The House of Favourite Newspapers

Kwa Mwanangu Nitakayemzaa

0

Baada ya historia ndefu ya msichana aliyezaliwa na ulemavu wa ngozi Abikanile na kupitia mateso mengi hatimaye anapoteza maisha wakati akijifungua na kuzikwa katika makaburi  ya familia ya Bwana David Dean huko jijini Roterdam.

Kabla ya kufa Abikanile aliandika barua iliyokabidhiwa kwa mdogo wake Alile ikiwa imemlenga mwanaye aliyemzaa ambaye alichukuliwa na Mzee Johannes, mfadhili wa Alile aliyekwenda kumlea huko Amsterdam.

TAMBAA NAYO…

Baada ya miaka 7

January 1, 2001

SHAMRASHAMRA zilikuwa hazielezeki siku hiyo ya kwanza ya mwaka, mji mzima wa Paris na majimbo yake ulitawaliwa na kelele zenye nderemo za kila aina, watu wengi walionekana kuifurahia siku hiyo.

Ilikuwa ni siku ya Jumamosi ambapo bwana na bibi Johannes pamoja na Mtima walikuwa katika mji huo kulitembelea Jumba la Maonyesho la Louvre, sehemu iliyokuwa inatembelewa na mamilioni ya watu kila mara wakitoka sehemu tofauti duniani.

Malengo ya Jahannes na mkewe kulitembelea jumba hilo katika Sikukuu hiyo ya Mwaka Mpya, yalikuwa ni kuitazama picha ya Mona Lisa, iliyochorwa na mchoraji maarufu duniani Leonardo da Vinci, moja kati ya kazi nzuri za kihistoria kuwahi kufanyika kwenye sanaa ya michoro.

“Mtima unaiona hiyo picha ilivyo nzuri?” Johannes aliongea huku anaonyesha kwa kidole.

“Ndiyo babu.”

“Hiyo ndiyo picha niliyokuwa nakueleza kila mara.”

“Nzuri, nimeipenda!”

Bwana Johannes na mkewe waliamua kuifanya safari hiyo makusudi kabisa ili kumuwezesha mtoto wa marehemu Abikanile, Mtima kuuona mchoro huo wa Mona Lisa baada ya kukigundua kipaji kikubwa cha uchoraji alichokuwa nacho.

Kwa Mtima ilikuwa siku nzuri sana ya kukumbuka kwenye maisha yake maana alipata fursa ya kuziona kazi nyingi za kuvutia za wachoraji maarufu waliowahi kuishi duniani wakiwemo Titian, Rembrandt na Renoir, walezi wake pia walipiga picha nyingi za kumbukumbu, ambapo baada ya ziara hiyo siku tatu baadaye walirudi Uholanzi.

Wakati huo, Mtima alikuwa na umri wa miaka saba na mwanafunzi katika shule ya vijana wadogo ya Eijk Musdom Elementary, moja kati ya shule bora  za vipaji walipokuwa wakisoma watoto wa matajiri na watu mashuhuri.

Katika shule hiyo, Mtima alikuwa na marafiki wakubwa wawili, Abdulrahman Abdi Godane, mtoto wa bilionea mkubwa nchini Somalia aliyekuwa anajihusisha na biashara ya uchimbaji wa mafuta sehemu tofauti duniani na mwingine aliitwa,  Destiny David, binti wa Bi Rukia Okelo, aliyekuwa Balozi wa Kenya nchini Uholanzi.

Tofauti na Mtima, Abdulrahman alikuwa anapenda zaidi mchezo wa mpira wa miguu na urukaji wa sarakasi (acrobatics) na walitokea kuwa marafiki kwa sababu wote walikuwa wanafanya vizuri kwenye vipaji vyao.

Destiny, yeye alikuwa mchoraji na muimbaji wa muziki, mara kwa mara  ndiye aliyekuwa anaonekana kuwa karibu na kijana huyo, wakiwa wanachora au wakati wa mapumziko Destiny akimuimbia Mtima nyimbo za wasanii maarufu duniani alizokuwa amezikariri.

“Mtima, hili kovu lilitokana na nini?” Destiny alimuuliza Mtima siku moja.

“Niliunguzwa na pasi.”

“Pole.”

“Asante.”

Hayo ndiyo yalikuwa maisha yao, kukaa pamoja, kufurahi na kushirikiana kwa kiasi kikubwa.

Miaka ikaendelea kupita na Mtima alizidi kukua na kukomaa kiakili ambapo kwa umri wake wakati huo, aliweza kufikiri kwa kirefu zaidi na kupambanua mambo kwa upana wake.

Akiwa katika umri wa miaka kumi na nne kuna jambo lilikuwa linaisumbua  sana akili yake, ilikuwa ni kuhusu asili yake na wazazi wake, hata asili ya jina lake ilimchanganya sana maana lilitofautiana sana na yale ya Kiholanzi aliyokuwa anayafahamu.

Kila mara alipokuwa akijaribu kudadisi juu ya hayo, walezi wake walimwambia wazazi wake walifariki miaka mingi iliyopita, lakini mama yake alikuwa ni mwafrika na mlemavu wa ngozi, kuhusu jina walimwambia alilirithi kwa babu yake kutoka upande wa mama yake pia alitambulishwa Alile kuwa ni mama yake mdogo.

Ndiyo, ilikuwa ni rahisi yeye kukubali juu ya ukweli huo aliokuwa anaambiwa lakini kilichokuwa kinamshangaza zaidi, alipohitaji kumfahamu baba yake mzazi kupitia picha aliambulia majibu yasiyoridhisha bila kuonyeshwa picha, akawa anajiuliza ikiwa kweli walezi wake ni bibi na babu yake kwa upande wa baba yake kwa nini wakose kumbukumbu yoyote juu ya mzazi wake huyo? Ukweli ni kwamba suala hilo lilimfanya aishi bila furaha.

Kila mara akiwa nyumbani na shuleni Mtima akawa mtu wa kukaa kwa kujitenga, kadiri siku zilivyozidi kusonga mbele tabia hiyo ikawa sugu jambo lililowasumbua sana walezi wake pamoja na walimu shuleni, walijiuliza ni kwa namna gani wamsaidie kijana huyo lakini walikosa jibu!

Je, nini kitaendelea? Walezi wa mtima watamficha ukweli juu ya asili yake mpaka lini? Vipi kuhusu maisha ya kijana huyo kwa ujumla? Usikose kufuatilia wiki ijayo hapahapa.

JIUNGE NA GLOBAL BREAKING NEWS!

Leave A Reply