Kwa Nini Diamond Anabagua Wanawe?

SIMBA anaiwakilisha vyema nchi ya Tanzania; siyo upande wa muziki pekee, bali hadi kupata watoto na wanawake wa nje ya nchi!

 

Ikumbukwe kwamba, Diamond Platnumz au Chibu Dangote, amebahatika kupata watoto wanne hadi sasa kutoka kwa wanawake watatu tofauti; Naseeb Junior aliyezaa na Mkenya Tanasha Donna, Dyllan aliyezaa na mwanamitindo wa Tanzania, Hamisa Mobeto na Princess Tiffah na Prince Nillan aliozaa na mwanamama tajiri wa Uganda, Zari The Boss Lady.

 

Maneno yamekuwa ni mengi juu ya namna Diamond anavyoonesha upendo wa tofauti kwa watoto hawa wanne.

Ukweli ni mchungu, lakini lazima uzungumzwe; Diamond anaonesha upendo zaidi kwa baadhi ya watoto huku watoto wake wengine wakiukosa upendo huo wa baba. Hili halipingiki na kila mmoja anajionea.

 

Staa huyu wa muziki kimataifa, yupo tayari kughairisha ratiba zake za kazi na kusafiri kuelekea ambako baadhi ya watoto wake huishi na kufurahi nao na kusheherekea siku zao za kuzaliwa huku akiwapa zawadi za kutisha wakati kwa wanawe wengine, wanaambulia tu kutakiwa heri ya kuzaliwa tena kupitia mtandao wa kijamii kama Instagram. Inaumiza na hilo lipo wazi kabisa na mashabiki wanajionea kwa macho yao kile wanachokiita skendo ya ubaguzi dhidi ya wanawe hao.

Mfano ni wakati wa birthday ya Dyllan aliyezaa na Mobeto, hakukuwa hata na pongezi za mapema za siku ya kuzaliwa ya mtoto huyo kutoka kwa Diamond hadi raia wenye hasira kali walipopiga kelele.

Ukiangalia kwa jicho la tatu, utagundua kwamba kuna tatizo la mapenzi kutofautiana kwa watoto hao. Utagundua labda ni kutokana na mama aliyemzaa mtoto huyo kutokuwa na mawasiliano mazuri na Diamond.

 

Kutokana na hilo, basi Gazeti la IJUMAA limeona likuletee listi ya watoto wanaopendwa zaidi na Diamond au Chibu na wale ambao hawapati mapenzi hayo kutoka kwa baba yao huyo;

TIFFAH DANGOTE NA NILLAN

Watoto wawili aliozaa na Zari; yaani Tiffah Dangote na Nilan; hawa ndiyo chaguo la kwanza kwa Diamond na anawaonesha mapenzi halisi ya baba kulinganisha na watoto wengine.

 

Kuna wakati Simba alipishana kidogo na Zari hivyo hakuoneha kuwajali sana watoto hao, lakini tangu wapatane, Diamond yupo tayari kufunga safari kutoka Dar, Tanzania hadi Durban, Afrika Kusini wanakoishi na kula nao bata la kufa mtu.

 

Staa huyo wa Ngoma ya Nitaanzaje, ukimuona wakati akiwa na Tiffah na Nillan, unaweza kusema ni baba bora na anastahili kujengewa sananu au kupewa tuzo ya dunia ya kuwajali watoto, maana anaonesha kuwajali na kuwathamini mno.

 

DYLLAN

Kwa upande wa Dyllan aliyezaa na Mobeto kuna utofauti mkubwa mno; jamaa haoneshi kumpenda wala kumjali kama anavyofanya kwa Tiffah na Nillan.

 

Wajuzi wa mambo wanaeleza kuwa, Chibu amemuweka mtoto huyo katika nafasi ya chini kunako moyo wake.

Ni mara chache mno, Baba T ameonekana kumzingatia Dyllan kama anavyowazingatia watoto wengine, ukizingati Dyllan anaishi eneo moja na analoishi yeye la Mbez-Beach jijini Dar, Tanzania.

 

Lakini imekuwa ni vigumu mno kufunga hata safari ya gari anayoweza kutumia chini ya dakika 15 au robo saa kwenda kumuona au kula naye bata, lakini anaweza kufunga safari ndefu ya ndege kwenda Afrika Kusini kuwaona Tiffah na Nillan; siyo sawa.

 

NASEEB JUNIOR

Kwa upande wa Naseeb Junior aliyezaa na Tanasha ambaye ndiye mdogo zaidi; Simba haonekani kuwa na mapenzi kiivyo, siyo tu kwa mtoto, bali hata kwa mama yake mwenyewe.

 

Mapenzi ya Diamond na Tanasha yalionekana kuwa ya moto mno na kila mmoja aliamini kuwa watafunga ndoa, lakini hesabu zilikataa kwa sababu mara tu baada ya Tanasha kubeba mimba, mapenzi yalianza kudhoofika. Mara tu baada ya kujifungua, kila kitu kiliharibika ndipo mwanamama huyo akafunga virago na kurudi kwao, Kenya.

 

Wataalam wa mambo wanasema kuwa, Diamond hana mawasiliano kabisa na bidada huyo licha ya kumzalia mtoto huyo ambaye kwa kiasi kikubwa amefanana mno na baba yake.

 

Cha kushangaza zaidi, ni kutokana na ukweli kwamba; Naseeb Junior na baba yake Diamond, wamezaliwa tarehe moja na mwezi mmoja, lakini Chibu hajawahi hata kuonesha makeke ya kumpa zawadi kama anavyofanya kwa watoto wake wengine.

 

Ni matumaini yetu Diamond ataonesha mapenzi mazito kwa watoto wake wote wanne, huku tukitegemea kuusikia wimbo kutoka kwake utakaowaonesha watoto wote mapenzi yake kama baba bora.

MAKALA: ELVAN STAMBULI


Toa comment