The House of Favourite Newspapers

Kwa nini unung’unike kwa mafanikio kiduchu?

0

young-couple-arguing-on-a-sofa-136381366849303901-130702114836Awali ya yote nichukue fursa hii kuwatia nguvu ndugu zangu Waislam ambao wako katika hatua za mwisho kumaliza mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Niwaambie tu kwamba wana kila sababu ya kutumia kipindi hiki kutubu madhambi yao na kuahidi kutomkosea Mungu tena ili na yeye aweze kuwabariki katika yale ambayo wanapanga kufanya.

Mpenzi msomaji wangu, tunazungumzia suala la mafanikio, hakika kila mmoja anatamani siku moja awe kati ya watu wenye mafanikio makubwa. Kila mmoja anataka kuwa bilionea.

Yaani awe na kipato cha kumuwezesha kuishi maisha mazuri yeye pamoja na watu wengine wanaomzunguka. Pia awe katika nafasi ya kuwasaidia wengine wenye uhitaji.

Hilo ndilo ambalo wengi wetu tunalitamani. Lakini tunatakiwa kujua kwamba, mafanikio si jambo ambalo linakuja kwa ghalfa. Kwamba eti unaweza kulala maskini na kuamka tajiri. Katika mazingira ya kawaida hilo ni jambo lisilowezekana!

Kumbuka mafanikio ya kweli yanakuja kwa hatua. Ni lazima uanzie kwenye umaskini, upambane taratibu kuelekea kwenye utajiri. Uanze na shilingi kuelekea kwenye kumiliki mamilioni. Hiyo ndiyo kanuni ya mafanikio ya kweli.

Ukitaka kuthibitisha hilo, fuatilia maisha ya wale ambao leo hii wana mafanikio makubwa duniani, utagundua wengi wao walianzia chini. Walikuwa maskini, wakajikubali kwanza kuwa wao ni maskini lakini wakauchukia.

Kuuchukia kwao umaskini kuliwafanya waanze kupambana kusaka mafanikio kwa udi na uvumba. Wakaanza kupanda ngazi kwa ngazi kuelekea kwenye mafanikio na leo hii ndiyo hao ambao wanatisha kwa ‘mkwanja’.

Sasa wakati kanuni za mafanikio zikiwa hivyo, wapo watu ambao hawatosheki na mafanikio madogo walioyano. Kwanza kama hujui nikufahamishe tu kwamba, ile kujaaliwa kuwa na akili timamu, afya njema, maarifa na nguvu za kutosha ni sehemu ya mafanikio ambapo unatakiwa kumshukuru Mungu kwa hilo.

Hivyo ndivyo vinavyoweza kukusaidia katika jitihada zako za kusaka mafanikio. Baada ya hapo, ukishaanza kuwa na uwezo wa kujikimu kimaisha, nikimaanisha kuwa na uwezo wa kujipatia mahitaji yote muhimu kama vile malazi, chakula, mavazi, matibabu na vinginevyo, hiyo ni hatua nyingine ya kuelekea kwenye mafanikio na unatakiwa kushukuru kwa kuwa wapo ambao hawana uwezo wa kupata hayo.

Baada ya hapo sasa, ukiwa na uwezo wa kujiwekea akiba benki, kwamba una uwezo wa kupata pesa zikakusaidia kwenye mahitaji yako ya msingi kisha zikabaki za kuweka akiba, napo unatakiwa kushukuru.

Kuanzia hapo na kuendelea kila hatua unayopiga mshukuru Mungu na endelea kupambana kuhakikisha unapata mafanikio makubwa zaidi.

Ninachotaka kukufahamisha leo ni kwamba, kwa hatua yoyote ya mafanikio uliyopo kwa sasa, shukuru Mungu na wala usiumie kwa kuhisi mafanikio yako ni madogo kuliko wengine. Kama huwezi kushukuru kwa kujaaliwa kuwa na nyumba yako ya kawaida kwa kuwa unatamani kuwa na ghorofa, ujue itakuwia ngumu sana kufika huko.

 Kama huwezi kushukuru kwa shilingi laki moja ulionayo benki eti kwa kuwa unatamani kuwa na mamilioni, ujue hali hiyo inaweza kuwa kizingiti cha kutimiza ndoto hiyo. Hii ni kwa sababu Mungu naye kila anachokujaalia anakupa mtihani.

Anakuangalia kwa kukujaalia hicho kidogo ambacho wengine hajawapa, utashukuru au utakufuru?

Ukishukuru, Mungu anakuzidishia lakini ukinung’unika na kujiona mnyonge hadi kufikia hatua ya kukufuru kwa kuona Mungu ana upendeleo, basi usije ukashangaa hata hicho kidogo alichokujaalia akakupokonya.

Ndiyo maana nasema, hata kama unatamani kuwa na mafanikio makubwa zaidi ya hayo uliyonayo leo, kwanza shukuru kwa hapo ulipofikia, kwani yawezekana wapo waliotamani kuwa hapo ulipo wewe lakini wameshindwa.

Tusiwe na mioyo ya kutamani mambo makubwa kwa haraka. Subira, uvumilivu na kuzidi kumuomba Mungu kila siku ili atusaidie kutimiza ndoto zetu ndilo jambo msingi.

 Ni hayo tu kwa leo, tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine. Pia niwakumbushe tu kwamba, kama una jambo lolote ambalo linakutatiza, usisite kuwasiliana na mimi kupitia namba zilizopo hapo juu.

Leave A Reply