Kwa nini uingilie ugomv i wa wazazi wako?
Asalam alaikum wapenzi wasomaji wa safu hii, nashukuru nina afya ya kutosha, kwa wewe ambaye huna afya nakupa pole Mungu atakujaalia utapona, kwa wenye misiba poleni sote tupo njia moja ni kufanya yale tulioamrishwa na muumba ili itakapo-wadia safari tuwe wasafi.
Leo nimekuja na mada hii kwa nia ya kuwaasa watoto wanaopenda kuingilia ugomvi wa wazazi pale wanapokuwa wanawaamulia kwani nimewahi kushuhudia mtoto akimjibu vibaya mzazi wake mmoja kisa tu anagombana na aidha mama yake au baba yake.
Hivi wewe unayefanya hivyo hujui kuwa hao ni kitu kimoja? Unapomtukana mmoja jua unawatukana wote, lakini je unadhani adabu inasema wawili wakigombana wewe uwaingilie kwa kumkosea adabu mzazi wako? Hebu liangalie hili kwanza kabla ya kutoa maneno machafu.
Kuna baba aliwahi kunisimulia tabia mbaya ya mkewe ambayo imekuwa ikisababisha kugombana naye na wakati mwingine kupigana lakini anashangazwa na mtoto wake wa kiume kila akigombana na mama yake yeye anamtukana na kumdharau kama vile si mzazi wake pia.
Kiukweli nilimlaumu bwana yule kwanza kugombana na mkewe mbele ya watoto lakini nikugeukie wewe kijana ambaye unaamua kabisa kumtolea maneno machafu baba yako kisa anagombana na mama.
Kijana ukiona wazazi wako wanagombana nakusihi kama unashindwa kujizuia nenda katafute watu wazima ambao wanaweza kumkalisha chini baba yako waongee naye lakini kamwe usimtolee maneno machafu.
Hivi utamwambia nini Mwenyezi Mungu ambaye amekataza hata kumgunia mzazi? Kweli umeumia kuona mama yako anapigwa? Jikaze tafuta njia ya kulimaliza tatizo lakini usimtukane mzazi kamwe.
Kumbuka wazazi ni rahisi kusameheana lakini si rahisi baba yako kukusamehe wewe, mke na mume kurumbana ni kitu cha kawaida na kitanda pekee ndiyo suluhisho la ugomvi wao.
Mbali na kitanda hata lugha laini inaweza kumfanya baba akamsamehe mama na maisha yao yakaendelea lakini mtoto utabaki kuwa mtoto tu, embu kuwa na adabu hata kama unaumia kiasi gani.
Ni kweli kibinadamu unaweza kuumia unapoona mama yako anatukanwa, kunyanyaswa au kupewa kipigo na baba yako.
Lakini hupaswi kuingilia ugomvi wao na kama utahisi ugomvi wao unaweza kuleta madhara ni vyema ukawaamulia kwa kuwasihi waache kugombana bila kutoa lugha isiyofaa kwa baba yako.
Kumbuka ukimtukana baba yako au kumchangia kumshushia kipigo na mama yako, utakuwa umefanya kosa kubwa.
Hata ikitokea mama anamshambulia baba yako kwa matusi, licha ya kuumia usithubutu kumtukana au kumpiga kwa sababu hakuna kitu kibaya na cha laana kama mtoto kufanya hivyo.
Kumbuka katika vitabu vitakatifu imeandikwa wazazi ndiyo Mungu wa duniani basi tuwaheshimu.
Kwa leo naishia hapa tuonane wiki ijayo.