KWA NINI WACHUMBA WANAKUPIGA KIBUTI KILA MARA ?-2

KILA mmoja anapenda kuwa na mwenzi wa maisha yake yote. Apendwe. Ampende. Hadi kifo kitakapowatenganisha. Ni hisia stahiki kabisa kwa kila binadamu mwenye pumzi ya uhai.  

 

Katika uhusiano, mengi yanaweza kutokea lakini kama tukizungumzia upande wa mateso katika mapenzi basi wanawake ndiyo hasa wanaohusika moja kwa moja katika hili. Ninaposema kuhusika moja kwa moja namaanisha kuwa, mwanamke anapoachwa na mpenzi wake ni vigumu kidogo kupata mwenzi mwingine tofauti na mwanaume ambaye uwezekano wa kumpata mwingine huwa mkubwa zaidi.

 

Zaidi ya hayo, yapo mambo mengine ikiwa ni pamoja na kupata mimba au kuachwa wakati umri wake ukiwa umesonga kiasi cha kushindwa kupata mpenzi mwingine mwenye nia ya dhati ya kumuoa na kuishiwa kuchezewa. Mateso haya mara nyingi huwaharibia wanawake wengi mipango ya maisha yao ya baadaye, kutokana na kushindwa kutimiza majukumu yao ya kujipatia kipato vyema. Hii hutokana na kuathirika kisaikolojia, hali inayowapelekea kuharibu kazi.

 

Kimsingi hapa ninacholenga ni madhara ya mwanamke kuachwa na mwandani wake, lakini mwisho wa yote hayo ni kuanzisha uhusiano na kuvunjika kila wakati, hapo sasa ndipo tunaposema kuwa mwanamke huyo hadumu na wapenzi wake. Bila shaka inawezekana kuna makosa ambayo mwanamke huyo huyafanya bila kujua kama anakosea. Lengo la kuandika mada hii ni kukutoa huko gizani ulipo hivi sasa na kukufanya uwe mpya katika ulimwengu wa fikra za kimapenzi.

 

Je, wewe ni mmoja wa wanawake ambao umeachwa hivi karibu na mpenzi wako na huna dira? Je, wewe ni mmoja wa walioachwa ukiwa hujui kosa lako au hutambui au hutaki kukubali kwamba kuna mahali uliteleza?

 

Wewe ni mwanamke ambaye unateseka, lakini si kwa kutaka bali ni kwa sababu ya mazingira lakini unataka kutoka katika mateso hayo? Mada hii ni dawa tosha kwako…hebu tumalizie mada yetu marafiki…

HUONESHI MAPENZI…

Naweza kusema kuwa hii ni sababu kubwa zaidi na yenye uzito wa kukukosesha mchumba wa kudumu. Huwezi kuwa na mpenzi ambaye huna uhakika kama ana mapenzi ya kweli na wewe au anakulaghai. Njia mojawapo ya kuonyesha kuwa ni kweli mpenzi wako unampenda kwa dhati ya moyo wako na siyo kujilazimisha ni kuonyesha mapenzi ya kweli.

 

Hebu jiulize, unaonyesha mapenzi kwa mwandani wako? Swali hili linawahusu wote, yaani wavulana na wasichana walio ndani ya ndoa na wachumba. Sijui kama naeleweka vyema ninaposema kuonyesha mapenzi kwa mwandani wako. Hapa kuna mambo mengi ikiwemo mashamsham na kuonyesha kuwa huna kinyaa kwa mpenzi wako.

 

Mwingine hata kumbusu mpenzi wake inakuwa shughuli, sasa kama hata kumbusu tu mpenzi wako unashindwa, hivi wewe una mapenzi kweli? Utakuta mwingine akiwa faragha anashindwa kumridhisha vyema au hataki kushiriki na mwenzake, huyu atakuwa anahitaji nini kama siyo kuachwa?

 

USHAURI WA BURE

Kama ni kweli una nia ya kuwa na mume hapo baadaye, lazima utulie na uishi kwa mwanaume mwenye malengo na mapenzi ya dhati. Achana na tabia za Kiswahili, usisikilize ushauri mbaya wa marafiki.

Onesha mapenzi ya kweli, mheshimu mchumba wako maana huyo ndiye anakwenda kuwa mume wako hapo baadaye. Uamuzi wa kuolewa au kumpa mshawasha mpenzi wako wa kukuoa upo mikononi mwako na bila shaka unaweza!

Kwa leo naomba niishie hapa, nawaahidi wiki ijayo nitazungumza na wavulana, USIKOSE!

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Uhusiano anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vingi, vikiwemo True Love, Let’s Talk About Love na Maisha ya Ndoa vinavyopatikana kwa oda. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha SIRI ZA NDOA YENYE FURAHA kitakachotoka hivi karibuni.

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Loading...

Toa comment