Kwa nini wanaume hawakubali kuachwa kirahisi?
Ni Ijumaa nyingine tena tunapokutana kwenye kona yetu hii, ni wajibu wa mimi na wewe kumshukuru Mungu kwa kutufanya tuendelee kuvuta pumzi.
Nakukaribisha jamvini, leo mada ni kama inavyojieleza hapo juu; kwa nini wanaume wanakuwa wagumu sana kukubali kuachwa na wanawake ambao wapo nao kwenye uhusiano wa kimapenzi?
Nimeamua kuja na mada hii baada ya kufanya utafiti kwa kipindi kirefu, nikiwashirikisha baadhi ya watu wangu wa karibu.
Katika utafiti huo, nilichokibaini ni kwamba, wanaume wengi wanapokuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na wanawake, huwa wanataka kwamba inapotokea wamekorofishana na wanataka kufikia mwisho, wanaume ndiyo wawaache wapenzi wao.
Hata kama mwanaume ndiye mwenye makosa, akiamua kuvunja mapenzi, anataka yeye ndiyo amuache mwanamke wake. Bila shaka katika jamii tunayoishi, inatokea mara kwa mara kwamba watu fulani waliokuwa wanaishi kwa kupenda, wanafikia mwisho kwa sababu moja au nyingine.
Hebu na wewe jaribu kukumbuka mifano michache, iwe ni ile ambayo imekutokea wewe au watu wako wa karibu, bila shaka utakubaliana na ninachokizungumza.
SIYO KAZI NYEPESI KUMUACHA MWANAUME
Katika utafiti huo, sikuishia tu kuangalia mifano, bali pia kuchimba kwa kina kutafuta sababu ya kinachosabisha hali hiyo. Nilichokibaini ni kwamba wanaume wana hulka ya kutokubali kushindwa kwa urahisi.
Hata kama amemkosea vipi mwenzi wake, hayupo tayari kuachwa au kukimbiwa na mwanamke kwa sababu kihulka wanaume wanaamini wao siyo wa kushindwa na jambo lolote.
Inapotokea mwanaume amefanya kila kinachowezekana kuhakikisha mwenzi wake anarudi kwenye himaya yake lakini anaonekana kuelekea kushindwa, yupo tayari hata kufanya fujo mpaka watu wote wakabaki kushangaa, yupo tayari kujeruhi, kuharibu mali na mpaka wengine wanafikia hatua ya kukatisha maisha ya wenzi wao au wanaume wanaotoka nao baada ya wao kuachwa.
Hakuna mwanaume anayeweza kuvumilia kumuona mwanamke aliyekuwa mpenzi wake, akimuacha na kuanzisha uhusiano wa kimapenzi na mtu mwingine! Sote tutakuwa mashuhuda wa kile kinachoitwa ‘wivu wa mapenzi’, kwamba wanaume ndiyo wanaoonesha kuongoza kwa kufanya vitendo vya ajabu kwa sababu ya wivu; hawataki kukubaliana na kitendo cha kuachwa.
HALI IPOJE KWA WANAWAKE?
Wakati ikiwa hivyo upande wa wanaume, hali ni tofauti kabisa upande wa wanawake. Katika utafiti wangu, nimegundua kwamba inapotokea mwanaume akaamua kukatisha uhusiano wa kimapenzi na mwanamke wake, kazi huwa siyo ngumu kama mwanamke akiamua kumuacha mwanaume.
Wanawake wengi waliowahi kuachwa na wenzi wao, watakubaliana na mimi kwamba mwenzi wako anapokutamkia kwamba hakuhitaji tena, huwa huna cha kufanya zaidi ya kuumia sana moyoni, kulia, kuhuzunika lakini mwisho wa siku unakubaliana na ukweli.
Kadiri siku zinavyokwenda ndivyo unavyoyazoea maumivu, unaanza kumsahau aliyekuumiza na mwisho maisha yanaendelea kusonga mbele kama kawaida. Inafika kipindi hata ukijua mwanaume wako baada ya kuachana na wewe anatoka na mwanamke mwingine, unaishia kuumia tu moyoni lakini unakubaliana na hali halisi.
Je, kwa nini wanaume wengi wanakuwa siyo waelewa linapokuja suala la kukataliwa na wapenzi wao? Kwa nini wanawake wanakuwa ni wepesi wa kukubaliana na hali halisi? Una mfano wa hiki nilichokiandika? Nicheki kwa namba za hapo juu, wiki ijayo tutamalizia sehemu ya pili ya mada hii.