The House of Favourite Newspapers

Kwa nini mapenzi yakupe huzuni kila siku?

0
Attractive couple having an argument on couch at home in the living room
Attractive couple having an argument on couch at home in the living room

Jumamosi iliyopita, nikiwa katika pilikapilika za kila siku, nilipokea simu kutoka kwa mtu aliyejitambulisha kwa jina moja la Nancy. Kwa jinsi sauti yake ilivyokuwa ikisikika, ilionesha dhahiri kwamba analia, nikashangaa kwa nini analia na kinachomliza ni nini?

Aliomba kukutana na mimi siku hiyohiyo akieleza kwamba ana matatizo mazito na anahitaji ushauri kutoka kwangu. Japokuwa nilimweleza kwamba siku hiyo nilikuwa na ratiba ngumu tupange siku nyingine, aliendelea kusisitiza huku akilia, nikawa sina cha kufanya zaidi ya kukubali ombi lake.

Saa nane za mchana, tayari nilikuwa nikitazamana uso kwa uso na Nancy, alionesha kuwa binti mzuri, mpole na anayejitambua lakini bado alikuwa analia. Macho yake yalikuwa yamevimba, uso wote ulibadilika na kuwa mwekundu, maskini! Alitia huruma.

Haikuwa kazi nyepesi kumtuliza, hatimaye nilifanikiwa kumfanya atulie

kwa sababu asingeweza kunieleza kinachomsumbua kama angeendelea kuwa kwenye hali ile. Baada ya kutulia, nancy alinieleza kilichomtokea na kusababisha awe kwenye hali hiyo. Alichonieleza ndiyo hasa kimenifanya leo nije na mada hii kwa sababu naamini wapo wengi wanaoteseka kama Nancy, pengine hata zaidi lakini hawana pa’ kusemea.

Alinieleza mambo mengi lakini kwa kifupi, alikuwa kwenye matatizo makubwa na mpenzi wake ambaye aliniomba nisimtaje jina, waliyedumu naye kwa zaidi ya miaka mitatu kwenye uhusiano wao.

Nilichojifunza kutoka kwa msichana huyo ni kwamba alikuwa na huzuni kubwa ndani ya moyo wake, kila kitu kilipoteza maana, alichokuwa anatamani kwa muda huo, ilikuwa ni kuyakatisha maisha yake ili akapumzike! Uwezo wa moyo wake kuhimili mateso ulikuwa umefikia mwisho na alichoona kinafaa ilikuwa ni kuyakatisha maisha yake.

Alinieleza kwamba kwa kipindi chote alichoishi na mwenzi wake, furaha ilikuwa kitu adimu sana maishani mwake, akanihakikishia kwamba hata mwili wake ulikuwa umepungua sana kwa sababu hakuwa akila vizuri wala kupumzika, chanzo cha yote ikiwa ni mapenzi! Bila mwenyewe kujijua, matatizo ya kimapenzi yalikuwa yamemuingiza kwenye huzuni kali ambayo kitaalamu huitwa Depression.

Kwa wanaoelewa kuhusu Depression, wengine huita msongo wa mawazo ingawa siyo tafsiri yake sahihi, watakubaliana na mimi kwamba unapokukumba, unaweza kuugua maradhi ambayo hospitali vipimo vyote vitashindwa kuonesha unaumwa nini.

Kabla ya kuendelea mbele, ningependa kila mmoja ajichunguze kwa makini kwenye maisha yake ya kila siku, ya kawaida na yale ya kimapenzi.

Je, muda mwingi unajihisi kuwa na huzuni moyoni mwako? Unahisi unatamani kulia hata bila sababu? Unahisi mwili wako uko tupu na huna matumaini kabisa kuhusu kesho?

Kuna muda unakasirika sana hata kwa sababu ndogo? Unahisi kichwa kuchanganyikiwa? Unahisi kila kitu kinakukera hata vile ambavyo awali vilikuwa vikikufurahisha? Kama ulikuwa unapenda kusikiliza muziki, kutazama tamthiliya au vipindi fulani kwenye runinga, hutaki tena?

Usiku hupati usingizi vizuri kama zamani, muda wote unahisi mwili umechoka, unajihisi kuwa na hatia na muda wote unajilaumu?

Kama jibu ni ndiyo, basi tambua kwamba na wewe ni miongoni mwa watu wanaosumbuliwa na huzuni kali ‘Depression’. Hata hivyo, japokuwa wengi hawajui, migogoro ya mara kwa mara ya kimapenzi, kuishi na mpenzi asiye mwaminifu, anayekushusha hadhi na kukudhalilisha kwa namna mbalimbali na anayeutesa moyo wako ni chanzo kikubwa sana cha Depression.

Kibaya zaidi, wengi huwa hawajui kwamba wanasumbuliwa na tatizo hilo ndiyo maana matukio ya watu kujiua, kuwaua au kuwajeruhi wengine, kusababisha madhara makubwa kwenye jamii au kuugua maradhi yasiyopona, yanazidi kuongezeka kila kukicha.

Swali ambalo nataka msomaji wangu ujiulize, kwa nini kila siku mapenzi yakusababishie huzuni na matatizo?

Kwa leo nafasi haitoshi, wiki ijayo nitaendelea kukusimulia kisa cha dada Nancy na kukupa mbinu za namna ya kuondokana na huzuni inayosababishwa na mapenzi ili hatimaye na wewe uyafurahie mapenzi kama wanavyoyafurahia wengine.

Tukutane wiki ijayo.

Leave A Reply