The House of Favourite Newspapers

Kwa Nini Watoto Hupoteza Hamu ya Kula?

na DAKTARI WA RISASI & MTANDAO| RISASI JUMAMOSI| AFYA

BAADA ya wiki iliyopita kuwaelezea namna ya kutafuta mtoto wa kiume au wa kike, leo nimewaletea mada mpya ya kwa nini watoto wengi hupoteza hamu ya kula. Kukosa hamu ya kula ni tatizo la kawaida kwa watoto ambalo husababisha wazazi wengi kuwa na wasiwasi juu ya afya ya watoto wao.

Kuna sababu nyingi zinazoweza kusababisha kukosa hamu ya kula na tatizo hili linapojitokeza tunatakiwa kuwa watulivu na kujaribu kuchunguza kwa makini ni kwa nini mtoto anakosa hamu ya kula. Baadhi ya sababu zaweza kutatuliwa na mzazi au mlezi lakini sababu nyingine kama zisababishwazo na magonjwa zitahitaji msaada wa wataalam wa afya.

MAGONJWA Moja ya sababu kubwa ambayo huwakosesha watoto hamu ya kula ni aina mbalimbali za magonjwa. Magonjwa kama malaria, kuhara, maumivu ya tumbo, maumivu ya kichwa, magonjwa ya kinywa na koo, homa na mafua au dalili nyinginezo ambazo humkosesha mtoto raha husababisha watoto kukosa hamu ya kula.

MATATIZO YA KIFAMILIA

Matatizo ya kifamilia na msongo wa mawazo ni sababu nyingine ambayo huwakosesha watoto raha na hamu ya kula. Kama walivyo watu wazima watoto pia hukumbana na matatizo ya kifamilia kama kupoteza ndugu au vitu wavipendavyo. Lakini pia watoto hukumbana pia na changamoto mbalimbali za kimaisha kama majukumu ya shule au pengine kukumbana na unyanyasaji kama kuzomewa na mambo mengine mengi yanayokiuka haki zao.

Kwa hiyo ili kumuepusha mtoto na ukosefu wa hamu ya kula, wazazi na walezi hawana budi kuwa makini endapo wataona mabadiliko yoyote ya kitabia ya mtoto. Kugundua na kuweza kuziondoa sababu zinazomsababishia mtoto msongo wa mawazo, tutaweza kuwarudisha katika hali ya kawaida na hamu ya kula itarejea tena.

UGONJWA WA ANOREXIA NERVOSA

Lakini pia wakati mwingine hali hii hutokana na ugonjwa wa kukosa hamu ya kula ujulikanao kitaalam kama Anorexia Nervosa. Watoto wenye ugonjwa huu huweza kukaa muda mrefu bila kula ingawa hawana tatizo jingine na endapo watapewa chakula huchagua aina fulani tu ya chakula jambo ambalo husababisha kutopata mlo ulio kamili na hii inachangia kupungua uzito pamoja na kudhoofu kwa afya zao. Jambo hili linapojitokeza ni vyema kumpeleka mtoto kwa wataalam wa afya wa masuala ya lishe ambao watakuwa msaada mkubwa katika kumsaidia mtoto wako kurejesha tena hamu ya kula.

UKUAJI

Kiwango kidogo cha ukuaji wa mtoto huchangia kupungua kwa hamu ya kula. Katika mwaka wa kwanza wa maisha ya watoto, watoto hukua haraka lakini baada ya mwaka mmoja kiwango cha ukuaji hupungua na kiwango cha chakula wanachokula pia hupungua. Katika wakati huo, hali hiyo ni ya kawaida kwenye hatua hiyo ya ukuaji kwa watoto. Itaendelea wiki ijayo.

Comments are closed.