The House of Favourite Newspapers

Kwa Nini Rodri Na Sio Vinicius?

Usiku wa Oktoba 28, 2024 katika ukumbi wa Théàtre du Chátelet ulioko Jijini Paris, Ufaransa kulifanyika halfa ya ugawaji wa moja kati ya Tuzo zenye heshima zaidi duniani, Ballon d’Or na kushuhudia nyota kiungo mkabaji wa Manchester City, Rodri (28) akitajwa kama mchezaji bora wa dunia kwa mwaka 2024.

Waandaji wa tuzo hizo ni ‘France Football’ jarida kubwa la michezo nchini Ufaransa, na hakuna uhusiano ulioko baina yao na FIFA kwa sasa baada ya umoja wao kuvunjika mwaka 2015 na baada ya hapo FIFA walianza na kutengeneza tuzo zao za mchezaji bora wa bora wa FIFA, ijapokuwa, tuzo hizo bado hazijawa na umaarufu mkubwa kama tuzo za Ballon d’Or.

Katika tuzo iliyozua maswali mengi kwa wapenzi na wadau wa soka duniani kote, ni ushindi wa Rodri kama mchezaji bora wa dunia, tuzo ambayo baadhi ya watu wanaamini ilipaswa kwenda kwa winga wa Brazil na klabu ya Real Madrid, Vinicius Junior (24), huku wengine wakiamini kwamba Rodri amestahili, maswali yakiwa Rodri kafanya nini na Vini kafanya nini?

RODRI
Kiungo huyu mkabaji amekuwa nguzo kubwa sana kwa Man City, kwa nafasi anayocheza sio mtu anayetarajiwa kuwa namba kubwa za magoli au pasi za magoli licha ya kufanikiwa kufunga magoli 12 na pasi za magoli 14 kiujumla, ambapo katika Ligi Kuu alicheza michezo 34 na kufunga magoli 8 na pasi za magoli 9 na kushinda tuzo ya mchezaji bora wa mechi mara 3.

Kiungo mkabaji huyo akiwa na Man City alishinda mataji kama Ligi Kuu, UEFA Super Cup, Kombe la Dunia la Vilabu, na katika Timu yake ya Taifa, alifanikiwa kushinda taji la UEFA Euro 2024 na kushinda tuzo ya mchezaji bora wa michuano hiyo. Rodri pia aliweka rekodi katika michezo 63 aliyoshuka dimbani amepoteza mchezo mmoja tu, Fainali ya FA dhidi ya Man United.

VINICIUS JR
Katika msimu wa 2023/24, Vini alicheza jumla ya michezo 49, akifunga jumla ya magoli 26 na pasi za magoli 11, huku magoli 15 na pasi za magoli 5 zikiwa kati Ligi Kuu ya LaLiga, akiisaidia timu yake kushinda ubingwa wa Ligi Kuu, Ligi ya Mabingwa barani Ulaya na kombe la Supercopa de España, akishinda tuzo ya mchezaji bora wa Michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Vini alishinda tuzo ya mchezaji bora wa mechi mara mbili tu akiwa na Real Madrid, na mara moja akiwa na Brazil katika michuano ya Copa America ambapo hakuwa na msimu mzuri baada ya kufunga magoli mawili tu na timu yake kutolewa katika hatua ya Robo Fainali dhidi ya Uruguay.

Hii sio mara ya kwanza kwa mtu mwenye takwimu ndogo za magoli ya kufunga kushinda tuzo hiyo, tuzo hizo hutolewa kwa uwezo na majukumu imara aliyofanya mchezaji katika klabu yake na Timu ya Taifa kama livyowahi kushinda Luka Modric mwaka 2018.