The House of Favourite Newspapers

‘Kwa Omog Simba wamepata bonge la kocha’

0

 

Joseph-Marius-Omog

Kocha wa Simba, Joseph Omog.

Sweetbert Lukonge na Omary Mdose
SIKU chache baada ya uongozi wa Simba kufanikiwa kumkabidhi Joseph Omog majukumu ya kuwa kocha wa timu hiyo, kocha huyo raia wa Cameroon amesifiwa kuwa ni bonge la kocha na anaweza kuifikisha mbali timu hiyo.
Kauli hizo zimetolewa na baadhi ya wachezaji wa Azam FC, timu ambayo Omog aliifundisha na kuiwezesha kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2013/2014.
Wachezaji ambao majina yao yameweka kapuni wameliambia gazeti hili kuwa kinachotakiwa ni uongozi wa Simba ni kumpa ushirikiano kwa kuwa uwezo wa Omog ni mkubwa na hawatakiwi kumuingilia.
Walisema kuwa wakati wakiwa na kocha huyo ambaye amesaini mkataba wa miaka miwili Simba, uwezo wao uliongezeka maradufu na ndiyo maana wakaweza kutwaa ubingwa kwa kuwa pia alikuwa na uwezo mkubwa wa kuwaandaa kisaikolojia.
“Alipokuwa anatufundisha tulikuwa fiti zaidi ya tulivyo sasa, yaani tulikuwa kama chuma hata ukiwauliza viongozi wetu watathibitisha hilo, kilichomuondoa hapa ni majungu tu,” alisema mchezaji mmoja.
Mwingine naye alipoulizwa juu ya ujio wa Mcameroon huyo alisema: “Kusema kweli Simba wamepata bonge la kocha, lakini itakuwa hivyo ikiwa atapewa ushirikiano, nawaonea huruma wachezaji wavivu, wachezaji nao wakijituma na kuzingatia mazoezi yake watakuwa fiti, hata Himid Mao ufiti wake umetokana na aina ya mazoezi ya Omog.”
“Kama unakumbuka msimu wetu wa ubingwa tulicheza mechi 26, tukashinda mechi 18, sare 8,” rekodi ambayo hatujaifikia hadi leo,” alisema mchezaji mwingine.
Katika msimu huo wa ubingwa Azam ilifunga mabao 51 na kufungwa mabao 14 na haikupoteza mchezo hata mmoja.

Leave A Reply