasi kwamba kila kona wakawa gumzo, walishaua watu wengi mno, azma ya Mtima ilikuwa kulipiza kisasi kwa unyama aliotendewa mama yake mzazi Abikanile kutokana na ulemavu wake wa ngozi, lakini katika hali isiyo ya kawaida, usiku f’lani Mtima aliota ndoto iliyomshtua sana!TAMBAA NAYO…

BAADA ya kushtuka toka ndotoni Mtima alijikuta akizama kwenye dimbwi zito la mawazo ambalo asingemudu kuogelea, mawazo yalizidi kupamba moto akajikuta pia akikumbuka matukio ya kinyama aliyowahi kufanya huko nyuma na aliyokuwa amepanga kufanya na rafiki yake Abdulrahman, kuua watu ovyo kwa kisasi.

Kumbukumbu hiyo ndiyo iliyomuumiza, Mtima akajihisi mwenye hatia mno kwa maisha hayo aliyokuwa amechagua kuishi, lakini moyoni alikumbuka kuwa sababu kubwa ilikuwa ni kulipa kisasi kwa yale aliyokuwa ametendewa mama yake mzazi, ukweli ni kwamba alizidi kupata wakati mgumu sana kuwaza jambo la kuamua wakati huo!

“Kwa nini tunaua watu wasio na hatia? Ni kweli nina hitaji kulipiza kisasi lakini dhambi itokanayo na damu ya watu wasiohusika hasa watoto wasiofahamu lolote tutaiepukaje?” Mtima alijiuliza maswali bila kupata majibu.

Kumbukumbu ya maisha yake ikazidi kumliza, akakumbuka udogoni kwake, alivyosaidiwa na kulelewa na familia ya Bwana na Bibi Johannes zaidi upendo waliomuonesha, hayo yote aliyoyakumbuka yalimfanya taratibu kuanza kuchukia kile alichokuwa anafanya.

Usingizi wote ukapeperuka, akaamua kuinuka na kuchukua msokoto wa bangi kisha kuanza kuvuta, lakini pia alipanga kutomshirikisha rafiki yake Abdulrahman juu ya ndoto aliyoota.
***
Kwa upande wa Destiny, baada ya kumaliza masomo ya uandishi wa habari nchini Marekani na kurudi Kenya, alianza mara moja kuifanya kazi ya kutembelea viwanja mbalimbali vya mapambano alikosikia Kundi la Wab linafanya uhalifu.

Kwa kuwa kabla ya kuichukua hatua hiyo alijitahidi kwa kiasi kikubwa kujenga uhusiano wa karibu na vyombo mbalimbali vya habari wakiwemo waandishi walioelewa kile anachofanya, jambo hilo lilimsaidia kufahamika kwa watu wengi, ikawa rahisi kufika kila kona aliyokuwa anahitaji kwenda.

Alikwisha tembelea nchi za Somalia na miji tofauti ya Kenya pia wakati huo alikuwa Tanzania alikosikia kundi hilo la Wab lilihamishia uhalifu wao, alifikia katika Hoteli ya Nsengiyunva Bay.

“Ninakupata,” Destiny aliitika baada ya kupokea simu yake ya mkononi.
“Niko mapokezi,” sauti upande wa pili ilisikika.
“Umeshafika mara hii?”
“Nilikotoka si mbali.”

“Sawa, nakuja.”
Destiny alijiinua haraka kitandani alipokuwa amejipumzisha, akajiweka sawa kisha akaelekea hadi mapokezi kuonana na mgeni wake ambaye alikuwa ni Elizabeth Shayo, mwandishi wa habari maarafu Tanzania waliyekuwa wanawasiliana mara kwa mara kupitia mitandao ya kijamii na alimtaarifa juu ya ujio wake Tanzania kabla ya kufika.
“Karibu sana Elizabeth.”

“Asante, habari za Kenya?”
“Kawaida tu.”

Walielekea hadi kwenye mgahawa wa hoteli hiyo wakachukua siti mahali na baada ya kuhudumiwa kwa vinywaji maongezi yao yalikolea.
“Kazi ya kuchukua matukio ya uhalifu wa Kundi la Wab ni hatari sana,” Elizabeth alimwambia Destiny wakiendelea na maongezi.

“Ni kweli, lakini kama mwandishi wa habari sipaswi kuwa muoga.
“Uko sawa, ila kumbuka kuna maisha mbele ya kila kitu.”
“Achana na hilo bwana, wewe niambie utanisaidiaje?”
“Nakusikiliza wewe!”

“Kupitia vyanzo mbalimbali vya habari, kundi hilo limetoa taarifa kuwa kesho linategemea kufanya mashambulizi katika kituo maarufu cha biashara jijini Dar, hospitali maarufu au kumbi za starehe.”
“Mh! Tutajigawaje?”

“Jambo la muhimu ni kutumia akili zetu za kuzaliwa pamoja na taaluma tuliyonayo.”
“Unamaanisha nini?”
“Namaanisha kwa kufikiria tu Wab wanafanya mashambulizi ili wawaumize watu na si vinginevyo, sasa kati ya maeneo hayo kuna uwezekano mkubwa wa kufanya tukio hilo hospitalini!”

“Hospitali ziko nyingi, hatuwezi kufahamu.”
Elizabeth alionekana kuwa na wasiwasi na mafanikio ya kazi hiyo ambayo Destiny alikuwa anaililia. Hakuona mwanga wa kulifanikisha jambo hilo, zaidi alimshangaa sana mwandishi huyo kwa jinsi alivyokuwa na matumaini ya kufanikisha malengo yake.
Je, nini kitaendelea? Usikose kufuatilia simulizi hii wiki ijayo.

Leave A Reply