The House of Favourite Newspapers

Kwa Mwanangu Nitakayemzaa

0

ILIPOISHIA:

Huku Mtima na Abdulrahman wakiwa kwenye hali tete ya kuuawa na wanajeshi wa Kenya, Destiny alikuwa amemaliza masomo ya uandishi wa habari chuoni Notheastern, Marekani ambapo alitakiwa kusafiri hadi New York kwa ajili ya kupata ujuzi kwenye kampuni ya habari ya Wend Production.

Tambaa nayo…

MUDA ulipowadia alipanda ndege na kusafiri hadi jijini New York alikopokelewa uwanja wa ndege na mwanaume aliyejitambulisha kwa jina la Kenny Smith.

“Wend yuko wapi?” Ndilo swali la kwanza alilomuuliza Smith wakiwa kwenye gari.

“Kwenye majukumu yake.”

“Nitaonana naye.”

“Ni vigumu, yuko bize sana.”

“Sasa nitaanzaje mafunzo?”

“Maelekezo yote ninayo.”

Kenny Smith aliliendesha gari hadi ulipo Mtaa wa Queens Bridge, akaingia kwenye jengo kubwa la kifahari alikomkutanisha Destiny na mwanamke wa Kizungu, Vanessa aliyempa maelekezo na utaratibu wa namna gani angeishi kwenye kampuni hilo kipindi chote cha mafunzo.

Baada ya mazungumzo hayo, Destiny alipelekwa kwenye Hoteli ya Savanna ambapo ndiko alitakiwa kuishi, siku iliyofuata Vanessa alimkabidhisha kwa Criss Jacquiler, mwandishi wa habari mzoefu aliyetakiwa kuzunguka naye sehemu tofauti duniani wakiandika na kuripoti habari.

Hivyo ndivyo ilivyokuwa, siku chache baadaye Destiny na Jacquiler walikuwa kazini wakianzia hapohapo Marekani baadaye wakahamia barani Asia, Ulaya kisha Afrika kwenye nchi zilizokuwa na machafuko pamoja na mlipuko wa magonjwa hatari, baada ya miezi sita Destiny alikuwa amekomaa sana na alifahamu mambo mengi katika taaluma hiyo.

“Kwa sasa sina shaka kabisa na wewe!” Siku moja Jacquiler alimwambia Destiny wakiwa nchini Syria walikokwenda kufuatilia habari za machafuko kati ya Serikali ya Dikteta Bashar al Asad na majeshi ya upinzani.

“Asante sana Criss, sijioni shujaa bila wewe.”

“Usijali, kazi niliyopewa ni kuhakikisha unakuwa mzoefu kwenye taaluma hii, lakini nini kilikuvutia kuwa mwandishi wa habari?”

Destiny alikaa kimya kwa sekunde kadhaa akitafakari nini ajibu, kutokana na ukaribu waliokuwa nao, hakuiona sababu ya kumficha lolote Jacquiler. Alimweleza kila kitu juu ya lengo lake la kumbadilisha rafiki yake kipenzi Mtima aliyekuwa ameamua kujiingiza katika masuala ya kigaidi.

Ukweli ni kwamba, hilo lilikuwa ni jambo lililomshangaza sana Criss Jacquiler, kwake likawa darasa jipya kuwa upendo wa dhati duniani upo na watu wanaopenda kwa dhati bado wanaishi.

“Lakini Criss, juu ya hayo yote, nini maana na thamani ya kazi ya uandishi?” Destiny aliuliza.

Criss Jacquiler, mwanahabari aliyebobea hakuwa na budi kumweleza kuhusu kile alichohitaji kufahamu, ambapo alianza kwa kumsimulia hadithi iliyowahusu daktari na mfinyanzi akimwambia; siku moja daktari alifanya mkataba na mfinyanzi akimtaka kufinyanga sanamu ya marehemu mke wake.

Baada ya makubaliano walipatana kazi hiyo isizidi miezi mitatu, ilipokatika daktari alikwenda kudai sanamu lake, lakini kwa mshangao mkubwa mfinyanzi ndiyo kwanza alikuwa ameianza kazi hiyo.

Kazi ya miezi mitatu ikachukua mwaka na zaidi, baadaye daktari alichukia na kutishia kukatisha mkataba, mfinyanzi hakukasirika bali alimjibu kwa upole akimwambia;

“Daktari! Kazi zetu zinatofautiana, wewe ni daktari, unawatibu watu wanaopona na kufa. Ukifanya kosa wakati wa upasuaji hata kama ni la uzembe ukasababisha kifo, kaburi linaficha makosa yako!

“Vi vigumu mtu kuibuka baadaye na kukuhukumu juu ya kosa ulilotenda, kaburi linakulinda daima, lakini mimi nikifanya kosa la ufundi nikatengeneza sanamu yenye dosari, ipo siku nitahukumiwa kwa kosa hilo. Hivyo ni lazima kazi yangu ya ufinyanzi niifanye kwa umakini zaidi.”

“Destiny!”

“Abee!”

“Umejifunza nini?”

“Nimejifunza kuwa kazi ya uandishi haitofautiani sana na ufinyanzi. Hakuna kinachomfichia mwandishi makosa yake asipokuwa makini katika kazi yake.”

“Hivyo ndivyo ilivyo, jitahidi kuzingatia weledi katika kazi yako, kumbuka maandishi hudumu vizazi na vizazi.”

Je, nini kitaendelea? Usikose wiki ijayo.

Leave A Reply