The House of Favourite Newspapers

Kwa Mwanangu Nitakayemzaa

0

Alile alikuwa bado mitaani kila siku akimtafuta dada yake Abikanile akisaidiana na rafiki yake Max Dean, miezi tisa ilikwishapita bila mafanikio yoyote ya kumpata wala kusikia fununu za wapi alikuwa, wakakata tamaa, lakini jambo la kushangaza siku ambayo waliamua kuahirisha rasmi kumtafuta, wakiwa mtaani waliliona kundi la watu, waliposogea kushuhudia nini kilikuwa kimetokea Alile alipigwa butwaa alipomuona msichana mwenye ulemavu wa ngozi akiwa amelala chini hajitambui, akamdondokea na kumkumbatia, watu wote waliokuwa mahali pale walibaki midomo wazi.

TAMBAA NAYO…

Akiwa mitaani Abikanile alizidi kula msoto huku ujauzito wake ukizidi kukua kwa kasi ya ajabu.

Jesse akawa msaada wake mkubwa, mara kwa mara alikuwa anamuacha kwenye makazi yao kwenda kuombaomba ambapo baadaye alimletea vyakula na mahitaji mengine muhimu.

“Abikanile..”

“Nambie Jesse.”

“Mtoto wako ukimzaa jina la baba yake litakuwa nani?”

“Swali gumu sana maana  sielewi atakuwa wa Lars au Ruben!”

“Kwani nani aliyeanza kukubaka siku ile?”

“Hiyo siyo sababu ya msingi, yeyote kati yao anaweza kunipa ujauzito!”

“Hili ni suala gumu!”

“Usijali Jesse, mtoto huyu nimepewa na Mungu! Hata kama baba yake hajulikani, nitampenda na kumjali mno maana ndiye ndugu yangu pekee nitakayekuwa naye duniani.

Huo ulikuwa ni usiku wa saa tano, muda ambao Abikanile na Jesse walikuwa wamejipumzisha, tofauti na siku zote tangu wafahamiane, siku hii waliongea mambo mengi mno.

Jesse alimsimulia Abikanile maisha yake kwa ujumla na sababu iliyomfanya afikie hatua ya kuishi maisha hayo ya kutangatanga mitaani, Abikanile naye kwa mara ya kwanza alimsimulia Jesse ukweli juu ya maisha yake.

Muda ukazidi kusonga mbele, hatimaye wakapitiwa na usingizi, wakalala.

Akiwa katikati ya usingizi ndani ya usiku mnene, Abikanile alishitushwa na sauti ya kilio kutoka pembeni yake. Alikurupuka na kuamka.

“MUNGU WANGU!”

Alipigwa na butwaa baada ya kufumbua macho na kushuhudia kundi la watu wasiopungua sita wakimfanyia Jesse unyama wa kumbaka.

Abikanile alitamani sana kumsaidia rafiki yake huyo lakini alishindwa, watu wale walikuwa ni wengi tena walikuwa na silaha mkononi.

Jesse alijitahidi kufurukuta ili kujikwamua mikononi kwa jamaa hao lakini alishindwa, wote walifanikisha kumuingilia bila huruma. Damu nyingi zilimtoka, pia alibaki analia kwa uchungu huku kadiri muda ulivyozidi kwenda akawa anaishiwa nguvu.

“Nakufa Abikanile rafiki yangu,” Jesse aliongea kwa shida huku amelala miguuni kwa Abikanile aliyekuwa anamhudumia.

“Hapana Jesse huwezi kufa…”

Ukweli ni kwamba hali haikuwa nzuri kwa upande wa Jesse, damu nyingi zilikuwa zinamvuja katika sehemu zake nyeti na aliendelea kuishiwa nguvu kwa kasi ya ajabu, alipiga kelele za maumivu huku Abikanile akijitahidi kumhudumia lakini mida ya saa kumi na moja za alfajiri Jesse alipoteza maisha!

Abikanile alilia mno, Jesse kwake alikuwa ni zaidi ya ndugu maana alikuwa anamsaidia kwa mambo mengi kutokana na hali aliyokuwa nayo, msichana huyo hakufahamu nini ingekuwa hatima yake baada ya kifo hicho cha Jesse.

***

Kulipopambazuka  mwili wa Jesse ulichukuliwa na polisi waliomzika kwenye makaburi ya watu ambao ndugu zao hawakuwa wanatambulika. Habari za Jesse zikawa zimeishia hapo!

Siku zikaendelea kusonga mbele lakini wakati huo maisha kwa Abikanile yalizidi kuwa magumu kuliko kawaida, ilifikia hatua akawa anamaliza hata siku mbili bila kuweka kitu chochote kile tumboni ingawa alikuwa na ujauzito mkubwa, jambo hilo likamfanya azidi kukata tamaa akafahamu kwa namna yoyote ni lazima angekufa.

Hayo yalikuwa ni majira ya saa nane za mchana katika siku ya Jumatatu, Abikanile alikuwa hajala kitu chochote takribani siku mbili, hakuwa na nguvu kabisa mwilini mwake jambo lililomfanya kuhisi kufakufa hivi!

Akiwa amelala hapo kwenye eneo waliloishi vijana wasio na makazi msichana huyo alikuwa anasikia uchungu kuliko kawaida, alifahamu anakufa bila kulitimiza lengo aliloishi nalo kwa miaka mingi,  lengo la kuziondoa tofauti, unyanyasaji na mauaji ya walemavu wa ngozi (Albinism), Afrika.

Jambo lingine lililokuwa linamuumiza moyo ni namna alivyokubali Bartoz Arian kumharibia maisha  kwa kumuingiza katika matumizi ya dawa za kulevya, alijikuta akimchukia sana kijana huyo lakini kwa wakati huo alikuwa ameshachelewa, tayari maji yalikuwa yameshamwagika.

Akiendelea kuelea katika dimbwi hilo la mawazo, Abikanile alijikuta akianza kukiwaza kiumbe alichokuwa nacho tumboni, kutokana na hali aliyokuwa anaihisi alifahamu fika kuwa hata kama akibahatika kujifungua ni lazima angekufa bila kumuona mwanaye.

Roho ikamuuma mno, akawaza nini afanye ili endapo ikitokea akafa baada ya kujifungua na mwanaye kuishi apate taarifa juu ya maono aliyokuwa nayo, lakini hata baada ya kujiuliza sana jibu lilionekana kuwa gumu.

Je, nini kitaendelea? Abikanile atakufa? Vipi kuhusu Alile na huyo aliyemuona? Usikose kufuatilia Jumamosi ijayo.

JIUNGE NA GLOBAL BREAKING NEWS!

Leave A Reply