The House of Favourite Newspapers

Kwa Nini Umfiche Mkeo ugonjwa ?

0

blackcouple-bedsmileAsalam Alaikum mpenzi msomaji, bila shaka unaendelea vema na ujenzi wa taifa, kwangu mimi nina majonzi ya kuondokewa na mfanyakazi mwenzangu Makongoro Oging’ lakini namshu-kuru Mungu kwani alimpenda zaidi.

Leo kwenye safu hii tutaongelea tabia ya wanaume kuficha ugonjwa kwa wake zao wakati tayari ni wanandoa kwa wenzetu Wakristo husema mwili mmoja, kisa cha kuandika makala haya ni kuelezea mkasa uliomkuta mwanamke mwenzetu ambao nimeona niulete kama mada ili kuwasihi wanaume wanaofanya hivyo waache kwa sababu haya si mapenzi bali ni roho mbaya na unaweza kujikuta unamuua mwenzako sababu tu ya kuficha magonjwa.

Kisa chenyewe kilimkuta msomaji mmoja ambaye aliniambia kuwa mume wake amekuwa akiumwa umwa kwa muda mrefu akimwambia ampeleke hospitali anakataa lakini siku moja akamfuma akimeza dawa kwa siri.

“Nililiamua kuzichunguza dawa nikagundua kuwa ni ARV, niliumia sana, nikamuita na kumuuliza kwa nini hakunishirikisha wakati tunashiriki kila kitu wote, akanyamaza na kuangalia chini, nilijikuta nikilia sana kisha nikachukua uamuzi wa kwenda kupima na kuanza dawa, nimekuambia Bi Chau ili iwe fundisho kwa watu wote,” alisema msomaji wangu.

Bila shaka umeelewa kwa nini nimeamua kuandika mada hii, wapenzi wasomaji wanaume hasahasa, kwa nini umfiche mkeo ugonjwa ulionao?  Na kwa wale wasiopenda kuongozana na wake zao hospitali mnakosea sana kama kweli unampenda unatakiwa kumlinda kwa kila hatua ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kile kinachokusumbua kama ni ugonjwa wa kuambukizwa unahakikisha na mkeo amepata dawa kwa sababu mwili wake ndiyo wako.

Sasa wewe unayeamua kujitibu halafu ukamuacha mkeo je, unakuwa umeacha kushiriki naye unyumba au ndiyo unaamua kuondoka nyumbani kwa sababu ninachojua mimi ili ndoa iwe ndoa unyumba ni lazima na kama una siri ya kiafya ni lazima umshirikishe mwenzako ili mambo yaende sawa.

Hapa nimewaongelea wanaume lakini wanawake pia wapo wanaowaficha waume zao maradhi yanayowasumbua naweza kusema mnajidanganya kwa sababu ukimuambukiza mumeo ugonjwa je, utamkwepa na kama utashiriki naye basi ndiyo hutokaa ukapona utakuwa unatwanga maji kwenye kinu.

Kwa leo naomba niishie hapa bila shaka mmenielewa nilitaka kuwaeleza ndugu zangu acha usiri kwenye uhusiano, haifai.

Leave A Reply