The House of Favourite Newspapers

Kwa nini Magufuli aone uozo wengine wasiuone?

0

71d6pombeTumshukuru Mungu kwa kutuamsha salama leo.
Nianze kwa kusema uamuzi wa Rais Dk. John Pombe Joseph Magufuli kueleza kwa kina namna nchi ‘inavyoliwa’ kwa kueleza safari holela za nje ya nchi zinavyoligharimu taifa mabilioni ya fedha na jinsi uhujumu unavyofanywa bandarini, kumezua mjadala mkubwa miongoni mwa baadhi ya wafuatiliaji wa masuala ya siasa nchini.

Ujasiri wa Rais Magufuli kueleza bila kificho jinsi safari za nje zinavyogharimu taifa na jinsi wizi wa kuibia nchi kupitia kodi unavyofanywa kabla ya kutangaza msimamo mkali wa kuzidhibiti, umedhihirisha pasi na shaka kuwa rais huyo mpya amedhamiria kubana matumizi ya fedha za serikali na kuziba mianya ya rushwa akiwa na nia ya kuzielekeza fedha hizo katika shughuli za maendeleo kwa nia ya kuboresha maisha ya Watanzania.

Wakati mwingine inatia uchungu unaposikia rais wa nchi akisema kwa masikitiko kuwa safari za vigogo nje ya nchi katika mwaka wa fedha 2013/2014 na 2014/2015 peke yake, taifa lilitumia Sh. bilioni 356.324 kugharimia safari hizo; kiasi ambacho kwa maelezo yake, kingetosha kujenga barabara ya lami ya urefu wa kilomita 400 na pia kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwamo ya maji, elimu na afya.
Uzuri ni kwamba rais anajua na alizitaja wizara zilizoongoza kwa kutafuna fedha za umma kwa viongozi wake kusafiri nje ya nchi.
Bila kumung’unya maneno akazitaja wizara na taasisi hizo za umma zilizoongoza kwa kutumia fedha nyingi kwa ajili ya safari za nje ya nchi kuwa ni Bunge, iliyokuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikano wa Kimataifa, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali (NAOT) na Wizara ya Mambo ya Ndani.
Huwa najiuliza, viongozi ambao wana dhamana ya kuhudumia wananchi wanaona ufahari gani kutumia mabilioni hayo ya shilingi huku wananchi wakikosa huduma muhimu kama ya matibabu? Mtu anakosa vidonge vya malaria halafu wewe kiongozi unayepaswa kusaidia jamii unatumia mabilioni hayo ya shilingi kwa anasa ni haki hiyo?
Ukweli ni kwamba fedha za umma zimetafunwa mno na tumshukuru Mungu kwa kutuletea Rais Magufuli ambaye sina shaka yoyote kwamba amekuwa mtetezi wa wanyonge wa kweli na Waziri Mkuu Kassim, Majaliwa anayeonekana kuwa mkali kwa wezi wa mali za umma.
Leo zikiwa zimetimia siku 46 tangu Magufuli aapishwe ameweka rekodi ya kuokoa kiasi cha Sh. 997.4 bilioni ambazo zilikuwa zitumike kwa matumuzi yasiyo ya lazima na ukwepaji kodi.
Sh. 997.4 bilioni zilizookolewa zitaweza kutumika kununua magari ya wagonjwa, kujenga zahanati, kujenga barabara za lami, kununua madawati, kujenga vyumba vya madarasa, kuchimba visima, kununua mashine za uchunguzi wa magonjwa, magari ya wanafunzi, pikipiki kwa maofisa kilimo, mikopo ya elimu ya juu na kadhalika.
Ukweli ni kwamba baadhi ya viongozi wanaopewa dhamana ya kusimamia rasilimali za umma hawana uzalendo na ni wabinafsi na ndiyo maana wanaibia nchi.
Inashangaza kuona watu hawaogopi kuibia taifa na wanakosa uzalendo. Mzalendo wa kweli hawezi kuona fahari kulala sehemu nzuri na kula vizuri huku Watanzania wenzake wakifariki dunia kwa kukosa dawa kwa sababu ya wizi wake.
Tujiulize, kwa nini Rais Magufuli auone wizi huo na viongozi wengine wasiuone? Kwa nini uzalendo umekufa katika nchi hii? Tufanye nini ili kila mmoja wetu awe anaumia anapoona fulani anaibia taifa kwa manufaa yake binafsi? Watanzania tuamke, tusiibiwe huku tukiona.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

Leave A Reply